24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATAKA WALA RUSHWA WAFUNGWE

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amesema anataka walarushwa wengi wafungwe licha ya kuwa kuna baadhi ya watu hawataki kusikia kauli hiyo.

Hayo aliyasema jana Ikulu Dar es Salaam baada ya kumwapisha Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo.

Alisema wakifungwa walarushwa nchi haitakuwa na rushwa kwani  ndio wamekuwa walimu wa walarushwa nchini, huku akiwataka viongozoi hao wa Takukuru kwenda kusimamia kazi hiyo na wasimwogope mtu yeyote.

“Mtu yeyote anayehusika na rushwa huyo ni adui wa Watanzania. Nataka walarushwa wote wafungwe, najua haya maneno kuna baadhi ya watu hawataki kuyasikia, ni lazima tufike mahali tuwe na Tanzania isiyokuwa na rushwa,” alisema.

Aidha Rais Magufuli alieleza kutoridhishwa na taratibu za uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka ya rushwa yanavyochukua muda mrefu na ametoa wito kwa viongozi wa Takukuru kufanyia kazi eneo hilo ili vita dhidi ya rushwa ionekane ikizaa matunda haraka.

“Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji,” alisema.

Aliwataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

“Na mimi nikiwa kiongozi wenu, nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba wote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi.

“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo, yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu,” alisema.

Pamoja na hayo ameipongeza Takukuru kwa kazi iliyoanza kuifanya, lakini ametaka juhudi zaidi ziongezwe ili watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya Rais Magufuli kuzungumza, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali Mbungo, alimshukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles