30 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

JPM ATOA MWANGA SEKTA BINAFSI

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

MKUTANO wa Rais Dk. John Magufuli na wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini uliofanyika Ikulu  jijini Dar es Salaam jana uliibua mazito kwa pande zote mbili.

Wakati Rais Magufuli akisema anayo orodha ya kampuni hewa 17,446 ambazo zimekuwa zikitumia mbinu ya kukwepa kodi kwa kudai marejesho ya fedha ya Ongezeko la Thamani (VAT), wafanyabiashara nao waliorodhesha yale yanayoonekana kukwaza biashara zao.

RAIS MAGUFULI

Rais Magufuli  ambaye ndiye aliitisha mkutano huo alianza kwa kuwahutubia wafanyabiashara hao zaidi akisema  baadhi yao wapo wasio waaminifu ambao wamekuwa wakikwepa kodi kwa kutoa rushwa na wengine kufanya udalali na kujihusisha na uhalifu.

Alisema jambo hilo limejitokeza katika biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho.

“Baadhi yao wamekuwa wakitumia mbinu ya kukwepa kodi kwa kudai marejesho ya fedha ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati mauzo yaliyofanyika ni hewa ya biashara za nje na kwenye hili nataka niseme wazi nina orodha ya kampuni 17,446 ambazo zimehusika na tuhuma hizo,”.

“Nitawapa nakala ya kampuni hizi hewa ili mkafanye uchambuzi wenu na kama yalikwepa kitu chochote yakajipange kulipa ndani ya siku 30.

“Miongoni mwa wanaofanya vitendo hivyo ni waliowahi kubinafsishiwa viwanda na Serikali, kupewa ardhi ili kuviendeleza, kwamba baadhi yao wameamua kuuza mitambo ya viwanda hivyo au kugeuza matumizi ya viwanda bila kufuata utaratibu.

“Wengine wametumia maeneo hayo kukopa fedha benki kwa ajili ya kazi hiyo na hawajafanya, hiyo ni dhambi na wengine najua mko hapa.

“Baadhi ya wafanyabiashara wamejenga viwanda kama gelesha na kuvitumia kupokea bidhaa kutoka nje bila kulipa kodi stahiki kama vile bidhaa hizo zimetengenezwa nchini,”alisema Rais Magufuli aliingiza mkono kwenye mfuko wa koti lake ili kutoa ‘flash’ yenye orodha ya kampuni hizo lakini akashindwa kuipata mara moja huku mwenyewe akishangazwa akisema au amelogwa?.

Baada ya kuhangaika kwa muda wa dakika kama mbili bila mafanikio, ndipo wasaidizi wake wakamsaidia kuitoa.

Aidha, alisema kumekuwa na uongezaji wa marejesho ya fedha ya VAT kwa wafanyabiashara ili waweze kupewa fedha nyingi kutoka serikalini huku akiuita kuwa ni wizi.

Rais magufuli alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitengeneza vitabu vya hesabu ili kukwepa kupeleka kodi kubwa ya ongezeko ya thamani Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

“Linapofika suala la kuwasilisha asilimia 18 ya VAT wengi wamekuwa wakibaki nayo kama mtaji badala ya kuipeleka serikalini na wamekuwa wakitengeneza vitabu tofauti.

“Kimoja ni cha benki chenye mahesabu ya kweli yenye faida na kitabu kingine ni cha TRA. Kwa kawaida kile kinachopelekwa benki kinakuwa cha kweli lakini kinachokwenda TRA ni kidogo wakati mwingine kinaonyesha hasara.

“Nataka nitoe mfano wa kampuni tatu, moja ya kampuni ina vitabu vitatu na fedha zake ni hatari ukiangalia, nina uhakika huyo mfanyabiashara ataenda akairudishe hiyo fedha iliyokuwa inatakiwa.

 “Kampuni nyingine namba mbili taarifa ya benki inaonyesha mwaka 2017 faida ilikuwa Sh milioni 958  lakini iliyopelekwa TRA ni Sh milioni 20 kwenye kitabu cha pili, kampuni namba tatu mwaka 2017 taarifa ya benki inaoyesha faida ilikuwa Sh milioni 501 lakini TRA iliambiwa kuwa imepata faida ya Sh milioni 72.

“Kampuni hiyo hiyo mwaka 2018 ilipeleka benki Sh milioni 508 huku kitabu cha TRA kikionyesha ni Sh milioni tatu.

“Kampuni namba nne ilipeleka kitabu benki chenye taarifa ya faida ya Sh bilioni 5.03 lakini TRA waliambiwa kuwa wamepata faida ya Sh milioni 255,”alisema Rais Magufuli.

TAASISI KUKWAMISHA BIASHARA

Pamoja na hilo Rais Magufuli pia alizungumzia uwepo wa taasisi nyingi zinazofanya shughuli za aina moja, ambazo zimekuwa ni chanzo cha kukwamisha ukuaji wa biashara nchini.

Alisema uwepo wa utitiri huo wakati mwingine umekuwa kikwazo kuanzisha na kuendesha shughuli za biashara nchini.

Alizitaja taasisi hizo ambazo zimekuwa zikiingiliana kimajukumu kuwa ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

“Nyingine ni Ofisi ya Mkemia Mkuu, Wakala wa Vipimo, NEMC, Tume ya Ushindani, Ewura, Sumatra na nyingine nyingi zimekuwa zikihusika katika kutoza tozo na ada mbalimbali.

“Siyo katika upande wa udhibiti tu bali hata katika taasisi zinazoratibu ukuzaji wa biashara na ujasiriamali nchini zipo nyingi na wengi wanaifahamu Sido lakini sina uhakika kama wanafahamu juu ya shughuli zinazofanywa na Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo).

“Kutokana na utitiri wa taasisi hizo zimekuwa hazihudumiwi na zimekuwa zinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo,”alisema Rais Magufuli.

Katika hoja hiyo hiyo aliinyooshea kidole Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), akisema ni ya muda mrefu lakini hana uhakika kama inawasaidia wafanyabiashara.

Pia alisema pamoja wafanyabiashara wa nje na kuja nchini lakini hajaona matokeo ya ujio wao tangu waanze kutembelea nchini.

“Ukiangalia ‘combination’ ya TPSF sina uhakika kama ina wafanyabiashara kutoka mikoani, ni kundi la watu fulani ambao wanakaa Dar es Salaam, unajua najitahidi niwe muwazi leo ili tutafute majibu ya kujibu.

“TPSF sina uhakika sana kama ni chombo kinachowawakilisha wafanyabiashara wote na ndiyo maana niliagiza wakuu wa wilaya na mikoa watoe wafanyabiashara watano watano kila wilaya waje kwenye kikao hiki ili tuje tusemane tupate ukweli,”alisema Magufuli.

“Sasa hayo mtayajibu ninyi wenyewe mimi si jukumu langu ila mwangalie je uwakilishi wa wafanyabiashara kweli umegusa nchi nzima, kuna umuhimu wa kuanzisha chombo kingine kitakachowafikia moja kwa moja, je mkurugenzi wenu ana duka au kiwanda.”

“Ukiwa msemaji wa wafanyabiashara lazima uijue biashara vilivyo ili tufike mahali tutengeneze kitu ambacho kitawasimamia ninyi,”alisema Magufuli.

AFUTA TOZO 101

Katika hatua nyingine Rais Magufuli alisema tangu alipoingia madarakani, tozo 101 za kilimo, uvuvi, ufugaji na uchimbaji wa madini zimefutwa.

 “Kodi zikiwa chache na viwango vikiwa vidogo biashara inastawi, kinyume chake biashara inadumaa na hii ndiyo sababu tumeanza kuchukua hatua za kupunguza viwango na utitiri wa kodi, tozo na ada zinazotozwa nchini.

“Tumerekebisha baadhi ya sheria zilizokuwa kikwazo cha kufanya biashara nchini ikiwemo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Vipimo, Tume ya Ushindani, Mahakama inayosimamia ushindani wa biashara.

“Lakini pia tunatafuta masoko na kuboresha huduma za biashara katika kutafuta masoko ya bidhaa tunazozalisha nchini kupitia maonyesho mbalimbali,”alisema.

Alisema ili kustawisha biashara wameanzisha huduma za pamoja  ‘Electronic single stop shop’ ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wafanyabiashara.

MAFANIKO KIBISHARA

Akizungumzia kuhusu mafaniko ya serikali kibiashara, Rais Magufuli alisema pamoja na mdororo wa uchumi lakini Tanzania imeendelea kufanya vizuri kibiashara.

Alisema mwaka 2018 iliuza kwenye soko la Afrika Mashariki (EAC), bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 447.5 ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 349.6 mwaka 2017.

“Bidhaa tulizoagiza kutoka nchi za Afrika Mashariki mwaka 2018 zilikuwa za dola za kimarekani milioni 302.93 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 220.4 mwaka 2017.

“Katika soko la Jumuiya ya Ushirikiano na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2018 Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 999.34 ukilinganisha na dola za Marekani milioni 877.8 mwaka 2017.

 “Bidhaa zilizonunuliwa kutoka SADC zilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 604.3 ikilinganishwa dola za Marekani milioni 600.6 mwaka 2017,”alisema.

Alisema tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, jumla ya kampuni na biashara mpya 74,715 zimesajiliwa huku kati yake 30,716 zikisajiliwa na Brela.

Alisema majina ya biashara 54,657 yamesajiliwa huku leseni za bishara zilizotolewa na mamlaka za serikali za mitaa ni 655,340 huku viwanda vipya 3,500 vikijengwa.

ATAMANI MABILIONEA 100

Aidha Rais Magufuli alisema atakapomaliza muda wake wa uongozi, anatamani Tanzania iwe na mabilionea zaidi ya 100.

Alisema suala hilo litamfanya afurahi kuwa  anamaliza muda wake na kuacha mabilionea wengi katika nchi kutokana na kile alichokuwa akikifanya katika kuboresha mazingira ya biashara.

“Thubutuni na msiogope kufanya biashara ya aina yoyote, nchi yetu imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri, rutuba, maji kwa ajili ya uvuvi, mifugo, madini fursa nyingi za uwekezaji zitumieni ili ziwanufaishe ili siku nikiwa naondoka angalau niache wafanyabiashara mabilionea zaidi ya 100 nitafurahi sana.

“Biashara mipakani kwetu Watanzania bado iko chini, tutumie fursa ya masoko ya Afrika ya Mashariki na SADC ili tuweze kwenda mbali kwa sababu masoko haya yanaunganisha mamilioni ya watu.

“ “Semeni yale yote ambayo mnaona ni kero kwenu na mnataka tuyafanyie kazi, msiogope na kila mmoja azungumze kadiri anavyoona kwa faida,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles