26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATIBUA NYONGO KATIBA MPYA

Na EVANS MAGEGE


KAULI ya Rais Dk. John Magufuli kusema kwamba hafikirii kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya, imeonekana kutibua nyongo kwa baadhi ya wachambuzi wa siasa ingawa wengine wanaiunga mkono.

Magufuli alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kongamano la siasa na uchumi lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambako alisema ikitokea fedha hizo zikatolewa zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kwa bahati mbaya Magufuli ameamua kutoa kauli hiyo kwa sababu hajafikiria umuhimu wa Katiba Mpya.

Alisema Magufuli anatakiwa kufahamu kuwa suala la Katiba Mpya si kitu cha Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, bali ni mapendekezo yaliyoanzia kwa Jaji Francis Nyalali na kuendelezwa na majaji wengine.

Alisema msukumo wa mabadiliko ya Katiba ulitokana na kuwapo umuhimu wa takwa la kisheria la kuweka muundo wa kidemokrasia wa siasa zenye ushindani na si ajenda ya rais yeyote bali ni ajenda ya kitaifa.

Baregu aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alikwenda mbali zaidi kwa kusema Rais anatakiwa atambue nchi ipo katika ombwe kubwa la kikatiba na Watanzania hawajui ipi bora kati ya Katiba inayotumika sasa, mapendekezo ya pili ya rasimu ya Jaji Warioba au iliyopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.

“Rais anatakiwa kutambua suala la Katiba kwa sasa ni sawa na jini ambalo limetoka ndani ya chupa hivyo hawezi kulituliza kirahisi ili lirudi ndani ya chupa,” alisema.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema anaunga mkono msimamo wa Magufuli kwa sababu mchakato wa Katiba uliopita ulitumia fedha nyingi pasipo kufikiwa lengo.

Alisema Katiba Mpya ni muhimu lakini kwa sasa anaona wananchi hawajakomaa na kuelewa wanataka Katiba ya namna gani.

“Katika mchakato uliopita watu walikimbilia suala la muundo wa Serikali, jambo hilo likatuvuruga na ikawa shida kubwa. Kwa hiyo nafikiri tungoje tuive kwanza maana tukiingia sasa tutapiga kelele na tusiambulie kitu tena,” alisema Kilaini.

Pia kwa muktadha huo, alisema ni afadhali shetani unayemjua kuliko malaika usiyemjua.

Alifafanua maana ya kauli hiyo kwa kusema: “Shetani unayemjua unaweza kupata mbinu ya kumkwepa lakini huyu unaweza kumwita malaika kumbe ni shetani mkubwa kuliko ulivyodhani,” alisema Kilaini.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema anaunga mkono kauli ya Magufuli kwa sababu huo ni ukweli wa mambo na si umung’unyaji wa maneno.

Alisema uhuhimu wa Katiba unahitajika lakini mchakato wake unahitaji muda kwa wananchi kufikirishana ili kujenga mwafaka wa kupata itakayokidhi mahitaji ya wengi.

“Sioni umuhimu wa kuharakisha suala hili, watu wanajaribu kujiumbia mirija yao ya kunyonya fedha za nchi, tuliona fedha nyingi zilipotea katika mchakato uliopita. Rais hili analitambua na ninamuunga mkono kwa msimamo wake kwa sababu kuna mambo mengi ya kuyatekeleza kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,” alisema Alhad.

Naye Mhadhiri mstaafu wa UDSM, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema kauli hiyo ya Magufuli ni kielelezo cha mkwamo katika kushamiri kwa demokrasia ndani ya nchi.

Alisema pamoja na mambo mazuri anayoyafanya Magufuli kwa taifa, lakini anatakiwa atambue mazuri hayo yanatokea katika muktadha ambao hauashirii vyema dhana ya wananchi kujitawala.

“Rais anatakiwa kufahamu kwamba, kinachojitawala si dongo fulani hivi  linalojiita Tanzania bali ni watu wanaoishi Tanzania na wanaojitawala kwa kujiwekea vyombo vyao vya kushirikishana katika kutoa maamuzi.

“Hivyo suala la Katiba Watanzania wanatakiwa kumwomba Mungu na kwa kutumia njia zilizo halali kumkumbusha Rais kwamba maamuzi ya fedha zao hutolewa na Bunge na si mtu mmoja,” alisema Dk. Lwaitama.

Alisema Magufuli anatakiwa kutambua Watanzania walipigania uhuru ili wawe huru na si kwa ajili ya mtu mmoja kuamua fedha zao azifanyie nini.

“Maendeleo peke yake hayakutusukuma tupiganie uhuru, kwa sababu kama reli au barabara hata wakoloni walikuwa wanajenga. Kwa mantiki hiyo, Watanzania waliamua kupigania uhuru kwa kutaka maendeleo kama hayo katika hali ya uhuru,” alisema Lwaitama.

Alisema Katiba Mpya inahitajika kabla Magufuli hajamaliza muda wake ili asije kiongozi mwingine akafanya mambo yake kwa kujitetea kwamba yaliyofanywa na mtangulizi wake yalikuwa ni mambo ya ovyo.

“Kwa sasa nionavyo Rais anachokitamani ni kitu kimoja na wananchi wanaamini kitu kingine, matokeo hayo lazima kuwapo mtanziko, sikatai tunafurahi sana anachokifanya na ni kweli tunataka fedha ya reli iwepo lakini na sisi pia tunahitaji fedha ya Katiba Mpya,” alisema Lwaitama.

Pia alisema suala la posho si lazima, hivyo kinachotakiwa ni Magufuli atangaze kuanza kwa mchakato wa Katiba bila kulipa posho kwamba watu watajitolea na mchakato utakwenda salama.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, alisema kauli ya Magufuli ya kutoonyesha kipaumbele cha Katiba Mpya inavunja msingi wa demokrasia.

Alisema Magufuli anaelewa kwamba wananchi wengi wanataka Katiba Mpya lakini haliweki jambo hilo katika kipaumbele chake hivyo ina maana ya kwamba anadharau matakwa ya wengi.

“Msingi huo ni kudharau demokrasia kwa sababu demokrasia msingi wake ni kwamba wengi wapewe na wachache walindwe.

“Mimi tatizo langu juu ya hiyo kauli yake ni kwamba, anaendesha nchi si kwa mood ya misingi yetu ambayo ni ya kidemokrasia kwa sababu wengi wakiwa wanataka ni wajibu wa Rais kama mlinzi wa Katiba yetu kusikiliza matakwa ya wananchi,” alisema Fatma.

Pia alisema anapata wasiwasi zaidi kwa msimamo huo wa Magufuli katika kipindi ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ni mchakato wa kidemokrasia.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema suala la Katiba Mpya si fedha kwa sababu kama tatizo ni hilo mbona kaipitisha nchi katika uchaguzi mdogo wa marudio?

“Tumeona kila Chadema wakihama wanakwenda CCM tunapitishwa kwenye chaguzi ndogo, kama ni hivyo basi kumbe suala la Katiba si hela kwa sababu kama ingekuwa tatizo ni fedha asingekubali kuwapokea ili fedha ya wananchi isitumiwe ovyo,” alisema Fatma.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles