31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

JPM: Kazi za dharura zielekezwe kwa majeshi

ANDREW MSECHU – dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli amewataka watendaji wake kutambua umuhimu wa majeshi likiwamo Jeshi la Wananchi (JWTZ) na kulikabidhi kazi zote za dharura pale zinapotokea.

Mkuu huyo wa nchi ambaye yuko katika ziara ya mikoa ya Kusini, alisema hayo jana baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha JKT Mlale.

 “Wakati wa amani ambao tuko salama, hakuna vita, tutumie vizuri vikosi vyetu vya ulinzi katika shughuli za maendeleo. Kwa hiyo ni vyema kazi zote za dharura watumike wanajeshi, wakati mwingine hakuna haja ya kutangaza tenda ambazo zinachukua muda mrefu bila sababu,” alisema.

Aliwataka makamanda wa vikosi vya majeshi kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kuomba kazi yoyote inayoonekana kuhitaji udharura ili kusaidia kuharakisha maendeleo ya nchi.

 “Ni vyema tenda zitangazwe, lakini pale inapotokea kwamba kuna hitaji la dharura ni vyema kutumia gia hiyo hiyo ya dharura kuharakisha mambo,” alisema.

Alisema JWTZ imekuwa mfano mzuri katika utekelezaji wa kazi pale wanapopewa maagizo kwa kuwa hufanya kwa wakati, hivyo kuyataka majeshi mengine kuiga mfano huo.

Rais Magufuli alisema ukuta wa Mererani alitarajia utajengwa kwa mwaka mzima, lakini alishangaa kukabidhiwa kazi hiyo baada ya miezi mitatu tu, huku ujenzi wa Mji Mkuu Dodoma ambako JWTZ wameshiriki ukikamilika kwa kasi.

Alisema kwa sasa tayari ameshawaagiza kutengeneza magari ya Zimamoto baada ya idara husika kusuasua kwa miaka miwili wakitafuta tenda kwa kampuni wanazotaka, ila tayari JWTZ kupitia Nyumbu wameshaanza kutengeneza magari hayo.

“Hawa hawali rushwa na inaonekana kuwa baadhi ya watendaji hawawahitaji kwenye tenda za Serikali, sasa nao waingie waombe,” alisema.

KUHUSU AMANI

Rais Magufuli alisema ni wazi kwamba kutokana na hatua za maendeleo ambazo taifa linapitia kwa sasa, yapo mataifa yanapenda kuona Tanzania inakuwa na vurugu, hivyo kuwataka Watanzania kuwa macho.

Alisema ni vyema kutambua kuwa kutokana na amani iliyopo nchini kwa sasa, Tanzania imekuwa eneo pekee ambalo ni kimbilio kutoka kwa nchi zenye vurugu kutokana na uthabiti na ulinzi wa amani yake.

“Vurugu hazilipi, ni hatari. Kama tunataka kujenga nchi ya amani yenye maisha mazuri lazima tuepukane na wale wanaotaka kutupeleka huko kwa nguvu zote.

“Kuna watu wamevimbiwa amani kama wale wanaovimbiwa na chakula au pombe, tusikubali kuwaona wakitaka kuvuruga amani yetu,” alisema.

Awali Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi, alisema hana wasiwasi na utendaji wa JWTZ kwa kuwa mipaka yote inalindwa vyema na kusababisha uhakika wa amani nchini.

“Jeshi pia limekuwa tayari kutoa huduma wakati wowote pale majanga ya aina zote yanapotokea nchini, lakini pia limepewa jukumu la ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, ambapo kwa sasa askari wetu wapo Darfur, Lebanon, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati,” alisema.

Mkuu wa JWTZ, Jenerali Venance Mabeyo, alisema jeshi hilo kupitia JKT limedhamiria kuishi ndoto ya ‘Tanzania ya Viwanda’ ya Rais Magufuli na liko tayari kufanya jitihada kuifikia.

Alisema historia inaonesha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika nchi zote duniani yalianzia kwenye majeshi, kwa hiyo JWTZ itaendeleza historia hiyo kupitia Nyumbu, Suma JKT na JKT.

“Kutokana na maagizo yako, tayari tumeshaanza kushona baadhi ya sare zetu wenyewe na tunaendelea kufanya marekebisho ili kufikia viwango vinavyohitajika,” alisema.

Alisema wakati wakitekeleza hayo, wanaendelea na jukumu lao la msingi la kuhakikisha kuwa nchi iko salama na wanafuatilia kwa karibu chokochoko zote zinazoanzishwa na watazishughulikia kikamilifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles