25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Changamoto zilizopo zisipotatuliwa na awamu ya tano, hazitatatuliwa maisha

Na Aziza Masoud-Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amewaomba viongozi wa dini kuendelea kumwombea ili aweze kupata nguvu za kutatua changamoto zilizopo nchini kwa kuwa anaamini zisipotatuliwa katika awamu hii, kiongozi atakayekuja hataweza kuzitatua.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipokuwa katika hafla ya kupokea Mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano ya Simu (TTMS), unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Alisema Tanzania ni Taifa tajiri lakini lina changamoto nyingi ambazo lazima zitatuliwe katika awamu hii kwa kuwa atakayekuja hatakuwa na uwezo wa kuzitatua.

“Taifa hili ni tajiri, lina changamoto nyingi na changamoto hizi ni lazima tuzitatue sasa, tusipozitatua katika awamu ya tano hazitatatuliwa maisha, ninaongea ukweli kama kuna changamoto zilizobaki tusipozitatua katika awamu hii sina uhakika kama atakayekuja atazitatua,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema ametoa kauli hiyo kwa sababu anaona magumu anayokumbana nayo wakati wa kutatua changamoto zilizopo.

“Katika kutatua changamoto hizi kuna magumu mengi mno, huwezi kuyataja yote ni magumu na ndiyo maana  ninahitaji nguvu za Mungu pekee kutekeleza.

“Niliwaeleza nilipoingia tu madarakani mtendaji mkuu wa TCRA (Ally Simba), nilimsimamisha  kazi na wengine  nikawatoa kabisa hapa, lawama zilikuwepo lakini tukapata mafanikio haya ya Sh bilioni 93 ambayo hata senti tano siwezi nikapewa zinaenda kwa Watanzania na hiyo ndiyo huduma kwa wananchi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuliweka Taifa katika mikono ya Mungu  kwa kuwa linapitia katika vita ya kiuchumi.

“Hii ni vita ni kama vita nyingine, vita ya uchumi inahitaji maombi  bila maombi kazi hii hatutaiweza, hao wanaokaa gizani wengi wao wanakuwa na panga, kisu au ameshikilia nyoka mfukoni,  lakini uko gizani  wao wanaondolewa kwa maombi yakuwapumbaza wasifanye walichokipanga ili sisi tuendelee kulitumikia Taifa hili,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema viongozi wanaofanya kazi katika taasisi za Serikali akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, wamekuwa wakiishi kwa vitisho kutoka kwa watu mbalimbali.

“Mtendaji Mkuu (Mhandisi Kilaba) huyu ametishwa sana na kuna mama  mmoja hapa ni mkurugenzi  naye ametishwa sana, akawa anaandikiwa barua kwamba ni Chadema, nikawaambia mimi hata kama ni Chadema, awe CUF awe CCM  ilimradi anafanya kazi yake, hapa mama wewe chapa kazi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema Serikali yake inahitaji watu wanaochapa kazi bila kujali itikadi za vyama kwa kuwa wote ni Watanzania na wapo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Wapo watu na kila siku anavaa nguo ya kijani lakini ni mwizi kuliko hata wa Chadema au wa CUF, wizi hauna dini, wachungaji hawa wanatufundisha neno la Mungu kila siku, wanahubiri mpaka wengine wanalia, lakini unalikuta jitu limenyanyuka tu linakwenda linatoa sadaka na linaondoka kimya kimya,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kama ilivyo katika maeneo mengine kwenye Serikali, pia kuna mchanganyiko wa watu mbalimbali  wakiwemo wabadhirifu lakini kwa kuwa chama chake cha CCM kinapinga mambo hayo, ndiyo maana wanajitahidi kuyaondoa ili waweze kusimamia ilani.

Mbali na hilo, Dk. Magufuli pia jana alivunja ukimya na kwa mara ya kwanza alitaja sababu iliyomsukuma kumwondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa TCRA, Ally Simba.

Alisema mkurugenzi huyo ambaye alitengua uteuzi wake Aprili 26, mwaka 2016, alishiriki kuchezea mkataba wa uendeshaji wa mfumo TTMS,  jambo ambalo lingesababisha Serikali kukosa mapato.

“Mwanzoni wakati naingia madarakani sikuridhishwa sana na utendaji wa taasisi hii (TCRA), palikuwa na mchezo mbaya sana na kweli Tanzania tumeibiwa mno, tumechapwa kweli, tumeliwa kweli nilipoingia madarakani 2015 mwishoni niliamua makusudi kutafuta mkataba original (halisi) wa huu mtambo ambao ulikuwa umefichwa na kupotezwa.

“Katika mkataba huu ambao ulisainiwa na haukuwa halisi watu wa TCRA na viongozi wengine waliondoa kwa hiyo kipengele kile cha fedha kikafutwa, nikafanya uchunguzi wangu kwakutumia vyombo vya ulinzi na usalama nikapata mkataba original (halisi), nikamtimua mkurugenzi Simba,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema baada ya kupata mkataba huo halisi, akalazimika kuupeleka bungeni ili uweze kupitishwa na ndipo akausaini ili uendelee kutumika na kuuondoa ule wa awali ambao ulichezewa.

 Aidha, Dk. Magufuli, alisema amemwongezea muda mkurugenzi aliyepo sasa kutokana na utendaji wake mzuri.

“Kuna watu wanafurahia mkurugenzi mkataba unaisha kwa hiyo nakuongezea miaka mingine mitano uendelee kushughulika nao,” alisema Dk. Magufuli.

Aidha, Dk. Magufuli, pia amemwagiza Waziri wa Fedha, Dk. Phillip Mpango, kuhakikisha taasisi zote zilizopo chini ya Serikali zinaingia katika utaratibu wa ukusanyaji fedha kwa njia ya kielektroniki ili kuondoa ubadhirifu.

Alisema mpaka sasa kati ya taasisi 667 zilizopo chini ya Serikali, taasisi 339 pekee ndizo zimesajiliwa katika mfumo huo jambo ambalo linachangia kupunguza mapato.

“Natoa maagizo taasisi zote za Serikali zenye kukusanya mapato kuhakikisha zinatengeneza mfumo wa elektroniki katika kukusanya mapato, nimeagiza pia Wizara ya Fedha kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinaunganishwa na mfumo wa ukusanyaji fedha za umma.

“Nitashangaa sana hizi taasisi baada ya hapa nitasikia kuwa bado hazijaingizwa katika mfumo huo, mawaziri mnaosimamia hizi taasisi na makatibu wakuu wa taasisi hizo kama wanaendelea kukaa bila kuunganisha maana yake wana lengo la kufanya biashara gizani.

“Kama alivyosema mheshimiwa Spika (Job Ndugai) na mimi nisingependa kuona taasisi ninazoziongoza bado zinaendelea na biashara gizani,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema wanataka kuwa na utaratibu wa utendaji wa tochi yaani wa uwazi ili kila kinachopatikana kionekane kinaingiaje na kinaenda wapi.

“Matumaini yangu waziri wa fedha utawaandikia barua na nakala umpe Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na mimi niendelee kuchungulia,  hakikisheni mnaziunganisha taasisi zote zilizobaki,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki mbali na kuonyesha uwazi pia unapunguza urasimu na vitendo vya rushwa.

“Nitatoa mfano mmoja kabla ya mfumo huu, Tanesco walikuwa kila mwaka wakilipia zaidi ya Sh bilioni 38 kwa wakala wa kuuza umeme, baada ya kujiunga sasa hawalipi hata senti moja kwa hiyo wameokoa hiyo fedha kwa mwaka,” alisema Dk. Magufuli.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli, aliwataka wananchi kutumia vizuri mitandao kwa kuwa inachangia kusababisha matatizo ikiwemo mmomonyoko wa maadili na kusababisha machafuko.

“Sekta hii kama mtu amenunua panga, jembe au kisu au bunduki vifaa vimetengenezwa ili kumsaidia binadamu kuendesha shughuli zake na kujiletea maendeleo, lakini ukikitumia vibaya  vina uwezo wa kukuletea madhara makubwa na sekta ya mawasiliano hivyo hivyo pia inaweza kuleta athari kubwa.

“Baadhi ya athari ambazo zimejitokeza ni pamoja na vitendo vya uhalifu duniani, mmomonyoko wa maadili katika jamii  na sehemu nyingine mtu anajipiga  picha yupo mtupu alafu anaposti, lakini pia  zimesababisha vurugu katika nchi nyingine mtu anaandika anahamasisha  kitendo chochote cha ajabu, nawasihi Watanzania wenzangu tujiepushe na vitendo hivi ambavyo vitafanya sekta hii kuleta madhara kwenye nchi yetu,” alisema Dk. Magufuli.

Aliwataka TCRA kuwa wakali na wasionee huruma watu wanaotumia vibaya huduma za mawasiliano badala yake watumie sheria kuhakikisha vitendo  hivi vya ovyo vinavyofanyika kwakutumia huduma ya mawasiliano vinakoma.

Pia aliwataka TCRA kuharakisha zoezi la usajili wa laini za simu kwa njia ya  kielektroniki (biometric), ili kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Kilaba, alisema chimbuko la mtambo huo ni shinikizo la Bunge na Serikali baada ya kushuhudia gharama za kimataifa zinashuka mara kwa mara hali ambayo ilikuwa inapunguza mapato ya kampuni za simu na Serikali.

Alisema katika kutekeleza mradi huo, TCRA ilitafuta mkandarasi na kusaini mkataba wa uendeshaji wa mfumo huo, Machi 2013.

“Mkataba huo ulifanyiwa mapitio  yaliyokuwa na lengo la kuweka mkazo zaidi wa kiufundi, mkataba ulianza 2013  na ulikuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi kwa muda wa miezi sitini hivyo umemalizika kuanzia Oktoba 2013 ukamalizika Septemba 2018,” alisema Mhandisi Kilaba.

Alisema katika mkataba Serikali imepata Sh bilioni 93.66 ambazo zimeshawasilishwa.

Mhandisi Kilaba alitaja kazi za mfumo huo ni pamoja na kugundua mawasiliano ya simu ya ulaghai, kuhakiki mapato yote ya watoa huduma za mawasiliano, kutoa takwimu zinazohusiana na matumizi ya huduma za mawasiliano yaani simu za sauti, matumizi ya data na jumbe fupi,” alisema Mhandisi Kilaba.

Alisema mfumo huo pia unafanya kazi ya kutambua taarifa za laini ya simu na namba tambulishi za kifaa cha mawasiliano.

Aliongeza kazi nyingine za mfumo huo ni kubaini na kufungia simu zenye namba tambulishi zilizonakiliwa na kutambua mapato na takwimu za miamala ya fedha mitandaoni.

Alisisitiza kuwa mfumo pia utasaidia kupatikana kwa takwimu za mawasiliano ya simu yanayofanyika ndani na nje ya nchi na kusimamia ufanisi bora wa huduma za mawasiliano jambo ambalo litaboresha viwango vya huduma hiyo.
Alisema mfumo wa TTMS ambao pia  unaweza kusimamia shughuli nyingi zaidi kutokana na mazingira na mabadiliko ya teknolojia zinapojitokeza ulianza kufanya kazi rasmi Oktoba mosi 2013.

Kwa upande wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango, alisema kukabidhiwa kwa mtambo huo kumefanya Serikali kuongeza chanzo cha mapato.

“Tumepata chanzo kipya kupata bilioni 93.66, utaratibu wa kulipa kodi duniani kwa sasa na duniani kote ni mfumo wa mlipa kodi kujikadiria mwenyewe kwakupeleka taarifa za makadirio ya kodi na ushuru, kabla ya mfumo huu TRA ilikuwa inashindwa kuhakiki mapato yake kwa ufanisi, mfumo wa TTMS umekuwa nyenzo muhimu ya nyongeza ya kiukaguzi Januari hadi Desemba 2018, miamala ya fedha trilioni 181.2 ongezeko la asilimia 35.2,” alisema Dk. Mpango.

Naye Spika wa Bunge, Ndugai, alisema awali kabla ya kuwapo kwa mtambo huo kulikuwa na mijadala mikubwa ambapo baadhi ya wabunge walikuwa wanataka kujua kwanini kodi zinazopatikana katika makampuni ya simu ni ndogo hasa walikuwa wanaangalia nchi jirani.

“Kuna nchi jirani ambayo ilikuwa na watumiaji wadogo wa simu kushinda sisi lakini mapato yao ni makubwa kuliko sisi, tukaamua kutengeneza sheria kwa wakati ule hatukufanikiwa lakini ulipoingia ukaagiza ipelekwe bungeni ikasainiwa. Bila hii isingewezekana, wanapenda giza sasa hii ni tochi  jambo hili lina faida nyingi, hii ni ishara ya kazi zinazofanywa na Bunge na uthibitisho tu kwamba Bunge letu si dhaifu,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles