23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

JPM: Kodi zetu zinatufanya tuheshimike

Na GRACE SHITUNDU-Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli ametaka Watanzania kuendelea kulipa kodi akisema ndizo zinazoimarisha uhuru wa nchi na kufanya iheshimike duniani.

Rais Magufuli ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za miaka 58 ya uhuru kesho jijini Mwanza, alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Magufuli alisema fedha zinazotumika kujenga daraja hilo Sh bilioni 699.2 zote ni fedha za ndani.

“Sh bilioni 699.2 ndiyo gharama za mradi huu, fedha zote zimetolewa na Serikali,  hatujaomba mkopo wala msaada, hatujampigia magoti mtu, hatujamlilia mtu, ni fedha za Watanzania.

“Maana yake katika makusanyo ya kodi zinazokusanywa kutoka kwa Watanzania ndio zimekuja kujenga daraja hili, ni fedha hizo hizo mnazokusanya ndio zimejenga reli, zinatoa elimu bure, zimejenga vituo vya afya 352, bwawa kubwa la umeme la Nyerere litakalotoa megawati 2,115.

 “Ndiyo maana siku zote nawaambia mtembee kifua mbele kwa sababu Watanzania ni matajiri sio masikini na mnaweza.

 “Natoa wito kwa Watanzania kuendelea kulipa kodi, inaimarisha uhuru wetu, inatufanya tuheshimike duniani, zinatufanya tufanye maamuzi sisi wenyewe,” alisema.

Rais Magufuli alisema mradi huo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa utawajenga wananchi kiuchumi katika ngazi zote za kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Wakazi wa maeneo haya mradi huu utawajenga kiuchumi mkiutumia vizuri, nimefurahi kuona vijana wengi wako hapa, jitokezeni kufanya kazi katika huu mradi.

“Wananchi mchangamkie fursa za ajira zinazoletwa na mradi huu na watakaopata ajira wafanye kazi kwa bidii na wawe waaminifu, msiibe mafuta wala vifaa, na  mama lishe na baba lishe tumieni huu mradi mtauza na mtatengeneza fedha”alisema Rais Magufuli. 

Alitoa wito kwa mkandari wa ujenzi huo kuhakikisha anamaliza mradi huo kwa wakati na ikiwezekana mapema zaidi ya walivyopangiwa.

“Nitoe wito kwa mkandarasi, wahakikishe mradi huu wanaumaliza mapema, ikiwezekana wamalize kabla ya muda, waanze kufanya kazi ikiwezekana usiku na mchana, pia wausimamie mradi huu vizuri, hii ni fedha ya Watanzania masikini”alisema Rais Magufuli.

Alisema daraja litapunguza muda wa kuvuka ziwa kutoka muda wa saa mbili hadi dakika nne na litakuwa kiungo muhimu cha usafiri kati ya jiji la Mwanzani  Geita, Shinyanga, Kigoma, Kagera na nchi jirani za Burundi, Uganda, DRC, Rwanda.

Alisema aliahidi kujenga daraja la kuunganisha Busisi na Kigongo na kusema kuwa wizara ya Ujenzi imefanya vyema kutangaza haraka zabuni ya ujenzi wa mradi huo.

Rais Dk John Magufuli akiwa na Kiongozi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Iseni B, Salma Yasini, ambaye amemkabidhi Sh. milioni  tano ukiwa ni mchango wake kusaidia ujenzi wa vyoo na madarasa shuleni hapo wakitokea kwenye sherehe za uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kigongo-Busisi  lenye urefu wa Kilomita 3.2 kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza jana.

Kuhusu suala la kilimo alisema “nimepita njiani naona mmelima kweli, hakuna njaa labda ambaye hataki kulima, atakayeona mvua inanyesha na asiende shambani na asile.”

Pia aliendelea kusisitiza amani na kusema, “Tuendelee kuitunza amani yetu, tusibaguane kwasababu ya dini, sura, mali zetu, sisi sote ni Watanzania na tuendelee kuijenga Tanzania yetu.

“Maendeleo tunayoyaona sasa hivi yanaenda kwasababu vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi, tuendelee kudumisha amani. Palipo na amani kuna maendeleo, tuendelee kuitunza hii amani kama mboni,”alisema.

Mfugale

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroad) Patrik Mfugale, akitoa taarifa ya mradi huo alisema daraja hilo ni kubwa kuliko yote Afrika Mashariki na la sita kwa ukubwa katika madaraja yote Afrika

Alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 na litakuwa na njia nne na litakuwa na nguzo 67 litajengwa kwa ubora wa kuishi miaka 100 ijayo.

Ujenzi wa daraja hiyo unatarajia kukamilika baada ya miezi 48 ikiwa ni pamoja na muda wa kujiandaa wa miezi mitatu na mkadarasi ameshaanza kupeleka vifaa.

Alisema malipo ya awali ya Sh bilioni 56.33 yatalipwa wiki ijayo na fedha za fidia Sh bilion 3.145 yapo tayari.

Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 na barabara zake za kiunganishi zenye urefu wa kilomita 1.66

Alisema daraja hili litaunganisha barabara ya Usagara, Sengerema, na Ziwa Victoria ambayo kwa sasa hadi uvuke ni lazima utumie vivuko na kutokana idadi ya magari ambayo ni magari makubwa 1600 yanapita hapo kila siku na hutumia masaa mawili na nusu au zaidi kama unakwenda Rwanda.

Akitaja idadi ya madaraja makubwa Afrika, alisema la kwanza liko Misri linaitwa 6th October  lina urefu wa kilomita 20.5, la pili ni Mainland Bridge lina urefu wa kilomita 11. daraja la tatu ni lililopo Suez Canal lina urefu wa kilomita 3.9,  la nne Linaitwa Mozambique Island lina urefu wa kilomita 3.8 na la tano lipo Msumbiji linaitwa Dona Ana lina urefu wa kilimita 3.67 na hilo la Busisi – Kigongo linakuwa la sita kwa kuwa lina urefu wa kilomita 3.2

“Serikali ilianza muda mrefu namna ya kuanza ujenzi wa daraja hili, lakini muda wote tulivyogeuka kwa hao watu tunaowaita wafadhili, walipoona urefu wake waligeuka nyuma na tulipoawambia tunahitaji japo dizaini walituambia watadizaini barabara ya Usagara kuelekea Musoma lakini kueleka Sengerema hawakutaka kusikia.

“ Wewe mwenyewe (Rais Magufuli) ulikuja ukaagiza kwani sisi si tunaweza? Ndipo mwaka 2014/15 uliagiza tuanze uandalizi wa usanifu pamoja na upembuzi yakinifu, tulifanya kazi hiyo na tuliimaliza sisi wenyewe kama Tanroad,”alisema.

Alisema katika kupata usanifu wa kina waliwaajiri kampuni ya Yooshin engineering kwa kushirikiana na Cherry engineering  ambapo walikamisha mwaka 2018 kwa gharama ya Sh bilioni  2.805.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles