25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

JPM ataka viongozi wasisubiri Takukuru

Nora Damian -Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amewataka viongozi waliopewa madaraka kudhibiti vitendo vya ubadhirifu katika maeneo yao, badala ya kusubiri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akizungumza jana baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ile ya Takukuru Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, alisema bado kuna changamoto nyingi ambazo Serikali kwa kushirikiana na wananchi wanatakiwa kuzishughulikia.

“Inaonyesha kuna mambo mengi ambayo tunatakiwa kuyafanya, kuna changamoto nyingi ambazo sisi kama Serikali, viongozi, wananchi tunatakiwa kushughulika.

“Takukuru imeokoa Sh bilioni 8.8, sasa unaweza kujiuliza katika maeneo hayo viongozi waliokabidhiwa madaraka na wanalipwa mshahara walikuwa wanafanya nini?

“Je, hakuna wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala, ma-DAS, makatibu tarafa, maofisa kata, mabalozi, viongozi wa vyama mbalimbali ‘including’ chama kinachotawala. Viongozi wako ofisini wana magari, simu bilioni 8.8 ziwe zimeliwa na sisi tupo,” alisema Rais Magufuli.

AMSHANGAA WAZIRI MKUU

Alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekuwa akijitahidi kukemea vitendo vya ubadhirifu katika maeneo mbalimbali nchini, lakini alishangaa kwanini vinapotokea mkoani kwake havikemei.

“Siku moja nilimwambia Waziri Mkuu na nataka niseme hapa, unatoka Lindi, nimekuwa nikisikia mahali pengine unakemeakemea, sana kwanini wananchi wa Lindi wadhulumiwe ufuta Sh bilioni 1.2 na wewe upo?

“Hatuwezi kila mahali panapotokea matatazo tunasubiri PCCB, haiwezekani sisi viongozi tunafanya nini, kwanini tuwe na haya madaraka?

“Nitoe wito sisi viongozi kuanzia mimi, makamu wa rais, waziri mkuu, wakuu wa mikoa, mawaziri mpaka kule chini tuendelee kutimiza wajibu wetu kudhibiti dhuluma kwa wananchi wadogo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ataikabidhi ripoti hiyo kwa wasaidizi wake ili wakaifanyie kazi kupitia maeneo yao kabla ya kuikabidhi bungeni.

“Ripoti nzuri zimejaa uwazi, kila mmoja katika maeneo yake tukaanze kuifanyia kazi, yaliyozungumzwa ‘including’ ya chama na mimi nashukuru kwa kuwa wawazi, yatakuja yote bungeni.

“Kuna maeneo mengi ambayo yalikuwa yanatajwa, Tamisemi, wizara mbalimbali, miradi mingine, sisi ndani ya Serikali tuanze kuyafanyia kazi.

“Tupeleke ripoti bungeni, lakini kila waziri, mkuu wa mkoa, katibu mkuu hoja zitakapokuwa zinatolewa bungeni tutakazokuwa na majibu tutoe kwa sababu hili ni bunge la mwisho ili likija jipya haya yasiwe viporo kwa watendaji wetu,” alisema Rais Magufuli.

Pia alimpongeza CAG kwa kuanza kukagua mashirika ya umma tofauti na awali ambapo yalikuwa yakikaguliwa na watu binafsi hatua iliyowezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni 1.4 kwa mashirika 10.

BALOZI

Kuhusu ufisadi katika balozi mbalimbali alisema; “Wizi wa mabilioni ya fedha uliofanyika katika ubalozi wa Ethiopia balozi nimeshamrudisha, hili ni fundisho kwamba ukiharibu kwenye sehemu yako ujiandae kuubeba msalaba.”

JESHI LA POLISI

Rais Magufuli alilishangaa Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya watu waliobainika kufanya ubadhirifu, hasa kwa kulipa mishahara hewa.

“Wamelipa watu mshahara wengine wameshakufa, Serikali hii haiwezi ikawa inalipa mishahara ya watu waliokufa kwa taasisi muhimu kama ya Polisi wakati ‘lockup’ mnazo ninyi, pingu mnazo ninyi. Mmeshindwaje kuwashika hawa, mnakamata wengine?” alihoji Rais Magufuli.

AMPANDISHA CHEO MBUNGO

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alitangaza kumpandisha cheo Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kutokana na utendaji mzuri.

“Tena nafikiri hutakiwi kuwa kaimu, kuanzia leo (jana) wewe uko moja kwa moja kabisa, pamoja na kwamba wako ndani ya chombo chako wabaya wabaya wachache, hasa huyu wa Kinondoni na watu wake, kama yuko hapa ajue ndiyo mbaya wangu mimi,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles