JPM ASHTUSHA

0
1267

Na WAANDISHI WETU

MSIMAMO wa Rais Dk.  John Magufuli kuzuia wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo ndani ya utawala wake, umeibua mjadala mkali kwa baadhi na hata kuleta hisia za hasira kwa watu wa kada mbalimbali katika jamii.

Hali hiyo imekumbusha kile kilichowahi kutokea kwa mtangulizi wake, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, ambaye alikuwa na msimamo unaofanana na wake, ambaye alisema watoto wanaopata ujauzito shuleni ni kwasababu ya viherehere vyao.

Mazingira ya kuwapo kwa mjadala mkali yanatokana na baadhi ya maoni yaliyotolewa na watu mbalimbali kupitia ama maandiko au matamko.

Mbali na maandiko na matamko, msimamo huo wa Rais ambao umeonekana kujadiliwa zaidi ndani na nje ya Bunge juzi na jana, umesababisha Asasi za Kiraia zipatazo 32 ambazo zinaunda Mtandao wa  Kupinga Mimba Utotoni (TECMN) nazo kujifungia kwa siku nzima kuujadili.

Hoja ambazo zinaibuliwa sasa nyingi ni zile za kupinga msimamo huo, zikijengwa kwa misingi ya mazingira yaliyosababisha mtoto kupata ujauzito, mapitio ya Dira ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 pamoja na Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978.

Baadhi wanadai kuwa msimamo huo hauwapi haki watoto ambao wamepata mimba katika matukio ya kubakwa.

Kwa misingi hiyo hiyo, inaelezwa watoto wengi wamejikuta au wanajikuta wanapata ujauzito katika mazingira ambayo si ya utashi wao, kutokana ufahamu unaoendana na umri wao wa utoto.

Kuhusu msimamo huo kupingana na Dira ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, baadhi wanaona unaweza kuathiri haki ya mtoto kupata fursa ya elimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Katika Dira hiyo, sura ya pili ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 (2.1.1) inatanabahisha kwamba lengo lake ni kuwa Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Dhima ya dira hiyo ambayo imefafanuliwa kwenye sura ya pili (2.1.2), inaeleza kuwa, Dira hiyo imelenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze

kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Hivyo azma ya Tanzania ni kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, ambapo sekta ya elimu na mafunzo imepewa jukumu la kuandaa rasilimaliwatu ya kutosha kwa ajili ya kukidhi mabadiliko hayo.

Kupitia kipengele hicho, ambacho kipo kwenye misingi ya umuhimu wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, wapo wanaodai kuwa, msimamo wa Rais unaweza kuathiri malengo ya muda mrefu ya nchi ya kupata wajuzi wa kutosha kujenga uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Katika mtazamo huo huo, baadhi wanaojadili hoja hiyo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii wamekwenda mbali na kueleza kuwa, msimamo huo wa Rais Magufuli unapingana na Ilani ya chama anachokiongoza, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020.

Ilani hiyo, ambayo MTANZANIA Jumamosi imeisoma, imejipambanua wazi kupitia sura namba 52, kipengele namba (ii) na (iii) kwenye ukurasa wa 99.

Kipengele cha (ii) kimeweka wazi kuwa “Wasichana wote wa Elimu ya Msingi walioacha shule kwa sababu za kupata ujauzito wataendelea na masomo.”

Pia kipengele(iii) kinataja malengo ya Ilani hiyo kwamba; “Wanafunzi wote wanaomaliza mzunguko wa Elimu ya Msingi wanaongezeka kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 95 ifikapo mwaka 2020”.

Kwa muktadha huo huo, baadhi wamekwenda mbali kwa kugusia Sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1978, ambayo inalinda haki ya mtoto kupatiwa elimu.

Kwamba sheria hiyo inaeleza wazi kuwa elimu ya msingi ni ya lazima kwa watoto wote na itatolewa bure ambapo kanuni zinazohusika na sheria hiyo zinahesabu kuwa ni kosa kwa mzazi atakayeacha kumwandikisha shule mtoto mwenye umri wa kwenda shule.

Katika kile kinachotafsirika aidha ni hasira au maoni hasi dhidi ya msimamo huo wa Rais, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetoa tamko la kupinga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo, alisema msimamo huo unapingana na kauli mbalimbali zilizotolewa na mawaziri, wizara na wakurugenzi kuhusu kuendelea na masomo kwa wanaopata mimba shuleni.

“Kuna mwongozo wa Wizara ya Elimu unaozungumzia wanafunzi wanaopata mimba kurudi shuleni, tumesaini maazimio mbalimbali kuhakikisha watoto wote wanapata elimu.

“Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema lazima watoto warudi shuleni, chakushangaza Rais anazungumza tofauti,” alisema.

Alisema wanaopata mimba wakiwa shuleni hawapendi kuwa hivyo, kwa sababu wengine hubakwa na wengine hupata mimba katika mazingira ya nyumbani.

Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Mwalimu Kasuku Bilago (Chadema), alisema sera hiyo ya watoto wanaopata mimba wasirudi shuleni itaathiri watoto wa maskini, kwa sababu wenye uwezo watawarejesha katika shule za kulipia.

“Katiba inasema kila raia atakuwa huru kutafuta elimu kwa upeo wowote kwa kiwango anachotaka, kubeba mimba shuleni isichukuliwe kama laana,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza, alisema wanafunzi wapewe elimu ya uzazi na serikali itengeneze mazingira bora ya kuhakikisha watoto waliopata mimba wanarejea shuleni baada ya kujifungua.

Akichangia, Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), alisema kuwakataza wanafunzi waliopata mimba kurejea shuleni ni kuhalalisha ndoa za utotoni.

“Tunaomba Rais Magufuli aliangalie upya suala hili, si kweli kwamba wakiruhusiwa kurejea shuleni wakati wa mapumziko wanafunzi darasa zima watakwenda kunyonyesha,” alisema.

Katika hatua nyingine, Profesa wa Sheria, Issa Shivji, aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa tweeter uliosomeka;

“Jamii inayomzuia mjamzito Elimu inamdhalalisha kila mama na mtoto. Mjamzito ni mama mtarajiwa. Anastahili heshima ya mama na huduma ya mjamzito.”

Mbali na hoja hiyo ya Profesa Shivji, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent Mashinji, naye alipinga msimamo huo wa Rais kwa kuufananisha na hukumu ya kifo kwa mwizi aliyeiba kuku.

“Tusimwangalie huyu binti katika umri wake wa miaka 16, 17 mpaka 22 anapopata mimba, bali tumwangalie kwa ukamilifu wake hadi kwenye “Life Expectancy yake ambayo ni miaka 62 kwa Tanzania,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema kiongozi mwenye nafasi ya juu kama ya urais lazima awe na maono.

“Kiongozi lazima awe na maono, hasa mwenye nafasi ya juu kama rais. Fikra zake lazima ziwe pana na asiishi kama karani.

“Binti mwanafunzi kapata mimba ya utotoni…anaondolewa shule, anakwenda kujifungua na kuleta mwingine/wengine, anaambiwa hawezi kusoma tena labda aende VETA, na huko VETA hawakusaili kama huna cheti walau cha form four! (kidato cha nne),”alisema Dk. Mashinji.

Alisema kutokana na hali hiyo, msichana huyo anaweza kuchagua kuwa mama lishe wakati mwanamume aliyezaa naye akiwa jela kwa miaka 30.

“Pamoja na karama zote ambazo Mwenyezi Mungu kamjalia…hapo ndio mwisho wake, kwa kumzuia kwenda shule haumkomoi yeye na wala hauzuii mchezo huu,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na asilimia 39 wapo katika umaskini uliokithiri, hivyo hawajui maana ya elimu wala umuhimu wake.

Alisema Rais Magufuli atakuwa shahidi wa maisha ya kijijini na hata umuhimu wa elimu.

“Isingekuwa elimu asingeweza hata kuwa mwalimu wa Kemia (Chemistry) na pia anajua maisha yalivyo magumu kijijini. Hebu tuwe binadamu kidogo na kuwawezesha hawa mabinti ili watoe mchango wa maendeleo kwa Taifa,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema bado anaamini elimu ni haki ya kila mmoja, hata kama ni  mfungwa.

Mbali na Dk. Mashinji, aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Nderakindo Kessy, akizungumza na gazeti hili, alisema suala la wanafunzi kupata mimba na kurudi shuleni linalochangiwa na mabadiliko ya ukuaji ni mjadala mpana unaohitaji uamuzi wa busara.

Alisema pamoja na Bunge la EALA kuwahi kujadili suala hilo kupitia Muswada wa Sheria wa Haki za Jinsia, lakini bado nchi washirika wamekuwa na changamoto kuhusu suala hilo.

“Sina uhakika kama huo muswada ulishasainiwa na maraisi wa nchi za jumuiya na kufanya kuwa sheria, lakini tulishawahi kujadili na vifungu vililenga zaidi kumlinda mtoto wa kike,” alisema Nderakindo.

Alisema japokuwa muswada huo ulilenga zaidi haki za wanawake, lakini pia ulimtetea na kumlinda mtoto katika masuala mengine, mfano haki ya kupata taulo za kike, haki ya kuendelea na masomo endapo atapata ujauzito.

Alisema kuna vitu vingi vya kuzungumzia suala hilo mbali na sheria, kwakuwa watoto wote ni wa Taifa moja, hivyo endapo atapata mimba inapaswa kuhesabika kama ajali.

“Tuone kama mtoto amepata ajali bila kujua, hapa sasa ndio tuseme dereva yeyote anayesababisha ajali achukuliwe hatua na siyo aliyeumizwa na ajali,” alisema Nderakindo.

Alisema hoja ya kutomrudisha mtoto wa kike shuleni baada ya mimba pia inapaswa kuzungumzwa kwa kuzingatia taarifa kutoka nchi mbalimbali duniani kwa kuangalia mabadiliko ya utandawazi.

“Kwa sasa watoto wana kila sababu ya kukua haraka kwa sababu ya vyakula tunavyokula na kemikali tunazotumia,” alisema Nderakindo.

Awali MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na Ofisa Habari wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Michael Malya, ambaye alisema wadau 32 wa Mtandao wa Kupinga Mimba Utotoni (TECMN) walikutana kwa lengo la kujadili ili kutoa tamko moja dhidi ya msimamo huo wa Rais.

“Mkurugenzi wa LHRC kwa kushirikiana na wadau wengine, wamekutana leo (jana) wanajadili hilo suala na watatoa tamko la pamoja baada ya majadiliano, hivyo kituo kwa sasa hakiwezi kutoa tamko,” alisema Malya.

Kwa mujibu wa Malya, pamoja na mtandao huo kutoa msimamo mwishoni mwa Mei na kupinga mwanafunzi kusitisha masomo baada ya kupata ujauzito, lakini kikao cha jana kilikuwa kwa ajili ya kujadili kauli ya Rais Magufuli.

Hivi karibuni wabunge wa Jamhuri ya Muungano waliwahi kujadili suala hilo na kugawanyika makundi mawili, ambapo kulikuwa na watu waliounga mkono na wengine waliopinga suala hilo.

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), alisema ili watoto waruhusiwe kuendelea na masomo baada ya kujifungua, kuna haja ya kubadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kwa sababu inawazuia wasifanye mapenzi wakiwa na umri mdogo.

Hivyo, anataka tahadhari zaidi zichukuliwe kabla ya kufikia uamuzi wowote, huku mila, desturi na imani za kidini zikizingatiwa, kwa kuwa dini zinazuia mapenzi katika umri mdogo.

KAULI YA RAIS

Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bagamoyo, mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na kuruhusiwa kurudi shuleni.

Pia alizitaka taasisi zinazotetea utaratibu wa wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni, kufungua shule zao za wazazi, lakini si kuilazimisha Serikali kufanya hivyo.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo siku chache baada ya Taasisi ya HakiElimu kuitaka Serikali kuharakisha kupitia na kupitisha  miongozo watoto wa kike waliojifungua warejee shuleni na kuendelea na masomo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here