29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM mgeni rasmi kampeni ya uzalendo

EDWIN MKENDA na TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha kampeni ya uzalendo na utaifa itakayofanyika Desemba 8, mwaka huu jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema lengo la kampeni hiyo ni kurudisha uzalendo na utaifa kwa Watanzania.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya kampeni hiyo ni ‘Kiswahili uhai wetu utashi wetu’.

“Mwaka huu tutakuwa na makongamano na kuenzi waandishi wa vitabu, waandishi wa habari na wasanii waliosaidia kukuza lugha ya Kiswahili,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema pamoja na kuwa Kiswahili kimekuwa ni lugha ya 10 kati ya 6,000 zinazozungumzwa zaidi duniani, lakini kuna baadhi ya Watanzania hawakipi kipaumbele na kukichanganya na lugha ya Kiingereza.

“Lugha hii ndiyo iliyoliunganisha taifa na lugha ya ukombozi na utambulisho wa taifa letu kimataifa,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema tafiti za Umoja wa Afrika zinaonesha itakapofika mwaka 2063 Kiswahili kitakuwa lugha kuu ya mawasiliano Afrika na kitambulisho cha Mwafrika katika mabara mengine.

Kutokana na hilo, amewataka wataalamu waliosoma lugha ya Kiswahili katika ngazi mbalimbali kujiandikisha katika Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) ili waweze kutambulika na kupata fursa za kwenda kufundisha lugha hiyo nchi za nje.

Alisema kuna mahitaji makubwa ya walimu wa lugha hiyo Afrika na nchi nyingine za mabara yote duniani.

“Mfano nchi ya Rwanda inahitaji walimu wa Kiswahili katika shule zake zote za msingi, lakini kwa sasa waliojiandikisha Tanzania ni takribani 100,” alisema.

Ameiagiza Bakita kuhakikisha kuwa na wakalimani wa kutosha wa lugha, hasa Kichina na Kijerumani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles