30 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

JPM ataka Zimbabwe iondolewe vikwazo

Na Mwandishi wetu

-Harare

RAIS John Magufuli amempongeza Rais Zimbabwe Emmerson, kwa kufanya mageuzi ya  uchumi katika nchi hiyo.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya taifa hilo.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli aliyasema hayo juzi usiku   katika dhifa ya taifa iliyoandaliwa na Rais Mnangagwa na kufanyika Ikulu,   Harare.

Taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli alisema tangu Rais Mnangagwa aingie madarakani, uchumi wa taifa hilo umeanza kuimarika.

Alisema  kwa sasa uchumi wa Zimbabwe unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 na mwaka unaofuata kuongeza hadi wastani wa asilimi 4.4.

“Kufuatia hali hiyo ameisihi jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo hivyo vinawaumiza wananchi wa Zimbabwe wakiwamo watoto na wanawake,” ilisema taarifa ya Ikulu.

Ilisema katika hotuba yake, Rais Magufuli aliwapa pole rais na wananchi wote wa Zimbabwe kwa watu takriban 400 kufariki dunia katika mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Idai kilichoikumba Zimbabwe Machi.

“Alisema Watanzania wanaungana na ndugu zao Wazimbabwe katika majonzi ya kuondokewa na jamaa zao na wanawaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina,” taarifa ilisema.

Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Zimbabwe ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu   Nyerere na Mzee Robert Mugabe, Rais Magufuli alisema Tanzania inatambua na inathamini uhusiano huo wa historia na undugu.

Alisema jukumu lililopo sasa ni kuelekeza nguvu katika uhusiano na ushirikiano wa uchumi utakaoziwezesha Tanzania na Zimbabwe kuongeza biashara na uwekezaji.

Awali katika mazungumzo yake na Rais Mnangagwa juzi mchana, walikubaliana kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyopo katika Kamati ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission – JPC) kwa manufaa ya nchi zote mbili.

“Rais Mnangagwa kuja kwangu hapa Zimbabwe ni kuthibitisha kuwa urafiki wetu bado upo imara na sisi Tanzania tumejipanga kuuimarisha zaidi.

“Tunataka tufanye biashara zaidi na nyinyi ndugu zetu wa Zimbabwe  tukuze uchumi wa nchi zetu na kuongeza kipato cha wananchi wetu,” taarifa ilimnukuu Rais Magufuli alisema.

Naye  Rais Mnangagwa alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na kwamba yeye na wananchi wa Zimbabwe wanatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi wakati Zimbabwe alipokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Idai.

Alisema msaada huo uliwagusa Wazimbabwe wengi na kuwakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema Zimbabwe itabaki kuwa rafiki na ndugu wa kweli wa Tanzania na hivyo amemhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wa uchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji na kushirikiana katika usafiri wa anga.

Taarifa hiyo ilisema Rais huyo alimshukuruRais Magufuli kwa kumpa mbinu mbalimbali za  uongozi ikiwamo kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo kwa Serikali na ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya chama chake ZANU-PF na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles