24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM KONGA ROHO YAKO, WANANCHI WATAKULINDA 

KATIKA kipindi chake cha uongozi, tangu akiwa waziri, Rais John Magufuli amejipambanua kama mtu anayechukia sana madudu serikalini. Kwa Kariba yake, anaonekana kuwa mtu ambaye linapobainika kosa au kasoro, hajali sana marekebisho yake yatafanyika vipi – anachotaka kuona yeye ni kuwa jambo hilo linarekebishwa haraka iwezekanavyo.

Hivyo, si ajabu kuona akiwatimua watu kazi mara anapopata taarifa fulani mbovu, hawi na subira. Si mtu wa kusema akae na kuipitia taarifa hiyo kwa kina. Huchukua hatua mara moja na hivi sasa watanzania wameshaanza kumzoea kwa tabia yake ya utumbuaji wa papo kwa hapo.

Lakini tabia hiyo wakati mwingine inamwingiza Rais Magufuli katika matatizo madogo madogo. Wakati mwingine anakutana na madudu ambayo anashindwa kuvumilia na kuchukua hatua hata kwa mambo ambayo awali alishaahidi kuwa hawezi kuyaingilia. Kutumbuliwa kwa Profesa Sospeter Muhongo majuzi ni moja ya mfano huo.

Sote tunakumbuka kuwa Rais Magufuli alishasema kuwa hawezi kufukua makaburi kwa sababu hataweza kuyafunika. Alitoa kauli hiyo kuwajibu watu waliokuwa wanamshinikiza achukua hatua dhidi ya madudu yaliyofanywa na baadhi ya viongozi katika Serikali zilizomtangulia.

Hili na mchanga wa dhahabu, ambalo limemwondoa Profesa Muhongo kwenye Baraza la Mawaziri, ni moja kati ya madudu ambayo yalifanywa na Serikali zilizopita. Ingawa Dk. Magufuli naye alikuwa katika Serikali, lakini wakati huo hakuwa na uwezo kama alionao hivi sasa. Ipo clip ya video ambayo bila shaka ilirekodiwa wakati akiwa waziri, inayomwonyesha Dk. Magufuli akisikitika jinsi nchi inavyoibiwa kupitia usafirishaji nje wa makinikia.

Alipochaguliwa, moja ya mambo ambayo watu walitarajia atalivalia njuga ni usafirishaji wa makinikia. Lakini aliposema kuwa hawezi kufukua makaburi, watu wakaanza kukata tamaa kuwa nchi itaendelea kupoteza katika eneo hilo.

Lakini kama ilivyo tabia yake ya kushindwa kuvumilia anapoona madudu serikalini, Rais Magufuli ameamua kuikiuka kauli yake ya kutofukua makaburi kwa amelishughulikia madudu ya sekta ya madini yaliyoanza katika serikali zilizopita.

Lakini hapaswi kupatwa hofu na kukengeuka huku kwa sababu ni dhahiri kuwa watanzania wengi watamuunga mkono kwa sababu wanaamini kuwa anafanya hivi kwa ajili ya masilahi ya nchi.

Hatari iliyopo inatokana na hamu ya Rais Magufuli kurekebisha makosa na kasoro kwa kasi kubwa. Hilo litasababisha mambo mengine yafanyike kinyume na uratibu na hilo linaweza kusababisha matatizo makubwa mbele ya safari.

Wapo watu waliojaribu kuonya kuhusiana na hili lakini wengi wamewaona kama wanapinga kile kinachofanywa na Rais Magufuli hivi sasa kuhusiana na usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Hao wanaowabeza wenzao ambao wanatoa mawazo mbadala kwa maoni kuwa hawapendi kile kinachofanywa na Rais Magufuli watambue kuwa wakosoaji hao ndio wanampa Rais nafasi nzuri zaidi ya kufanya uamuzi wenye manufaa kwa nchi.

Ni kwa kupitia ushauri wa hawa ambao wanaonekana wana mawazo kinzani ndipo Rais ataweza kufahamu kwa undani nini cha kuepuka na nini cha kufanya.

Badala ya kuanza kuwajadili watu hawa wenye mawazo mbadala, ni vema hoja zilizo katika mawazo yao zikaangaliwa kwa undani na kama kuwapinga basi wapingwe kwa kuonyesha kuwa hoja zao hazina msingi.

Naiona hatari kuwa kuna baadhi ya watu wameacha kabisa kufikiri baada ya kuona kile ambacho hawakukitarajia kikifanywa na Rais. Akili zao zote zimefunikwa na furaha na kutoamini wanachokishuhudia kiasi kuwa uwezo wao wa kufikiri umeathirika na hilo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles