Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
RAIS John Magufuli amemmwagia sifa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwa kusema kuwa ni tofauti na viongozi wengine waliowahi kushika nafasi za juu.
Akizungumza jana wakati wa kuwaapisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Faraji Mnyepe na Skauti Mkuu, Mwanatumu Mahiza, Rais Magufuli alisema Mwinyi hana makuu na ni mnyenyekevu.
“Mwinyi amejishusha, anatambua kuna kuishi na kuna kufa, ambao wameshashika nyadhifa kubwa ni wachache sana wenye maono hayo.
“Sikusita kumteua (kuwa Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania – TSA), na niliamini kwa chombo hiki kinahitaji mzee mwenye busara kama mzee Mwinyi.
“Mimi nakuhusudu sana, ‘you are so hamble’ ni rais uliye tofauti sana, umejaliwa unyenyekevu, tutaendelea kukuombea uendelee kuishi ili busara zako tuzitumie kwa maendeleo ya taifa hili,” alisema Rais Magufuli.
Naye mzee Mwinyi ambaye alihudhuria hafla hiyo kama Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania (TSA), alisema anamhusudu Rais Magufuli kutokana na mambo anayoyafanya ambayo yanagusa moyo wake.
“Mtu anayefanya mambo mazuri ‘unamu–admire’, mimi nakuhusudu kwa sababu unafanya mambo mazuri kwa wananchi wa Tanzania.
“Mambo unayoifanyia nchi hii yanagusa moyo wangu, hili ndilo igizo la urais na wewe unamudu kufanya, wengine wanatamani kufanya… kufanya na kumudu ni vitu viwili tofauti naomba uendelee,” alisema mzee Mwinyi.
Alisema anatamani kupata fursa ya kuwa karibu zaidi na Rais Magufuli kama baadhi ya watu wanavyodhani na kwamba baadhi wamekuwa wakimfikishia maombi yao kwa nia ya kumtaka ayafikishe kwake.
“Kuna watu wanadhani niko karibu nawe sana kiasi kwamba shida zao waniambie mie ili mimi nikusogelee nikuambie hili kuna hili, fulani mfanyie hili, hayo si kweli, natamani ingekuwa kweli,” alisema.
Alikitaka Chama cha Skauti kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka kuiletea aibu nchi.
“Leo nina miaka 94, sina siku nyingi za kuiacha dunia, sitaki kwenda na aibu. Skauti muwe hadithi nzuri kwa wale watakaosimuliwa habari zenu, vinginevyo mtatutia aibu,” alisema mzee Mwinyi.
Alisema pia ameanza kusahau sahau baadhi ya maneno kutokana na umri alionao na anafikiria kutafuta mwalimu wa kumfundisha Kiswahili.
“Mfanye kwa mujibu wa… maneno mengine nimesahau, ‘rule’ mnasemaje (baadhi ya wajumbe wakaitikia kanuni), msiende upande mtanitia aibu,” alisema.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitoa wito kwa vijana kujiunga na skauti kwa sababu ina nia njema ya kujenga maadili na mshikamano kwa Watanzania.
“Katika skauti vijana wanalelewa katika misingi ya uzalendo, wanajengewa maadili mema, kujitambua, wabunifu na kuwa na moyo wa kupenda kufanya kazi,” alisema Profesa Ndalichako.
Awali Skauti Mkuu, Mahiza alisema wamejipanga kuhakikisha skauti inaendelea katika vyuo vya kati na vikuu kwa sababu kwa miaka mingi walielekeza nguvu katika shule za msingi na sekondari.
“Tutahakikisha tunafanikisha ujenzi wa kambi ya kimataifa Dodoma kwa sababu hivi sasa tuna kambi ndogo mkoani Morogoro,” alisema Mahiza.
JPM ATAKA MABADILIKO MAMBO YA NJE
Rais Magufuli alimtaka Dk. Mnyepe kwenda kuibadilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki sliyosema ina changamoto nyingi.
“Kuielewa wizara na kuyatekeleza ni mambo mawili tofauti, umeielewa nenda katekeleze… unaweza ukajua sana ‘theory’ lakini ‘practice’ ikawa haiko vizuri,” alisema.
Naye Dk. Mnyepe alisema wizara hiyo ina matatizo makubwa ndani na nje na kwamba watumishi wengi wamebweteka na kufanya kazi kwa mazoea.
“Ulipomwapisha Naibu Waziri (Dk. Damas Ndumbaro) ulisema wizara haikufurahishi na sababu zote ulizozitoa ni za kweli.
“Kuna ‘culture’ kwamba ukishaajiriwa kwenye wizara ile kituo chako cha kazi ni nje ya nchi na wanadhani ukirudishwa unatafutiwa kituo kingine cha kazi.
“Kuna makundi na mambo mengi, hivyo nitakwenda kuisimamia, kujenga utaratibu wa kazi kati ya wizara na wizara, mabalozi ndani na nje na nchi na nchi,” alisema Dk. Mnyepe.