30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

JPM atinga gerezani, aelezwa mambo mazito

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAFUNGWA na mahabusu katika Gereza la Butimba jijini Mwanza, wamemweleza Rais Dk. John Magufuli kero kubwa tano huku ya kubambikiwa kesi za mauaji ikiongoza.

Walitoa kilio hicho jana baada ya Rais Magufuli kutembelea gereza hilo na kuzungumza na wafungwa, mahabusu na askari magereza.

Kalikenya Nyamboge ambaye anatumikia kifungo cha miaka 30, alimtaja ofisa usalama aliyetambulika kwa jina moja la Mwasifika na kudai amekuwa akishirikiana na baadhi ya mahabusu na wafungwa kuingiza simu gerezani.

“Kuna watu umewapa madaraka wakusaidie kazi, lakini badala yake wanaleta vitu ambavyo havitakiwi, kuna ofisa usalama anawapa simu washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi, matokeo yake simu zinakamatwa, tunanyang’anywa vitu.

“Huyu ofisa yupo mpaka leo, ondoka naye, tusaidie kwa hilo ili amani iwepo,” alisema Nyamboge.

Diwani mstaafu wa Kata ya Mbugani, Hashimu Kijuu, ambaye ni mahabusu katika gereza hilo, alisema watu wengi wamekuwa wakibambikiwa kesi za mauaji.

“Kuna kijana mmoja anaitwa Kulwa ana kundi la watu watano alibambikiwa kesi, yeye ni mfanyabiashara wa mafuta ya dizeli. Siku moja bajaji yake iliyokuwa imebeba lita 120 ilipofika njia panda iliharibika.

“Alipigiwa simu atafute bajaji nyingine, akatafuta toroli aje ahamishe mafuta, akapita OCCID mmoja wa Nyamagana alivyoona akawapigia maaskari waje wachukue yale mafuta.

“Yalibebwa mpaka kituoni halafu wakawa wanataka Sh milioni moja, akawaambia hana, mafuta yakataifishwa akapewa kesi ya mauaji,” alisema.

Kijuu kwa upande wake alisema aliuza shamba lake lililopo Kisesa, lakini aliishia kupewa kesi ya utakatishaji fedha.

“Askari Sangali aliniambia nitakaa jela mpaka nikute mke wangu kaolewa, maneno gani haya, uchungu umenipanda mno, nashindwa kusema. Shamba nililouza ni la kwangu, kwanini nipewe kesi ya utakatishaji,” alisema.

Shukrani Masegenya anayetumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, alimwomba Rais Magufuli kuwapunguzia vifungo. 

“Pamoja na kufundishwa stadi za kazi, kuna wengine wamefungwa miaka 30 na wengine wamefungwa maisha, sasa utafundishwa stadi za kazi wakati maisha yako yote yataishia hapa gerezani?

“Tunaomba Rais utupunguzie vifungo ili hata tunapofanya kazi tujue tutakwenda kuwa kioo cha jamii tutakapokuwa nje,” alisema.

Askofu Edson Mwombeji, alimwomba Rais Magufuli aingilie kati vifungo vilivyotolewa na mahakama ili waweze kuchapa kazi.

Abdulrahman Ismail alisema alibambikiwa kesi ya mauaji na hadi sasa amekaa gerezani kwa miaka minane.

 “Askari wamekuwa wakikaa mahakamani na kusubiri watu walioachiwa kisha kuwakamata tena na kwenda kuwafungulia mashtaka mengine.

“Wanatengeneza namna ya kupata rushwa, juzi kuna mtu aliachiwa askari akawa anamvizia kwenye baraza amkamate, yule mtu akamchana kwa wembe,” alisema Ismail.

Mwita Mataluma anayetumikia kifungo cha maisha kwa kesi ya mauaji, alisema amekaa gerezani kwa miaka 40 na kumwomba Rais Magufuli ampunguzie adhabu.

“Rufaa yake ilishindikana kwa sababu aliambiwa jalada limepotea, tunakuomba katika watu unaowasamehe na huyu mzee umwangalie, tangu 1979 yupo gerezani,” alisema mmoja wa wafungwa kwa niaba ya mzee huyo.

Rais Magufuli alimtaka mzee huyo azungumze mwenyewe, lakini alionekana akishika kichwa huku akibubujikwa na machozi.

“Nilifungwa kwa kosa la mauaji kwa sababu nilimuua mke wangu kwa bahati mbaya, nimekaa gerezani miaka mingi, naomba msaada wako ikiwezekana niachiwe,” alisema.

Rais Magufuli alimuukuza; “ulimuulia wapi mke wako?” Akajibu; “Kinesi Mara.” Akajmuuliza tena; “sasa ukiachiwa si utakwenda kuoa tena utamuua mwingine.” Akajibu; “siwezi kufanya lolote, tabia yangu ni nzuri, kama nitaachiwa nitakwenda kuishi vizuri.”

 Mfungwa mwingine anayetumikia kifungo kwa makosa ya ubakaji, alisema hadi sasa amekaa gerezani kwa miaka 18, lakini alibambikiwa kesi kwa kuwa walikuwa wanagombea cheo cha Katibu wa Bakwata Mkoa wa Tabora.

“Kulikuwa na ugomvi, nilipewa cheo ambacho kilikuwa kinaviziwa na watu, nililetewa binti baadaye wakasema nimembaka,” alisema mfungwa huyo.

Clement Lugale, alisema ana kesi ya mauaji tangu mwaka 2014 haijaamuliwa na kumwomba Rais Magufuli amsaidie.

“Tulikuwa washtakiwa watatu na mshtakiwa wa tatu alikiri akafungwa mwaka 2014, tumebaki wawili mpaka leo maamuzi hakuna. Aliyekiri ameshamaliza kifungo na kuachiwa,” alisema Lugale.

Gideon Chacha, anayetumikia kifungo cha unyang’anyi wa kutumia nguvu, alisema alifungwa na Mahakama ya Mwanzo miaka 15, lakini aliwahi kuandika barua kumkataa hakimu aliyemfunga ambayo anayo hadi sasa.

“Hakimu alisema ‘kama nilisomeshwa na baba yako utatoka jela, lakini kama nilisomeshwa na baba yangu utaona’, huu ni mwaka wa 10, nimeandika barua nyingi sijawahi kujibiwa,” alisema Chacha.

Mfungwa mwingine mwenye ulemavu wa miguu, alisema alifungwa Desemba 2016 kwa kosa la ubakaji na kudai kuwa alibambikiwa kesi kwani kwa hali aliyonayo asingeweza kukimbia kama ilivyodaiwa mahakamani.

KERO ZA ASKARI

Mmoja wa askari katika gereza hilo, Koplo Paschal, alisema alipata ajali akiwa kazini na kuvunjika mguu tangu 2013, lakini hajalipwa fidia ya kuumia kazini hadi sasa.

Askari mwingine, Jonas Mabula, alisema wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na ukosefu wa vifaa, hali inayosababisha wakati mwingine kuwachanganya wafungwa wagonjwa katika gari la kubebea kuni.

“Jeshi letu limesahaulika sana, tunafanya kazi katika mazingira magumu, vyombo vya usalama hatuna, magari mpaka inafikia kipindi tunaona wenzetu inawezekana wao wakawa na kazi nzuri kuliko sisi.

“Hapa hatuna hata ‘ambulance’, hawa unavyowaona (wafungwa, mahabusu) tunawaingiza kwenye gari la kuni kuwapeleka Hospitali ya Bugando.

“Bajeti zetu zimekuwa duni, uniform (sare) tunajinunulia ili tupendeze kwa sababu kazi tunaipenda,” alisema Mabula.

Alimwomba Rais Magufuli kuwapatia gari la kubebea wagonjwa, gari la watumishi, matrekta, boti ya kisasa, mashine ya kuchimba kokoto na fedha kwa ajili ya kuweka kikosi cha KM.

 “Mkuu wa gereza hana gari ni aibu, akienda kwenye vikao vya ulinzi na usalama anadandia magari ya askari. Makazi yetu si rafiki, tumefyatua matofali 40,000 tunaomba utujengee hata ghorofa moja, ni aibu ukizunguka kambini,” alisema.

MAJIBU YA KERO

Rais Magufuli alisema amebaini mambo mengi katika gereza hilo na kuwaomba wamvumilie atakwenda kuzitatua.

“Ninajua wako watu waliofungwa hawajafanya makosa, ninajua pia wako wamekaa mahabusu wanacheleweshewa kesi zao ili wasipate haki zao, wapo watu wameachwa humu kwa sababu hawajazungumza vizuri na polisi ili wamalize upepelezi na kwenda kutoa ushahidi.

“Nimegundua mambo mengi hapa, hata vingine hamjaeleza, naomba muamini nimeyaona, nimeyasikia, ninaomba mvumilie, mniachie niende nikazifanyie kazi hizi changamoto,” alisema Rais Magufuli.

Alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Murilo Jumanne, kushughulikia kesi za mahabusu 925 ambazo hazijasikilizwa.

“Kuna kesi zingine za kubambikizwa, zingine hazina mshiko, kakae na watu wako wanaohusika na upelelezi mzifanyie kazi. Si lazima utumie wapelelezi walioko hapa Mwanza, wanaweza wakatoka wa mahali pengine ili kusudi hawa waliocheleweshwa haki ipatikane,” alisema.

Rais Magufuli pia aliagiza kuitwa kwa askari polisi aliyefahamika kwa jina moja la Sagali, anayedaiwa kuwabambikia kesi mahabusu wawili ambao mmoja ni ya mauaji kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya kumwomba rushwa ya Sh milioni moja akashindwa kutoa.

Hata hivyo askari huyo alipofika alimweleza Rais Magufuli kwamba anafahamu kesi ya Diwani mstaafu Kijuu na kwamba alikuwa na tuhuma za kughushi na kuuza eneo na baada ya kufanya upelelezi alimtafuta mwenye eneo ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya kisomali.

“Kwa hiyo Msomali ana shamba wakati kwa mujibu wa sheria ya Tanzania ardhi yoyote haiwezi kumilikiwa na mtu ambaye si raia,” alisema Rais Magufuli.

Askari huyo alisema baada ya hapo aliandaa jalada na kupeleka kwa wakili wa serikali ambaye aliandaa mashtaka.

Ofisa Usalama wa gereza hilo aambaye alituhumiwa kuingiza simu alisema; “Vitu vyote ambavyo havitakiwi kuingia gerezani mimi ndiyo huwa navikagua na kuvikusanya.” Rais Magufuli akamuuliza; “viko wapi sasa.” Akajibu; “viko ofisi ya mkuu wa gereza.”

Akaulizwa tena; “Ulikusanya simu ngapi?” Akajibu; “nne.” Akaulizwa tena; “gereza hili lote liwe na simu nne tu.” Akajibu; “ndizo nilizokusanya.” Rais Magufuli akasema; “nikiamua sasa hivi kufanya ukaguzi nitapata simu nne tu.” Akajibu; “hupati simu.”

Ofisa huyo akasema; “Huyu (mfungwa aliyetoa tuhuma hizo) amesema kwa sababu ni miongoni mwa watu ambao walitaka asikilizwe yeye, nashukuru amezungumza ameniinua kwa kiasi fulani.”

Kauli hiyo haikumpendeza Rais Magufuli, akasema; “Naona una kiburi, unazungumza mbele yangu kwamba amekuinua, una uhakika gani kwamba mimi nitatoka na jibu gani kwako.”

Rais Magufuli pia aliagiza watu wote waliouliza maswali katika mkutano huo wasisumbuliwe kwa yale waliyozungumza bali wawe marafiki zao.

Aliahidi kutafuta magari ili yasaidie wafungwa na watendaji wengine katika gereza hilo na kuwataka wakuu wa magereza kuwa wabunifu.

“Changamoto mlizozungumza zinatia uchungu lakini nitazibeba, msiichukie hii kazi mkaona ninyi ni tofauti na majeshi mengine, timizeni wajibu wenu,” alisema Rais Magufuli.

Pia aliahidi kutoa magunia 15 ya mchele na ng’ombe watatu ili wafungwa hao waweze kupikiwa.

Baada ya kusikiliza kero, wafungwa hao walimwombea Rais Magufuli sambamba na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwakani ufanyike kwa amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles