24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Mimi mpangaji Ikulu

 ANDREW MSECHU

MWENYEKITI wa CCM, Rais Dk. John Magufuli amesema yeye ni mpangaji katika Ikulu ya Rais, lakini ataendeleza ujenzi wa Ikulu ya kisasa ya Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla ya kuwashirikisha wanachama wa CCM katika kuweka kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ikulu ya Dodoma jana, ambapo alisema kuwa hana maneno mengi lakini aliwakaribisha kwa kazi moja ya kushuhudia Ikulu yao.

“Nimewakaribisha hapa kwa kazi moja, hii ni Ikulu yenu, mimi ni mpangaji, wenye Ikulu ni ninyi. Na ndiyo maana sikubagua, hata wa vyama vingine nimeakaribisha kwa kutambua tuna wajibu wa kujenga Tanzania moja.

“Historia ya Ikulu hii mlishaambiwa kuwa inatokana na maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM mwaka 1973 yakiongzwa na Nyerere (Baba wa Taifa Mwal Julius). Yalikuwa makao makuu yawe Dodoma. Mwaka 1973 mimi nilikuwa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi Chato na maamuzi haya yakawa yametolewa.

“Si ajabu hata sikuelewa maamuzi haya vizuri. Niliingia kwenye siasa mwaka 1995 nilipochaguliwa rasmi kuwa mbunge na kwa heshima Rais Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa), akanichagua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na kukaa kwenye uwaziri kwa miaka 20. Na sikuwahi kugombea kito chochote cha NEC, kwa hiyo sijawahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wala wa NEC katika miaka yake yote nilikuwa waziri,” alisema.

Alisema hata walipokuwa wakimuomba agombee hakugombea, kwa sababu tu kwamba kama ameshindwa kumshauri Rais ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM kwenye Baraza la Mawaziri kwa nini atumie njia nyingine, hivyo akaona ametosha na uwaziri na asipoweza kumshauri kama waziri hata angekuwa mjumbe wa NEC aingeweza kumshauri na akamsikiliza.

Rais Magufuli alisema anawashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kukubali kwao kumpa nafasi ya kuwa mwenyekiti na kuwa Rais mwaka 2015 akiwa anafahamu kuwa ni kazi kubwa yenye majukumu mengi na yenye matusi na mateso lakini ameifanya kwa sababu ya nguvu zao na msaada wa Mwenyezi Mungu.

Aliwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu, wana CCM na watanzana wote bila kujali vyama na makabila kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kipindi chake cha miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake.

Mbali na hao pia aliwashukuru pia viongozi wa dini zote kwa jinsi walivyomtanguliza Mungu kwa pamoja kuliombea Taifa na mpaka sasa liko salama.

Aidha mkuu huyo wan chi, alivishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya kuhakikisha usalama nchini kwa kuwa wakati anaingia madarakani kulikuwa na matatizo katika maeneo ya Rufiji na Kibiti lakini viliweza kujipanga na kudhibiti usalama katika maeneo hayo na kuifanya Tanzania iwe ya amani.

UKUBWA WA IKULU

Rais Magufuli alisema historia ya Chamiwno imeelezwa na wameanza kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kujenga ukuta kuzunguka kilometa 27 ambao tayari umeshakamilika kwa kutumia vijana wa JKT ambao amefanya kazi kubwa.

Alisema Ikulu hiyo huenda ni kubwa kuliko zote duniani na kwamba zipo nchi kadhaa zilikuja zikitaka kuwajengea Ikulu lakini alisema hii ni dharau kwa kuwa ukimruhusu jirani aje hadi kukutandikia kitanda chako cha kulala na mke wako iko siku atafanya maajabu.

Alisema aliamua kuwa Ikulu itajengwa na Watanania ndiyo maana walifanya ukarabati na kuwaondoa wanyama katika maeneo hayo na waliyatengeneza yote yaliyoanza kutumiwa na Baba wa Taifa.

“Tumejenga pia ofisi za muda jengo la ghorofa mbili tatu pale, na makazi ya rais. Tumeamua kuiweka pia historia ya Ikulu ya Dar es Salaam ambayo Wajerumani waliijenga uniti mbili, wakaja Waingereza wakajenga mbili, Nyerere naye akajenga mbili na kufanya jumla ya uniti nane.

“Tuliamua kwamba katika kipindi hiki, Ikulu yote ya Dare es Salaam tunaihamishia hapa na kazi hiyo inafanywa na Watanzania, vijana wetu kupitia Jeshi la wananchi, kupitia JKT na mabadiliko kidogo tofauti na ile ya Dar es Salaam hii itakuwa na underground, kwa hiyo itaboreshwa zaidi,” alisema

Alisema alihakikishiwa na Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Charles Mbunge, kwamba ndani ya miezi sita Ikulu yote itakua imekamilika hivyo kuwa na Ikulu mpya mfano wa ile ya Dar es salaam ambayo imejengwa na Watanzania. 

Aliwashukuru wote walioshiriki kuteneneza historia ya Ikulu hiyo na kuwaomba wale ambao walishiriki katika historia hiyo majina yao yandikwe ili kuweka historia hiyo.

DK. MWINYI

Kwa upande wake, akizungumza katika hafla hiyo, mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema wakati wanagombea nafasi hiyo ya kupeperusha bendera ya CCM Zanzibar walikuwa 32 na sasa amebaki peke yake.

Alisema kwa mantiki hiyo vita zote huko nyuma ilikuwa ni kuhusu yeye na sasa wanakwenda kupambana na upinzani hivyo anaona maambano hayo si yake bali ni ya timu yote ikijumuisha viongozi, wanachama na wakereketwa ambao wamekuwa wakimhakikishai kuwa wako pamoja na wanakwenda kushinda 

Alisema anawashukuru wenzake waliopambana kwa kumhakikishia kuwa wako pamoja na wanakwenda pamoja kama timu ya ushindi kwa upande wa CCM.

Dk. Mwinyi alimshukuru Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo ambaye amefanya naye kazi kwa muda mrefu na kwamba anamshukuru kwa kumuunga mkono vya kutosha, yeye pamoja na wapiganaji wote.

Alisema Zanzibar kuna kazi ngumu kuliko ilivyo bara hivyo aliwaomba wawe pamoja nao kwa kuwa kazi yao ni kubwa kidogo na pamoja na kwamba itafanyika wanahitaji umoja.

Baada ya kutangazwa mshindi na kuwa mgombea atakayeipeperusha bendera ya CCM Zanzibar, Dk Mwinyi anatarajiwa kupokewa rasmi Julai 15, Jumatano akitokea jijini Dodoma baada ya kukamilika kwa mchakato wa kupata mgombea wa chama hicho.

SAMIA SULUHU

Kwa upande wake, Makamu wa Rais ambaye pia ameteuliwa kuendelea na wadhifa huo, Samia Suluhu Hassan, alisema anamshukuru Mungu kwa kumaliza vikao vyote na kupata matokeo waliyoyatarajia.

Alisema anaungana na wote huku akisisitiza kwamba sasa wanahitaji kuwa wamoja na kuungana ili kuhakikiha kuwa CCM inashinda wa kishindo.

Samia alimshukuru Rais Magufuli kwa niaba ya wanawake wote waliokuwepo na wote wa Tanzania kwa kuonesha imani yake kwao kwa kumteua yeye kuwa mgombea mwenza.

“Nguvu niliyoipata kufanya kazi na ukawa na imani na kuridhika na mimi, niliipata kwa wanwake wa CCM na wa Tanzania, lakini zaidi katika kutekeleza yale tuliyoyasimamia katika elimu, afya, kuwashusha ndoo wanawake na kuwapatia umeme katika ameneo yote ya nchi,” alisema.

Alisema anamuahidi kwa niaba ya wanawake wote wa Tanzania kuwa watafanya kazi bega kwa bega ili kuhakikisha wanakamilisha malengo ya Ilani ya CCM kwa Watanzania.

KAULI YA LOWASSA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alisema jana alipata heshima ya kusema na anafurahi zaidi kwa kuwa wako wengi wanaoshiriki katika historia ya ujenzi wa wa taifa

“Ninataka tuondoke hapa na neno linaloitwa umoja, tufute tofauti zetu zote tuurejee kama timu moja ya ushindi wa chama chetu tuungane kumtoa mpinani.

“Tushikamane kwa kuwa muda wa tofauti zetu zimekwisha na kinachobaki ni kuhakikisha tunatekelea kile walichowaahidi Watanzania,” alisema.

JOHN CHEYO 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisema alipata wivu kumuona Rais Magufuli akimuinua Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na kumpa asante kwa kumuunga mkono wakati waliomuunga mkono mwanzo kilikuwa chama chake cha UDP.

Alisema anajivunia kuwa Mtanzania kwa kuwa ndiyo nchi pekee ulimwenguni ambapo mpinzani anaweza kukaribishwa na kupewa nafasi ya kuhutubia mkutano mkubwa wa chama ambacho si mwanachama.

Alisema anawashangaa swatu wanaojiita wapinzani ambao wanatembea barani Ulaya, Amerika wakiponda nchi tamu kama Tanzania iliyo chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

“Kweli ninyi watu wa CCM mnapaswa kujivuna kwa kuwa na Mwenyekiti kama Magufuli, amewang’arisha, nasema ukweli wa Mungu, miaka mitano iliyopita mlikuwa mmesambaratika na mngesambaratishwa lakini sasa mko wamoja.

“Sisi UDP tunatangaza rasmi kuwa mgombea wetu ni Magufuli na ninawaonea huruma watakaompinga Magufuli. Ninawaomba tupate wabunge angalau watatu na tunataka madiwani na wabunge hao kwa sababu ya msingi kwamba tangu nimeanza siasa nimesema nchi hii ni tajiri na huo ndiyo wimbo wa Rais Magufuli,” alisema.

Alisema iwapo atapata wabunge wawili au watatu wakiwa bungeni watapaza sauti moja tu kuwa ni marufuku kumkopa mkulima na kwamba bila fedha hakuna mazao kwa kuwa wakulima wakiwezeshwa wanawezesha jamii inayolipa kodi kwa sababu kwa chochote watakachopata watakwenda kununua bidhaa ambazo kodi yake inaenda serikalini

Cheyo alisema hakuna chama kilichoandikishwa kama chama cha upinzani wala kwa nia ya kuiondoa CCM na kwamba ukieleza hivyo hutapata usajili, hivyo anawashangaa wanaosema waugane kuiondoa CCM.

KAULI YA PINDA

Akitoa salamu kwa niaba ya mawaziri wakuu, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema amefurahishwa na taarifa kuwa Tanznaia sasa imeingia kwenye uchumi wa kati kwa kuwa si jambo dogo.

Alisema hiyo inamaanisha kutoka katika hatua iliyokuwa inaifanya Tanzania itazamwe kwama miongoni mwa nchi maskini duniani hivyo Watanzania wana kazi kubwa mbele yao kwa kuwa bado wako katika ngazi ya chini kabisa katika nchi ambazo zinasemekana kuwa katika uchumi wa kati na kwamba juhudi zaidi zinahitajika.

Alisema ni vyema Watanzania wote waelimishwe kuwa ni nini wanachotakiwa kufanya ili kuingia rasmi kwenye uchumi wa kati.

Pinda alisema anazipongeza Serikali zote, ya Muungano na ya Zanzibar kwa kumpata mgombea wa urais na kwamba hawana shaka naye hata kidogo na wanaamini kuwa ataitendea haki Zanzibar, hivyo Watanzania wanatakiwa kuungana ili kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua.

Alisema dalili za mwanzo zinazoonekana ni nzuri hivyo kuna kila sababu kwa Zanzibar kufanya vizuri kwenye uchaguzi ujao kuliko miaka iliyopita.

BUTIKU

Aliyewahi kuwa msaidizi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye pia ni Katibu wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku alisema Rais Magufuli ni jemedari mkuu na amedhihirisha ukuu wake, na leo hakuna mashaka.

Alisema Rais Magufuli ni msomi kama wengine lakini anawazidi wengine kwa sababu anaijua nchi yake na ni shujaa asiyeogopa, anayeona mbali na asiye na mashaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles