29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: MBARAWA CHUKUA HATUA KALI KWA WATENDAJI WAKO

Na CLARA MATIMO- SIMIYU


RAIS  Dk. John Magufuli, amemwagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, kuwachukulia hatua kali watendaji wa wizara hiyo ambao wamekwamisha miradi inayotekelezwa  na serikali katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo juzi, wilayani Busega mkoani Simiyu, baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira mjini Lamadi unatekelezwa na serikali  kupitia  mpango wa uboreshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira wa Ziwa Victoria kwa gharama ya Sh bilioni 12.83.

Alisema  hadi sasa ni asilimia 17 tu ya miradi  ya maji  nchi nzima ambayo inatekelezwa na serikali imekamilika, lakini mingine inasuasua kutokana na usimamizi mbovu  wa baadhi ya watendaji katika wizara hiyo.

“Nakuagiza Waziri Mbarawa, chunguza miradi yote ya maji ikiwemo ya visima kama utabaini kuna mradi uliokwama kutokana na uzembe wa Mtendaji yoyote mchukulie hatua, serikali haiwezi kuwa inatoa fedha tena ambazo zingine tunazikopa na baadaye tutazirudisha na riba halafu watendaji ambao wanalipwa mishahara kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wao ndiyo wawe kikwazo.

“Natambua zipo sababu mbalimbali ambazo zinasababisha miradi hiyo kukwama ikiwemo baadhi ya watendaji kuwapa tenda ya ujenzi wakandarasi ambao hawana sifa kwa kuwa wanajuana ili wawapatie asilimia fulani kwenye fedha hizo”, alisema Rais Magufuli.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Waziri Mbarawa alisema  mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi  na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (Mwauwasa)  kwa niaba ya wizara yake kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka  Shirika la  Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya(EIB).

Alisema mradi huo, unajengwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC)  ya nchini China chini ya Mhandisi Mshauri Kampuni ya Egis ya Ufaransa kwa kipindi cha miezi 24 kuanzia Mei 2017 hadi Mei 2018.

“Hivi sasa hapa kwenye mji huu wa Lamadi, mheshimiwa Rais  mahitaji ya maji ni lita milioni 1.82 kwa siku uzalishaji unaofanyika kwa siku ni lita 425,000 ambazo zinakidhi  mahitaji ya maji kwa asilimia 23 tu mradi huu ukikamilika utawezesha wananchi wote wa mji huu kupata  huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 100 maana  utazalisha lita milioni 3.3 kwa siku moja.

Mtendaji  Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD)  hapa nchini, Stephanie Mouen, alisema asilimia 80 ya ufadhili wanaotoa umejikita katika miradi ya maji ambapo alifafanua kwamba wataongeza ufadhili kwa kuzingatia vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano.

“Kiasi cha Sh bilioni 200 zitatolewa kila mwaka ili kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya umeme na maji na mradi huu ambao Rais Magufuli ametuwekea jiwe la msingi leo ni jitihada za kikanda za AFD  katika kuhifadhi vyanzo vya maji ziwa vitoria,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles