28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

JPM ASAMEHE WAFUNGWA 2,291

RAIS Dk. John Magufuli

 

Na PATRICIA KIMELEMETA – DARES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ametoa msamaha wa wafungwa 2,291, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, ilisema msamaha huo umetolewa chini ya ibara ya 45(1)(d).

Alisema msamaha huo utawahusu wafungwa wote ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wawe wametumikia nusu ya vifungo vyao vilivyobaki, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

“Wafungwa hao ni wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu (TB) na saratani (kansa) ambao wako kwenye ‘terminal stage’, wathibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au mganga mkuu wa wilaya,” alisema.

Alisema wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi, umri huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au mganga mkuu wa wilaya.

Aliwataja wengine watakaopata msamaha huo ni wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

“Pia wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili na ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au mganga mkuu wa wilaya,” alisema.

Alisema ni mategemeo ya Serikali, kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Meja Jenerali Rwegasira alisema msamaha huo, hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na waliohukumiwa adhabu hiyo kisha kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

“Msamaha huo hautawahusu pia waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

“Wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo.

“Wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo,” alisema.

Meja Jenerali Rwegasira, aliwataja wafungwa wengine ambao hawatahusika na msamaha huo kuwa ni wale waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea.

“Pia wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo na wale wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002) pamoja na waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

“Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki na waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

“Waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu na wale waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

“Wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili na wale wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha za Serikali pia hawatahusika,” alisema.

Meja Jenerali Rwegasira aliwataja wengine wasiohusika kuwa ni wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali na wale walioingia gerezani baada Machi 16, mwaka huu na warejeaji wa makosa au wafungwa waliowahi kufungwa gerezani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles