28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awashtukia wanaomlilia

Elizabeth Hombo Na Ramadhan Hassan

RAIS Dk. John Magufuli amewapiga marufuku watu wanaomlilia kwenye mikutano yake wakitaka awasaidie akisema Serikali haina fedha za bure.

Alitoa kauli hiyo jana baada ya kuweka jiwe la msingi katika stendi ya kisasa ya Nzuguni jijini Dodoma.

Alisema watu hao ambao wamekuwa wakienda kwenye mikutano yake wakilia wakidai wana shida, wawe wanaanza kulia kuanzia katika nyumba zao na kwamba yeye hadanganyiki.

Alisema anazo taarifa za baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimdanganya ili awape fedha.

“Serikali haina fedha za kutoa bure mnafahamu tunapokuwa kwenye mikutano hivi mwingine anajiliza ametoka nyumbani hajalia ila akifika hapa ndio analia si angelia toka nyumbani hadi hapa ukifika machozi yanakuwa yamekauka.

 “Unatembea vizuri unaimba halafu ukifika hapa haaaaaa wala siwasikilizi sidanganywi, wala sidanganyiki wewe utalia hapa ukienda nyumbani utanyamaza.

“Nataka niwaambie ukweli ndugu zangu ni lazima Dodoma tuijenge hatuwezi kuchelewa kujenga Dodoma kwa mipango ya ovyo ovyo,”alisema Rais Magufuli.

AIKOSOA TBA 

Wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Wilaya Chamwino mkoani Dodoma utakaogharimu Sh bilioni 3.4, Rais Magufuli alikosoa ushauri uliotolewa na Wakala wa Majengo nchini (TBA).

Kutokana na hilo, alimtaka Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Charles Mbuge kuwaweka mahabusu wataalamu wa TBA watakaochelewesha ujenzi huo.

“Hizi hela zimetoka siku nyingi maendeleo ya kazi hayaridhishi nasema kweli au uongo?”alihoji Rais Magufuli huku akisema awali zilitolewa Dola za Kimarekani 1000 sawa na Sh bilioni 2.4 huku Hazina kukiwa na salio la Sh milioni 995.

Alisema awali ujenzi huo ulitolewa kwa TBA lakini walikuja na makisio ya Sh bilioni 6 kiasi alichosema ni kikubwa kuliko makisio ya Serikali.

“Sasa hospitali za wilaya tunaweka Sh bilioni 1.5, hapa maana yake ni kama hospitali mbili na nusu. Vituo vya afya tunatumia Sh milioni 500 na panakuwa na majengo matano hadi sita. Kwanini hapa eneo moja iwe Sh bilioni 6?

“Sasa kwa sababu mmenikaribisha kuweka jiwe la msingi na mimi mwenyewe niko hapa hata nikiwa nafanya mazoezi tutajuana vizuri. Kwanini mlichelewesha ujenzi,”alihoji Rais Magufuli.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alimwonya mkurugenzi wa TBA huku akihoji sababu za jengo hilo kuwa na lifti wakati ni la ghorofa moja.

Akimjibu kiongozi huyo wa nchi, mkurugenzi huyo wa TBA alisema awali walikusudia kuweka lifti lakini akasema jambo hilo litatekelezwa fedha zitakapopatikana.

Majibu hayo yalionekana kutomridhisha Rais Magufuli ambapo alisema: “Sasa katika jengo la ghorofa moja lazima uweke lifti? Kwa hiyo wewe unahitaji lifti au unahitaji hospitali ya kutibu wagonjwa.

“Nisikilizeni wewe mkurugenzi pamoja na Brigedia Jenerali hawa wakiwachelewesha si una ma MP? Ukiona wanakuchelewesha weka ndani. Nataka jengo likamilike tunachelewa,”alisema Rais Magufuli.

Akitoa mfano wa nyumba za Serikali zilizojengwa eneo la Mbweni jijini Dar es Salaam, akisema pia TBA walileta makisio yao aliyosema yangechelewesha ujenzi.

“Kule Mbweni wakaanza kutoa makisio niliwazuia kwenda kule na nyumba zikajengwa mpaka leo zipo. Kwa hiyo wakianza kuwachelewesha msikubali. Kwa sababu hata jeshini kuna mainjinia, kwani mpaka mshauri wa ujenzi  atoke TBA,”alisema Rais Magufuli.

AWAONYA VIGOGO POLISI

Akiweka jiwe la msingi katika mradi wa nyumba za askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) zilizopo Nzuguni, Rais Magufuli aliwataka maofisa wa polisi kuwaacha askari wa vyeo vya chini kufanya shughuli zao.

Katika hilo, alisema maofisa hao wanatoa maagizo askari wa vyeo vya chini wanapowakamata watuhumiwa.

“Tuwaache askari wa chini wafanye kazi nadhani ujumbe umefika,”alisema Rais Magufuli.

Alisema atafanya mkutano na askari wa vyeo vya chini bila kuwepo kwa maofisa wao, ili wazungumze mambo yanayowahusu.

Wakati huo huo, Rais Magufuli, aliwapa ofisi jeshi la polisi jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya jeshi hilo na serikali kuhamia jijini humo.

Ofisi hiyo ni jengo la ghorofa nne lililokuwa linatumiwa na Uwasa ambapo yatakuwa makao makuu ya jeshi hilo. 

“IGP nimefurahi umesema umehamia hapa Dodoma, ningeshangaa kuona mimi nimehamia hapa wewe bado hujahamia, ningeteua IGP wangu wa hapa Dodoma.

“Lakini kwa sababu umewahi umehamia hapa nakushukuru na kwa sababu umehamia kufanya hivyo kwa sababu askari hasubiri nyumba nimeamua kuwapa zawadi.

“Si hela mimi sitoagi hela nimeamua kwa vile mmeshatekeleza wito wa kuhamia hapa na sitaki kujua mmehamia wapi inawezekana mnakaa kwenye miembe kwenye nini.

“Lakini jukumu lenu mmelifanya la kuhamia hapa nimeamua kuwapa jengo moja kubwa lenye ghorofa nne lililokuwa linatumiwa na Uwasa.

“Sasa ndiyo yatakuwa Makao Makuu ya Polisi na ninakupa picha zenyewe ni matumaini yangu leo (jana) nitaona makao makuu ya polisi kwenye jengo hilo,”alisema Rais Magufuli. 

Vilevile alisema Serikali imehamia Dodoma na hakuna lugha nyingine kwamba watahamia, hapa ndiyo makao makuu hakuna jingine na watabanana hapo hapo kwa wagogo hakuna namna.

“Dodoma inapendeza, Dodoma inavutia na katika miaka michache ijayo jiji hili litaipita hata jiji la Dar es Salaam na majiji mengine,”alisema Rais Magufuli.

DODOMA KUWA KAMA ULAYA

Aidha alisema Serikali inajenga uwanja wa kisasa wa Msalato kwa gharama ya Sh bilioni 500 ambapo alidai anataka Dodoma liwe Jiji la mfano na ndoto za baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ziwe ni za kweli.

“Tunataka Dodoma hata Ulaya waijue tunataka liwe Jiji la mfano na kwamba ndoto za baba wa Taifa zilikuwa ni za ukweli.

Alisema pindi miradi ambayo inajengwa jijini Dodoma itakapokamilika litakuwa ni Jiji la kisasa ambalo kila mmoja atapenda kulitembelea.

“Ni matumaini yangu miradi hii itakapokamilika litakuwa ni Jiji la kisasa Stand hii ni ya aina yake tumepanga kuunganisha katika reli ya kisasa ili pawe na ‘Special’ treni ya kuja hapa lakini tutaunganisha mpaka katika uwanja wa ndege wa Msalato na pia tunaunganishja na Mji wa Serikali wa Mtumba,”alisema.

UDANGANYIFU

Aidha, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya watu kutokana na fursa ya Serikali kuhamia Dodoma wamekuwa wakifanya udanganyifu ili waweze kupata viwanja vya bure pamoja na kutaka walipwe fidia.

“Katika maendeleo yoyote changamoto hazikosekani Mkuu wa Mkoa ameeleza kwamba mlipoamua Makao Makuu yawe Dodoma lazima changamoto ziwepo lakini zipo za ukweli na za uongo.

“Wapo wengine wanafikiri hii ni fursa ya kutengeneza hela za bure za Serikali wanajidanganya sana kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na sheria ya vijiji ya mwaka namba 5 ya mwaka 1995 kifungu namba 3 (G).

Alisema sheria hizo  zinaeleza kwamba ardhi ya mtu ikichukuliwa na kama ilikuwa ni ardhi yake ni lazima alipwe fidia lakini ardhi ya mtu ikichukuliwa ambayo sio yake akikaa pale kwa kuvamia hawezi kulipwa fidia ila anatakiwa alipe fidia ni kwanini alivamia pale.

“Kwamba Mkuu wa Mkoa ameeleza mengi zile nyumba za Kisasa nilieshiriki kuzijenga ni mimi nikiwa Waziri wa Ujenzi watu wote pale walilipwa fidia.

“Na baadhi ya viwanja vya Serikali vilipotea kwa watu na wapo viongozi walivibinafsisha vile viwanja wakati ni mali za Serikali ukisikia leo mtu akijitokeza anadai fidia kwenye nyumba za Kisasa unashangaa kwa sababu mimi nilizilipa zote na ‘Document’ ilisainiwa mpaka kwa Mkuu wa Mkoa.

“Eneo hilo lote na lile la Polisi ukiona mtu anajitokeza anadai fidia utamshangaa kwa sababu eneo hili lilikuwa mali ya Serikali na polisi walikuwa wakifanya mazoezi ya ‘Range’ sasa ndio walikuwa wanakaa humo na bunduki zikiwa zinapigwa hata nyani walikimbia

“Kwa hiyo ni lazima tufike mahali tuelezane ukweli ukianza kusema kila mahali ni pako ila wapo wachache kule Chamwino tutaanza kuwalipa lakini asilimia 90 tumeishalipa wamebaki wachache.

“Nataka niwaambie Dodoma kuwa makao makuu kisiwe chanzo cha kuitapeli Serikali hiyo haitawezekana na Serikali ina njia zake za kufanya kazi na utapeli ni kosa la jinai kwa hiyo watu wadai maeneo wanayostahili na ndio maana nikawaletea viongozi hapa makini mkuu wa Mkoa nimemtoa Songea nikamleta hapa.

MATAPELI

Pia Rais Magufuli alidai kwamba pamejitokeza matapeli ambao wamekuwa wakidai kwamba wanauwezo wa kudai ardhi ambapo alisema watu hao ni matapeli na wanatakiwa kuangaliwa kwa umakini.

“Pamejitokeza matapeli wanaojifanya na wanajichangia hela kwamba mimi ndio nitakuwa Mwenyekiti wa kudai uenyekiti wakidai ardhi, umeupata wapi wewe,wale ni matapeli wanawalia hela zenu.

“Nataka niwaambie ukweli hata Dar es salaam walijitokeza wakati tunajenga barabara ya Ubungo hadi Kimara wakatupeleka Mahakamani tukashinda walijitokeza Mawakili wa ajabu ajabu mpaka leo hawajalipwa na hela zimeliwa,tujiepushe na matapeli,”alisema.

WAMACHINGA

Katika hatua nyingine Rais,amelitaka Jiji la Dodoma kutowatoza fedha wafanyabaishara wadogo wadogo maarufu kwa jina la wamachinga ambao watakuwa wakifanya biashara katika stendi mpya ya Nzuguni bali kitambulisho cha mjasiriamali ndio kinatakiwa kitumike.

 “Bahati nzuri mimi nakaa hapa hapa nitakuwa napita nawaangalia kwa sababu hizi fedha ni zao hizi hela sio za Jiji kwa hiyo hata wale watakaopewa bei iwe nzuri isiwe ya kuwakomoa.

ATOA ONYO KWA MKANDARASI

Pia alimtaka Mkandarasi ambaye ambaye anatekeleza miradi ya soko la stendi kuhakikisha anaimaliza kwa wakati mara baada ya kuongezewa muda.

“Nitumie fursa hii kumwomba Mkandarasi ambaye anatekeleza miradi hii miwili kuhakikisha anaikamilisha kwa muda uliopangwa nimesikia kwenye taarifa kwamba miradi  hii imeanza kutekelezwa Julai 2018 na ilitakiwa kukamilika Disemba.

“Lakini sasa ameongezwa muda hadi Februari 15, 2020 nimekaa Wizara ya Ujenzi kwa miaka 17 haiwezekani miradi mwili iongezewe ‘Extended’ ya aina moja inayolingana kwamba huu ulichelewa mwezi mmoja na ule umechelewa mwezi mmoja.

 “SOKO KUITWA NDUGAI

Aidha,Rais alisema soko la kisasa aliloweka jiwe la msingi litaitwa jina la Ndugai kutokana na Spika wa Bunge,Job Ndugai  kukubali kupitisha azimio na sheria ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi.

“Lile soko liitwe kwa jina la Ndugai kwa sababu Ndugai ndio Spika wa Bunge lakini Ndugai wakati tunapitisha azimio na sheria kuwa Makao makuu ya Nchi yeye alikuwa Spika angeweza kulipinga lakini yeye aliruhusu kwa hiyo ile soko litaitwa Ndugai.

Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro alisema ametoa takwimu za matukio ya uhalifu nchini ambapo kwa ujumla yamepungua kwa asilimia 24.9.

IGP Sirro alitoa takwimu hizo katika uzinduzi wa ujenzi wa nyumba 118 za polisi zinazojengwa jijini humo eneo la Nzuguni.

“Hali ya uhalifu nchini kwa sasa imepungua sana licha ya changamoto ya matukio machache ya kihalifu lakini ambayo hata hivyo yameendelea kudhibitiwa kwa nguvu kwa ushirikiano wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama.

“Takwimu za uhalifu makosa ya jinai katika kipindi cha miaka minne ya utawala wako, makosa makubwa ya jinai kwa ujumla wake yamepungua kwa asilimia 24.9.

“Lakini makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu yamepungua kwa asilimia 54.2, kwa makosa ya usalama barabarani kwa asilimia 69.4 kwa takwimu hizo tangu uingie madarakani uhalifu umepungua sana,”alisema.

Alisema kushuka kwa uhalifu ni matunda ya mchango mkubwa wa Rais Magufuli katika kuhakikisha watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama wanapata mafunzo, vifaa, motisha na mahitaji mengine muhimu. 

 “Mheshimiwa Rais, nikuhakikishie hata uchaguzi ulioko mbele yetu utafanyika salama Jeshi la polisi tumejipanga vizuri pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles