24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 25, 2022

JPM aponda sera ya madini ya Chadema

Na NORA DAMIAN-ITIGI

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amewataka Watanzania kuwa makini na kuepuka sera zinazolenga kuwarudisha enzi za utumwa.

Alisema nchi imejengwa kwa nguvu kubwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alipambana hadi ukapatikana uhuru lakini baadhi ya watu wanataka irudi kwenye utumwa.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Polisi Square uliopo Tarafa ya Itigi mkoani Singida jana, Rais Dk. Magufuli alisema Tanzania ni taifa huru na kwamba njia ya kushinda yanayopangwa ni kuyakataa kwani yamepitwa na wakati.

“Katika ilani yao wanazungumza  wakishapata madaraka madini yetu watayaweka dhamana maana yake atatafutwa mtu wa kutoka nje anakabidhiwa madini yote anaanza kuchimba eti ni dhamana ya wao kuendesha nchi.

“Uchukue madini yote ukabidhi watu fulani ndiyo dhamana ya kuongoza nchi, dhamana watakayoitumia kutengeneza barabara…tunaingia kwenye utumwa.

“Wataweka dhamana ya madini kesho yake wataweka dhamana ya wanyama wetu na mbuga zetu…tunaingia kwenye utumwa wa aina nyingine,” alisema.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha mapinduzi yaliyopatikana katika sekta ya madini yanaendelezwa ili sekta hiyo iendelee kuchangia zaidi katika pato la taifa na kupunguza umaskini.

“Sisi tunazungumza mali yote itakayokuwa inakusanywa kama ni ya madini ni ya Watanzania wote, itauzwa kwa bei ya wakati huo na ndiyo maana tuliwabana hata wale wengine mpaka wakaingia kwenye mazungumzo kwamba faida tunagawana nusu kwa nusu.

“Tumeruhusu hata watu wa kawaida wakachimbe dhahabu zao na ndiyo maana tumefungua maduka Tanzania nzima ya dhahabu, ndiyo maana Tanzanite tukaizungushia ukuta, ndiyo maana kina Laizer wamekuwa mabilionea Watanzania wa kawaida hilo ndiyo lengo letu na hiyo ndiyo Tanzania tunayoitaka.

“Ndugu zangu ninawaomba hawa muwafundishe kwa kuwanyima kura, wanakotupeleka si huko,” alisema.

ATAHADHARISHA MAJIMBO

Dk. Magufuli alisisitiza Watanzania kuendelea kuungana na kuepuka sera zinazolenga kuwagawa kwani wote waliwekwa kama taifa moja ambapo dini na makabila yote yaliungana pamoja na Zanzibar kisha ikazaliwa Tanzania.

“Mfano tumejenga barabara kutoka hapa Itigi hadi Chaya kilometa 89 kwa shilingi bilioni 103, tukajenga tena Chaya hadi Nyaua kilomta 85 kwa Sh bilioni 117 ni zaidi ya bilioni 200, bado hujaweka vituo vya afya, elimu bure.

“Sasa ukigawanya maeneo ya majimbo mngeijenga, mngepata wapi pesa za kujenga…unapotengeneza majimbo utachagua kabila gani litawale pale?

“Tunapotaka kujega barabara fedha tunatoa za Watanzania wote huo ndiyo umoja, ukisema jimbo moja lijitegemee kila kitu hatutafika. Naomba mkatae umajimbo na ukabila umepitwa na wakati,” alisema Dk. Magufuli.

ALIYOAHIDI

Dk. Magufuli aliahidi kutengeneza kwa kiwango cha lami kilomita 10 za barabara katika Tarafa ya Itigi na kumtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani Singida kutangaza zabuni ya ujenzi huo haraka.

“Tangaza tenda mwezi huu pesa usiulize mimi nitatoa kwa ajili ya kutengeneza barabara hii na wala hii si hongo…mimi bado ni rais,” alisema Dk. Magufuli.

Kuhusu barabara ya Itigi – Rungwa – Makongorosi alisema awali zabuni ilitangazwa lakini gharama ilikuwa kubwa na kusababisha mradi huo kufutwa lakini akaahidi kuwa itatengenezwa.

“Sasa zamu ya Itigi – Makongorosi tutajenga kilomita 50 na tutaweka makandarasi wengi kama tulivyoweka kwenye barabara ya Tabora – Mpanda ambapo tunajenga kilomita 359,” alisema.

Kuhusu umeme alisema akichaguliwa miaka mitano ijayo kila kijiji Tanzania kitakuwa na umeme kwani wamejipanga kwa ajili ya kusambaza katika vijiji vyote ambavyo havina.

Alisema ombi la kutaka Itigi iwe wilaya linaendelea kushughulikiwa na kwamba wako kwenye mwelekeo mzuri.

Dk. Magufuli pia aliridhia Kituo cha Afya Itigi kipandishwe hadhi na kuwa hospitali ya wilaya ili kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri hadi Manyoni kwenda kupata huduma.

“Napenda niwathibitishie tumejipanga vizuri kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kweli Tanzania, ninawaomba propaganda mzipuuze tujenge nchi yetu kwa ajili ya maendeleo ya kweli,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,160FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles