Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Tanzania.
Timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele, imekuja nchini kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).
Katika mazungumzo na timu hiyo yaliyofanyika jana Ikulu Dar es Salaam, Rais Magufuli alieleza nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya Mto Rufiji, yanatekelezwa haraka iwezekanavyo.
“Sasa hivi nchi yetu inazalisha megawati 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge itatuzalishia megawati 2,100. Umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika viwanda, hivyo Serikali tumeamua kutekeleza mradi huu.
“Najua kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe na sauti moja, eneo litakalotumiwa ni kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia 3 tu ya eneo lote la hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa kilometa za mraba 45,000,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia, Dk. Bekele, alisema Ethiopia kwa sasa inazalisha megawati 4,300 za umeme kwa kutumia maji na ina miradi mingi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji.