32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATEMA CHECHE MARA

 

Na ANDREW MSECHU


Rais John Magufuli emesema hatamvumilia mtu yeyote anayesababisha tabu kwa Watanzania maskini, huku akiagiza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria wakandarasi wote waliopewa miradi ya maji ambayo haijakamilika katika Mkoa wa Mara.

Rais Magufuli pia ameagiza kukamatwa kwa mtu aliyenunua  hoteli ya Musoma na kushindwa kuiendeleza kwa miaka 10 iliyopita.

Alimtaja mtu huyo kuwa ni mwana CCM ambaye pia amepewa miradi ya maji aliyoshindwa kuikamilisha.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara mjini Musoma jana, Rais Magufuli alisema anapata tabu kuona Watanzania masikini wakinyanyaswa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia vibaya rasilimali na fedha za miradi huku wateule wake wakiendelea kuwepo bila kuchukua hatua stahiki.

“Ninawaeleza wateule wangu katika ngazi zote, kama nisingechaguliwa na hawa wananchi masikini wanaonyanyaswa, hata nyie nisingewaona na msingekuwa hapo mlipo. Lazima mjue kuwa nimewachagua na mpo hapo mlipo kwa sababu ya hawa walionichagua. Sasa ili wananchi hawa wasiendelee kuteswa, nawaambia nitawatesa ninyi niliowachagua,” alisema.

Akizungumzia Hoteli ya Musoma, alisema aliyeinunua na kushindwa kuiendeleza anyang’anywe hoteli hiyo na ikiwezekana adaiwe gharama zote za miaka 10 ambazo angetakiwa kuzilipa iwapo hoteli hiyo ingekuwa ikifanya kazi.

Alisema amepata taarifa za mwenye hoteli hiyo kuvishika vyombo vya dola kwa kutumia mfuko wake na kwamba anatakiwa kutambua uhalifu hauna chama, hivyo mkono wa sheria lazima ufanye kazi kwa kuwa mambo ya aina hiyo ndiyo yaliyoifikisha nchi hapa ilipo sasa.

Alisema anashagaa kuona muhusika huyo ndiye aliyelipwa mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maji ambayo haijakamilika huku aliyelipa akiwa yupo na aliyelipwa akiendelea kuwepo na viongozi wakiendelea kuangalia.

Aliagiza  hatua zichukuliwe haraka dhidi ya wote waliohusika katika utoaji wa fedha hizo.

Rais Magufuli alisema amebaini kwamba mara nyingi viongozi hutoa taarifa za uongo kwake na kwamba kwa sasa hahitaji taarifa kutoka kwa wakuu wa mikoa au wilaya kwa sababu anao Watanzania ambao humfikishia taarifa sahihi naye yuko tayari kuzifanyia kazi.

Akizungumzia urais wake, alirudia kauli yake aliyowahi kuitoa mara kadhaa akisema hakuwahi kufikiria kuwa Rais na kwamba alijaribu kubipu na kujikuta amekuwa, hivyo ana deni la kuhakikisha Watanzania wanatendewa haki.

“Siku nilipotangazwa na kuambiwa sasa nakuwa Rais nilipata taabu sana. Moyo wangu ulisononeka hasa nilipokuwa nikiwaangalia Watanzania ambao sasa wote walikuwa wakinitegemea mimi. Nilitamani nisingegombea, lakini nilipata moyo baada ya kuamini kwamba wataniombea na nitapata uwezo wa kutatua taabu zao,” alisema.

Alisema hata hivyo anaamini kwamba kutokana na nafasi hiyo, aliipata ili wale wanaokula fedha za umma nao waone uchungu wanaowasababishia Watanzania.

Alieleza kusikitishwa kwake na namna watu wenye fedha wanavyowapora masikini na wazee ardhi, akiwemo bibi kikongwe wa zaidi ya miaka 100, ambaye alimfuata akilia kuhusu kuporwa kiwanja chake na mtu mwenye fedha huku viongozi wa serikali wakiendelea kuwalinda watu wa aina hiyo.

Rais Magufuli ambaye pia alitembelea Shule ya Msingi ya Mwisenge, aliyosoma Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alieleza kushangazwa kwake na hali ya uchakavu aliyoikuta hapo, ikiwa haiakisi sifa ya shule aliyowahi kupitia muasisi wa taifa.

“Nimeshangaa kuona shule hii ikiwa katika hali mbaya namna hii, wakati viongozi wapo, wakuu wa wilaya wapo, wakuu wa mkoa wapo, mawaziri wanaohusika wapo, watu wanaohusika na makumbusho wapo, lazima tujiulize tumepungukiwa na nini?

“Kama Nyerere angezaliwa Ulaya, eneo kama hili tungekuwa hata tunakwenda kutalii, lakini huku sijui tumepungukiwa na nini?” alihoji.Alisema tayari ameshatoa maelekezo shule hiyo ikarabatiwe katika mazingira yake ya asili na halisi kisha iwekwe uzio ili yeyote atakayefika huko aweze kuona kuwa ni sehemu iliyopewa hadhi inayostahili.

Alisema aneo jingine alilotoa maelekezo ya ukarabati wa haraka na Uwanja wa Ndege wa Musoma ili uweze kufikika kwa urahisi na ndege zinazonunuliwa na serikali ziweze kutua ili kuupa hadhi inayostahili mji huo.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles