JPM ATANGAZA MAAMUZI MAGUMU

0
594
Rais Dk. Joh Rais Dk. John Magufuli (katikati) akitoka kukagua moja ya mabanda yaliyopo katika Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ya mwaka huu Dar es Salaam jana.
Rais Dk. Joh Rais Dk. John Magufuli (katikati) akitoka kukagua moja ya mabanda yaliyopo katika Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ya mwaka huu Dar es Salaam jana.

NA CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema mvua inyeshe au jua liwake atatekeleza mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge ulioshindikana kwa zaidi ya miaka 40 baada ya kuwekewa vikwazo mbalimbali.

Stiegler’s Gorge ni mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maji katika bonde la Mto Rufiji kwenye pori la akiba la Selous.

Mradi huu ulikuwa ni mawazo ya aliyekuwa Rais wa kwanza na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyoyatoa tangu mwaka 1975.

Hata hivyo, mradi huo ulipata vikwazo vingi vikiwa ni vya uharibifu wa mazingira kila ulipotakiwa kuanza, tangu enzi za utawala huo hadi hivi sasa Rais Dk. Magufuli ameazimia kuutekeleza.

Ukimwacha Mwalimu Nyerere, wamepita marais wengine ambao ni Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na wote kwa sababu hizo na nyingine walishindwa kuutekeleza mradi huo.

Taarifa kwamba Rais Magufuli amedhamiria kutekeleza wazo hilo la Mwalimu Nyerere, zilijulikana mapema wiki hii baada ya kukutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.

Ethiopia ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotajwa kufanikiwa kuzalisha umeme mwingi unaozidi megawati 60,000 kutoka vyanzo mbalimbali kama maji, upepo, jua na joto kutoka ardhini.

Jana katika ufunguzi wa Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Rais Magufuli alisisitiza kwa mara nyingine dhamira yake hiyo ya kufufua mradi wa Stiegler’s Gorge ambao utazalisha umeme wa megawati takribani 2,100.

Akisisitiza, alisema mradi huo utatekelezwa kwa fedha za ndani ambazo alisema zipo na kwamba upembuzi yakinifu umekwishafanyika.

Pamoja na hilo, alisema amekwishatoa maelekezo Wizara ya Nishati na Madini na zabuni itatangazwa.

Alisema ana imani kukamilika kwa bwawa hilo kutasaidia kuisukuma sera yake ya ‘Tanzania ya Viwanda’.

Rais Magufuli alisema anafahamu zipo kelele nyingi za watu watakaohoji fedha za ujenzi zitakakopatikana, lakini atatekeleza mradi huo na endapo atapata wafadhili wenye masharti nafuu ataungana nao.

Alisema mradi huo ukikamilika, ikichanganywa na megawati 1,460 zinazozalishwa sasa na megawati 600 zinazozalishwa kutoka miradi ya Kinyerezi I, II, III nchi itaweza kuzalisha megawati 4,000 hadi 5,000.

Kuhusu vikwazo vya kimazingira, Rais Magufuli alisema hawezi kusikiliza kelele za watu wa mazingira kwa sababu ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kuhifadhi mazingira tofauti na inavyofahamika.

“Mbuga ya wanyama ya Selous ipo Tanzania na wenye maamuzi ya kuchimba bwawa la kuzalisha umeme au la ni sisi,” alisema Dk. Magufuli.

Katika kukazia hilo, alisema kasoro za kimazingira za uchimbaji wa bwawa hilo hawezi kuzipa nafasi kwa kuwa litanufaisha taifa na wanyama watapata maji ya kutosha.

Alisema mradi huo utasaidia wananchi masikini wanaoizunguka mbuga hiyo kwa kupata shughuli za kufanya.

“Washirika wa kimaendeleo wanaotupenda watakuja kutusaidia, tuna maliasili ya kila aina, mfano gesi hatujaitumia vizuri, makaa ya mawe, upepo wa Singida pia hatujaona manufaa hadi leo,” alisema Dk. Magufuli.

STIEGLER’S GORGE NI NINI?

Stiegler’s Gorge ni mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme wa maji katika bonde la Mto Rufiji katika pori la akiba la Selous.

Mradi huu utakaozalisha megawati 2,100 za umeme uko kilomita zaidi ya 200 kutoka Dar es Salaam.

Katika utekelezaji wake, utatumia kilometa za mraba 1,350 ambazo ni sawa na asilimia 3 ya eneo la hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa kilometa za mraba 45,000.

Utafiti uliofanywa miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80 (1978-1980) na RUBADA (Rufiji Basin Development Authority) kwa kushirikiana na kampuni ya kigeni ya M/s Norplan/Hafslund, ulionyesha kwamba mradi huo una uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme mwingi wa maji zaidi ya umeme ambao nchi inahitaji.

Matokeo ya utafiti huo pia yalionyesha kwamba kupitia bonde hilo, mradi huo una uwezo wa kuhimili mitambo mitatu mikubwa ya kuzalisha umeme, mtambo wa kwanza ukizalisha megawati 400 ambao ungefungwa upande wa kaskazini mwa bwawa.

Mtambo wa pili una uwezo wa kuzalisha megawati 800, ambao ungefungwa upande wa chini ya bwawa na mtambo wa tatu  ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 900 ambao ungefungwa upande wa kusini mwa bwawa na kukamilisha megawati 2,100.

Inaelezwa mradi huo ukikamilika una uwezo wa kuzalisha umeme takribani mara mbili ya mahitaji.

Kwa mujibu wa wataalamu, mradi wa umeme wa maji wa Stiegler’s Gorge unategemea ustawi wa Mto Rufiji, ambao nao pia unategemea kwa asilimia 60 ustawi wa Mto Kilombero, hususan Bonde la Mto Kilombero.

Mto Rufiji hupata maji yake mengi kutoka mito miwili mikuu ya Kilombero na Ruaha Mkuu.

 KUHUSU SABASABA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema hakubaliani na wazo la Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tantrade), chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Christopher Chiza kujenga hoteli na maduka ya kisasa katika viwanja vya Sabasaba.

Badala yake alishauri Tantrade wazipeleke fedha zilizotengwa kwenye mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa ambacho kitakuwa mfano kwa wafanyabiashara.

“Sioni sababu ya kujenga majengo makubwa hapa ya hoteli na baa ambapo watu watalewa na watapigana tu… naona mwenyekiti wa bodi na wajumbe wake mnataka kuchezea fedha hizo, angalieni kwa undani wazo langu,” alisema Dk. Magufuli ambaye kabla na baada ya kufika uwanjani hapo kulikuwa na ulinzi mkali kiasi cha baadhi ya watu kuzuiwa kuingia na vyakula ndani.

Alisema ni vyema wajumbe wa bodi hiyo wakapanga mkakati wa kushirikiana na wadau mbalimbali wa biashara kwa kuingia mkataba wa kujenga majengo ya kisasa ndani ya uwanja huo na kukatana kidogo kidogo.

“Majengo yaliyopo wapewe wanaokuja kuonyesha biashara, wapeni hata mikataba kwa miaka 50 mtakuwa mmewabana na kila mwaka watakuja hapa,” alisema Magufuli.

Alisema wazo hilo huenda likapokewa tofauti, lakini hata kama ni baya walifanyie kazi.

KODI

Akizungumzia suala la kodi, Rais Magufuli amewapongeza wananchi kwa mwamko mzuri wa kulipa kodi, hasa ya majengo.

Alisema awali wananchi walikuwa wakikerwa na mfumo wa ulipaji kodi kwa kuwa haukuwa wazi, lakini kwa sasa wanafurahia kulipa.

“Watanzania wanakataa kodi za ovyo ovyo na hakuna asiyependa kulipa kodi,” alisema Magufuli ambaye pia aliwapongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuongeza muda wa kulipia kodi za majengo hadi Julai 15.

Katika ufunguzi huo, Rais Magufuli alitoa zawadi kwa taasisi na sekta binafsi zilizofanya vizuri, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kikiibuka kidedea kwa kuwa washindi wa jumla wa maonyesho hayo.

Ameagiza maonyesho hayo yaongezwe muda hadi Julai 13, ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuendelea kuuza bidhaa.

Naye, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema maonyesho hayo yataongeza chachu ya wawekezaji wa viwanda wa ndani na nje.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here