24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM atumbua vigogo sita, wengine wachunguzwa

Na WAANDISHI WETU-UKEREWE/DAR

MJI wa Ukerewe na vitongoji vyake jana ulizizima kwa simanzi wakati wa shughuli za mazishi ya miili ya marehemu waliofariki dunia kwa ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere, iliyotokea Septemba 20, mwaka huu.

Hata hivyo saa chache baada ya maziko ya watu tisa ambao miili yao haikutambuliwa kuzikwa na serikali katika Kijiji cha Bwisya wilayani Ukerewe, Rais Dk. John Magufuli, alitangaza kuivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kwamba bodi hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti wake Brigedia Jenerali mstaafu Mabula Mashauri imevunjwa kuanzia jana wakati kamati ya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ikiendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.

Brigedia Mashauri, aliteuliwa kuongoza bodi hiyo Oktoba mwaka jana na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa pamoja na wajumbe wengine watano.

Profesa Mbarawa aliwateua wajumbe hao wa bodi kuongoza bodi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Oktoba 16, mwaka jana.

Wajumbe wa bodi iliyotumbuliwa na Rais Magufuli ni Mhandisi Emmanuel Saigurd, Profesa Zakaria Mganilwa, Veronica Matikila, Mhandisi Stephen Makigo na Yona Mwampagatwa.

IDADI YA WALIOFARIKI

Aidha ilielezwa kuwa miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo imeongezeka na kufikia 224.

Akitoa taarifa za ajali jana wakati wa shughuli za mazishi yaliyofanyika jana eneo la Shule ya Sekondari Bwisya mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema kivuko hicho kilikuwa kimebeba watu 265 wakati uwezo wake ni kubeba abiria 101.

Akitoa mchanganuo wa vifo, Waziri Kamwelwe alisema wanawake 126, wanaume 71, watoto wa kike 17, watoto wa kiume 10 na kufanya jumla ya maiti 224.

Alisema miili 219 iliyotambuliwa yote ilichukuliwa na kwenda kuzikwa na ndugu zao, wanne walikuwa hawajatambuliwa na wamechukuliwa vipimo vya DNA ili ndugu zao watakapofika waweze kutambua kuwa wamepoteza ndugu.

“Miili mingine mitano iliyotambuliwa ndugu zao waliamua kuungana nasi katika mazishi haya lakini kuna huyo mmoja tuliyempata sasa hivi taratibu zitaendelea baadaye,” alisema Kamwelwe.

“Idadi ya 265 inatokana na waliofariki kuwa 224 na waliookolewa 41. Hata hivyo, shughuli za uokoaji zinaendelea,” alisema.

Akizungumzia mchanganuo wa fedha alisema fedha zilizochangwa na wananchi ili kusaidia shughuli za mazishi ni Sh milioni 190.

“Mpaka sasa pesa zilizochangwa na wananchi ni Sh190 milioni ili kusaidia katika shughuli hizi. Mbali na hilo Serikali pia iko katika mpango wa kununua vivuko salama ili wananchi waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi,” alisema.

HALI YA KIVUKO

Akielezea hali ya kivuko Waziri Kamwelwe, alisema kivuko hicho cha MV Nyerere kilichotengenezwa mwaka 2004 na kuanza kazi mwaka huo huo kilifanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 2015 na kurejeshwa katika hali ya upya.

Alisema waliona injini zake zilianza kupata uchakavu na Julai mwaka huu waliweka injini na gia boksi mpya na hakikuwa na tatizo lolote la kiufundi hadi taarifa za kupata ajali wiki iliyopita Septemba 20 saa 8.10 mchana zilipotolewa.

Alisema kwa hatua ya dharura wamezungumza na uongozi wa Kivuko cha MV Nyehunge kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma ya usafiri mpaka hapo watakapo kikarabati au kupata kingine.

Alisema mipango ya Serikali ya muda mrefu ni kujenga kivuko kikubwa kitakachofanya safari zake kati ya bandari ndogo ya Bugorola iliyopo kisiwa cha Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.

“Tumefanya utafiti kwenye visiwa vidogo vyote na kubaini kuna mialo zaidi ya 140. Hii itaimarishwa ili iweze kufikika na vyombo vya usafiri ambavyo ni imara,” alisema.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Jenista Mhagama alisema baada ya mazishi Serikali itahakikisha inarejesha hali ya eneo hilo kwa kujihakikishia wamemaliza miili yote katika kivuko.

“Ninapenda kusema kwamba lazima tuhakikishe miili yote imetambulika, imezikwa lakini hata ile ambayo haijatambuliwa inahifadhiwa kwa upande wa Wizara ya Uchukuzi wahakikishe kivuko chetu kinarudishwa nchi kavu na kufanyiwa matengenezo,” alisema Jenista

MAJALIWA APIGA KAMBI UKARA

Akizungumza katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema baadhi ya fedha  zitakazopatikana katika michango ya Watanzania zitatumika kujenga uzio na mnara katika makaburi ya watu waliokufa katika ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere.

Fedha hizo zinachangwa kupitia akaunti maalumu iliyofunguliwa katika Benki ya NMB pamoja na namba maalumu ya Tigo kupitia simu ya mkononi.

“Fedha hizi ni za wafiwa hivyo hatuna budi kuzitumia kulingana na mwenendo wa tukio,” alisema Majaliwa.

Alisema huo ni msiba mkubwa kwa taifa, hivyo ataendelea kukaa katika Kisiwa cha Ukara hadi atakapohakikisha shughuli zote za oparesheni ya uokoaji zimekamilika.

Akizungumza wakati wa maziko ya watu tisa kwenye makaburi ya pamoja kwenye Kisiwa cha Ukara jijini Mwanza, Majaliwa alisema vifo hivyo vimekuwa pigo kwa familia, dugu, jamaa, marafiki na kwa taifa kwa kupoteza wapendwa wao katika ajali hiyo hivyo Watanzania wajipe moyo kwamba ‘Ni mapenzi ya Mungu’.

“Taifa limepatwa na msiba mkubwa kwa kupoteza ndugu, jamaa na wapendwa wetu. Kwa sasa wafiwa wanahitaji kufarijiwa, zaidi kuliko kutoa taarifa za upotoshaji na za malumbano ambazo zinaweza kuongeza simanzi na uchungu.

“Watanzania tujipe moyo kuwa ni mapenzi ya Mungu wakati Serikali ikiendelea kutafuta namna ya kurejesha hali katika eneo hili,” alisema.

Alisema miili minne iliyozikwa katika makaburi hayo ya pamoja ni ya marehemu ambao hawakuweza kutambuliwa na ndugu zao na miili mitano ni ya marehemu ambao walitambuliwa na ndugu zao lakini waliomba kwa ridhaa yao izikwe katika makaburi hayo ya pamoja na kufanya miili hiyo kufikia tisa.

Alisema miili mingine 214 ilitambuliwa na ilichukuliwa na ndugu zao kwenda kuizika katika maeneo yao na kwamba bado wanatoa fursa ya utambuzi kwa mwili mmoja uliopatikana jana na kufanya idadi ya waliofariki dunia katika ajali hiyo kufikia 224, kabla ya kuchukua uamuzi wa kuuzika katika makaburi hayo ya pamoja.

Alisema katika hali inayotia moyo, watu 41 waliokolewa wakiwa hai na wavuvi waliojitokeza kufanya shughuli ya uokoaji muda mfupi baada ya kutokea ajali hiyo, kabla hata vikosi vya uokoaji havijafika katika eneo la tukio.

“Hadi sasa inaonesha kulikuwa na watu zaidi ya 260, yaani 41 waliookolewa na 224 waliopoteza maisha,” alisema.

Akielezea namna ajali hiyo ilivyotokea, Majaliwa alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa kivuko hicho cha MV Nyerere kilichokuwa kikifanya safari zake katika visiwa vunavyounda Kisiwa cha Ukerewe kilibeba mizigo mikubwa tofauti na uwezo wake, hivyo kushindwa kuhimili uzito.

Alisema kwa mujibu wa taarifa hizo, kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba tani 25, abiria 101 na magari matatu kilibeba zaidi ya abiria 224, ambao ni zaidi ya mara mbili ya uwezo wake na bado taarifa kuhusu uzito wa mizigo haijapatikana.

Hata hivyo Majaliwa alikanusha madai kuwa kivuko hicho kilipata ajali kutokana na ubovu na kueleza kuwa Serikali imekuwa ikikifanyia ukarabati mara kwa mara na Julai mwaka huu, injini mbili na gia boksi zake zilifungwa mpya zenye thamani ya Sh milioni 191.

Alisema tayari watendaji wote wanaohusika na kivuko hicho wameshakamatwa kwa mahojiano ya awali na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, akisisitiza kwamba Serikali itaunda Tume Maalumu ya uchunguzi itakayohusisha wataalamu, vyombo vya dola ili kubaini chanzo.

JUHUDI ZA SERIKALI

Majaliwa alisema pamoja na juhudi za uokoaji, ajali hiyo imetokea wakati Serikali ikiwa imezindua juhudi mpya za ujenzi wa Meli kutoka Mwanza kwenda Bukoba na ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama katika Bandari ya Mwanza, ikiwemo chelezo kitakachotumika katika ujenzi na ukarabati wa meli hizo.

Septemba 3 mwaka huu, Rais John Magufuli alishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi huo wa chelezo, meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo na ukarabati wa meli mbili ambazo zimekekuwa zikifanya safari zake katia Ziwa Victoria.

Alisema akaunti hiyo iliyopewa jina la Maafa MV Nyerere nio namba 311005726 iliyofunguliwa katika Benki hiyo ya NMB Mwanza kwa kufuata taratibu zote za kisheria na tayari akaunti nyingine ya Tigo Pesa yenye jina la RAS Mwanza imefunguliwa kwa namba 0677 030 000 kwa ajili ya wale ambao hawataweza kutumia huduma za benki.

MBUNGE MKUNDI

Naye Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema) alisema ajali hiyo imeleta simamzi kwa taifa inatakiwa iwe funzo la namna ya kujipanga kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya namna hiyo yanapotokea.

Alisema kwa kuwa tayari imeshatokea, watu wa Ukerewe watapata faraja iwapo watapata chombo kingine cha usafiri kitakachokuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao, kwa kuwa ndiyo njia pekee ya usafiri wanayoitegemea.

“Tuko katika kipindi kigumu sana, tunaomba muendelee kuwa nasi na tuendelee kushikamana. Faraja yetu, tunahitaji kupata uhakika wa mazingira mazuri ya kupata usafiri ambao hautaleta hofu kwa watu wetu, tupate chombo ambacho hakitaturejesha katika janga kana hili,” alisema.

MANUSURA WAELEZA

Manusura aliyekuwa jirani na chumba cha nahodha wa Kivuko cha MV Nyerere asimulia kwamba, nahodha wa zamu aliyekuwa akiendesha, Abell Maatane Mganga (35) inadaiwa alikuwa akinywa bia, kuchati na kuongea na simu ya kiganjani.

Akizungumza MTANZANIA Kisiwani Ukara, manusura huyo aliyeomba kutotajwa jina, alisimulia kuwa pamoja na abiria na mizigo kujaa kupita kiasi, nahodha huyo alikuwa akiongea na simu huku akinywa bia.

“Nahodha alistuka kivuko kikiwa kimekaribia kutia nanga, hivyo kumlazimu kukata kona ya ghafla na kusababisha mizigo kuhamia upande mmoja,” alisema.

Naye Cesilia Sabasaba (34), mkazi wa Kijiji cha Nyang’ombe Kata ya Bwisya alieleza kwamba chanzo ni nahodha kufanya uamuzi wa kukata kona ghafla baada ya chombo kupoteza mwelekeo wa usawa wa daraja la kivuko kuelekea pembeni ikiwa ni mita chache kutoka daraja linalotumika.

“Alipochukua uamuzi wa kukata kona ndipo tukaona vitu na bidhaa mbalimbali vikiporomoka kutoka upande mmoja kwenda sehemu ambayo gari lilikuwa limeegeshwa ndipo ghafla kivuko kilipinduka na gari lilikuwa la kwanza kutumbukia kwa sababu ya uzito w

Kazi ya kukiondoa Kivuko cha Mv Nyerere ndani ya maji ili kuweze kufanyiwa ukarabati imeanza baada ya kufanikiwa kusafirisha tingatinga ambalo lilifika jana Bwisya.

Baada ya kufika watalaamu walifunga nyaya ngumu na kuanza kukivuta.

Akizungumza jana wakati akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dk. Mussa Mgwatu, alisema wameanza zoezi la kukitoa majini kivuko hicho kwa kushirikiana na Kampuni ya Songoro Marine ya Mwanza.

Alisema katika zoezi hilo watatumia maputo maalum (Airbags) ambayo yataingizwa ndani ya kivuko kilichozama yakiwa hayana upepo kisha kujazwa ili kukifanya kielee zaidi na kukivuta ufukweni.

Kwa upande wake Mhandisi wa Kampuni ya Songoro Marine, Meja Songoro alisema hatua ya kwanza ilikuwa ni kukitoa kwenye tope hivyo walifunga waya maalum na kukivuta kwa kutumia tingatinga.

“Tumefanya kazi ya awali kukivuta tumefanikiwa kukitoa kwenye tope umbali wa mita kama 8, sasa hatua yetu ya pili tumeanza kupeleka ‘airbags’ (Maputo) ambayo baada ya kuyaweka vyema yatajazwa upepo hivyo kifanya kuelea, tutakivuta tena hadi ufukweni,” alisema Songoro.

Alisema kazi ya kukitoa kivuko hicho inaweza kuchukua siku saba au pungufu na kubainisha kwamba kazi hiyo ni ya pili  ambapo awali walikuwa wakitoa meli ndani ya maji kwa muda wa wiki mbili.

HABARI HII IMEANDALIWA NA FREDRICK KATULANDA na PETER FABIAN (UKARA) na ANDREW MSECHU (DAR ES SALAAM

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles