25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AWAASA VIONGOZI WA DINI

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, amewataka viongozi na waumini wa madhehebu  ya dini mbalimbali kujiepusha na migogoro inayoharibu sifa na heshima ya dini.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana alipohudhuria ibada ya kuwekwa wakfu  Askofu wa tano wa Kanisa la Anglikana  Dayosisi ya Dar es Salaam, Askofu Jackson Sosthenes Jackson katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano, Dar es Salaam.

Alisema Serikali haina dini, lakini watu wake wanaheshimu viongozi wa kiroho hivyo wakiwa na migogoro yao wanashindwa pa  kukimbilia.

“Viongozi wa Serikali tunasikitishwa na uwepo wa migogoro katika madhehebu ya dini, tunapata mashaka kama kweli viongozi wa madhehebu husika wanazingatia matakwa ya uchungaji,’’ alisema.

Huku akinukuu mistari ya Biblia kutoka kitabu cha Nabii Tito, inayoeleza ili mtu awe askofu anatakiwa kuwa na sifa za kutokuwa mlevi, asiwe mgomvi, mpenda mapato ya aibu, awe mtenda mema na apate kuonya watu kwa mafundisho.

“Niliposoma haya maandiko, nikagundua askofu umepewa  kazi kubwa ambayo unatakiwa kama kiongozi wa kiroho kuwasimamia watu wako.

“Licha ya Serikali kutokuwa na dini, kama sisi huku viongozi, nikiwamo mimi napenda kusikiliza mawaidha ya dini ya Kikristo na Kiislamu  na kuyafuatisha, kukiwa na migogoro midogo midogo huwa hatufurahii, najiuliza nitakimbilia wapi? alihoji Rais.

Alisema hakuna kazi ngumu kama viongozi wa dini kuongoza watu waliogawanyika na wakaweza kwenda sawa.

Hata hivyo, alisema kwa hatua iliyofikia sasa ndani ya kanisa hilo, ni ishara kubwa shetani ameshindwa na migogoro iliyokuwapo imemalizika baada ya kuona viongozi mbalimbali wakimo maaskofu kutoka kila eneo wamehudhiria sherehe hiyo.

“Tayari shetani ameshindwa na kulegea moja kwa moja, askofu fanya kazi yako, uwasamehe wale waliokosea kufanya kazi ya kumpendeza Mungu kama ambavyo maaskofu waliotangulia walivyokuambia katika mahubiri yao,’’ alisema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli alimpongeza Askofu Mkuu  wa Kanisa la Anglikana, Dk. Jacob Chimeledya kwa kuumaliza mgogoro uliokuwa ukilikabili kanisa hilo na hatimaye kufikia hatua ya kumuweka wakfu Askofu mpya wa Dayosisi ya Dar es Salaam.

Donard Mtetemela

Askofu Mkuu mstaafu wa kanisa hilo,  Donard Mtetemela amemtaka Askofu Jackson kutovaa viatu vya kiongozi yeyote aliyepita maana havitamtosha badala yake vitampwaya.

Alimtaka kuongoza kama alivyobarikiwa kwa kumpendeza Mungu, kufuata kwa matendo mema mahubiri yake, kusamehe waliokosea na hata kuwasimamia wanakondoo wake vyema.

Pia alitoa simulizi ya kumbukumbu ya uongozi wake alivyowahi kupatwa na majaribu alipoingia ofisini kwa mara ya kwanza.

Alisema aliingia mgeni mmoja  ambaye naye ni Canon, alipofika alimuomba nauli ili arudi alipotoka, akamjibu hana nauli kwa maana yeye hakumwita.

“Nilimjibu sina nauli, siwezi kukupa kwa kuwa sikjakuita, yule Canon akasema maneno machafu dhidi yangu, kisha akafunga mlango na kuondoka zake, nilipoona hivyo nilinyanyuka nikafunga mlango na kwenda kukabidhi funguo ya ofisi kwa viongozi wangu nikaondoka.

“Baada ya hapo nilifuatwa na askofu kiongozi wangu alinieleza nilipelekwa pale kwa ajili ya kuwa kiongozi mkubwa wa kiroho, kukomaa na alinitaka kuwa na ngozi ngumu,’’alisema.

Alimtaka Askofu Jackson awe na ngozi ngumu na nene itakayoweza pambana na hali yoyote ikiwa ni pamoja na kukwepa mishale ya sumu na kuendelea kumtumikia Mungu.

Alisema kuna viongozi wa dini wanadiriki kuhonga fedha ili waweze kuwa viongozi jambo ambalo si sahihi.

Alisema katika kuongoza kanisa, migogoro inakuwa inapikwa na shetani, si vyema akapewa nafasi atawale.

“Shetani anajua ana muda mchache, anatumia muda wake vizuri au niseme vibaya, sisi hatupigani na wanadamu tunapigana na shetani amekuja, migogoro katika kanisa ni kazi ya shetani,’’ alisema.

Alisema migogoro haihusu Anglikana peke yake, hata walipokuwa na migogoro wao waliguswa makanisa yote yanayotii jina la Yesu.

“Sisi Angilikana tulivua nguo hadharani tukasema ushoga hapana, kuna watu ndani walikuwa mashoga hawakutaka kujiweka hadharani ila hapa nasema kama ukivaa nguo chafu ndani, nje safi ukatoka jasho ni lazima uchafu utaonekana tu,’’alisema Askofu Mtetemela.

Naye Askofu Jackson, alisema atafanya kazi kwa kuleta matumaini mapya katika dayosisi hiyo.

Alimuomba Rais Dk.Magufuli kuwarudishia Shule ya Sekondari ya Minaki ili waweze kuijenga kwa pamoja na kuendelea kutoa huduma.

Aliahidi kusimamia mali zote za kanisa kwa kufuata Katiba ya Kanisa ya nchi sambamba na kuimarisha vyombo mbalimbali vya kimaamuzi

Dk. Jacob Chimeledya

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya aliiomba Serikali kuthibitisha uhalali wa usajili kwa taasisi za kidini .

Alisema kuna taasisi za kidini zinaanzishwa kiholela kwa lengo la kuchafua Kanisa lingine hivyo vyombo vinavyohusika serikalini vinatakiwa kuwa makini na hilo.

Sherehe hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbaimbali, akiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe mama Anna, Naibu Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson, Jaji Mkuu mstaafu Augustino  Ramadhani, Jaji Mkuu mstaafu Joseph Sinde Warioba, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Utawala Bora, George Mkuchika na maaskofu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles