25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM APIGA TENA

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli ameipa rungu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuitaka kuacha kutoza faini pekee, bali ikibidi izifute kampuni za simu za mkononi ambazo hazitajisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Aliyasema hayo jana wakati akizindua mfumo wa ukusanyaji kodi kielektroniki, ambao umeratibiwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Agizo hilo la Rais Magufuli, limekuja ikiwa ni wiki chache baada ya kuzuia usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje ya nchi kwa kile alichodai kuna utoroshaji wa dhahabu.

Rais alizuia makontena ya mchanga wa dhahabu 277 mali ya Kampuni ya Acacia yasisafirishwe nje hadi uchunguzi wake ukamilike baada ya kamati aliyoiunda kuchunguza kubaini yakiwa na kiwango cha madini chenye thamani kati ya Sh bilioni 829.4 na trilioni 1.439.

Akizungumza jana, Rais Magufuli alisema: “Tulipitisha sheria kampuni zote za simu zijisajili DSE, lakini zinasuasua na zingine zinazunguka.

“TCRA wanatoza faini ndogo na kwa mtu anayepata mamilioni, lazima ataacha kujisajili kusudi uwe unampiga faini kwa sababu faida nyingi anabaki nayo. Msipige faini tu, futeni haya makampuni, tufike mahali tutoe ‘decision’ (uamuzi) hata kama inauma.”

Alisema kama kampuni hizo zikijisajili DSE, miamala yao itaonekana hatua itakayowarahisishia TRA na ZRB kukusanya mapato.

Kuhusu mfumo wa ukusanyaji kodi aliouzindua, alisema unalenga kulinda usalama wa taifa, taasisi za Serikali na makampuni binafsi, kupunguza kero za Muungano na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kwani ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi.

“Napenda kukusanyiwa kodi, nafahamu hakuna mtu duniani anayependa kulipa kodi, hata enzi za Yesu walikuwapo na walipakodi katika maandiko yote hawakupendwa.

“Kamishna wa TRA na ZRB, msitegemee hata siku moja mtapendwa na watu, nyie kusanyeni tu lazima kila mmoja alipe, iwe anataka ama hataki,” alisema.

Hata hivyo, alisema licha ya mfumo huo kuanza kazi tangu Oktoba mwaka jana, mwitikio wa Serikali na taasisi binafsi kujiunga si mkubwa hivyo aliziagiza wizara za Tamisemi na Maliasili na Utalii zijisajili kwa lazima.

Alitoa mfano wa Ethiopia ambayo ina kampuni moja ya simu yenye watumiaji kati ya milioni 30 hadi 35 ambayo mwaka jana ilitengeneza faida ya Dola za Marekani bilioni 1.5.

“Sisi tuna watumiaji wa simu kati ya milioni 40 hadi 45, waulize TRA wamekusanya kiasi gani, utalia.

“Vodacom, Tigo, Airtel na wengine muingie kwenye mfumo huu ili kusudi tusiwaonee na ninyi msituonee. Kwani mnaogopa nini, mitambo ipo mna wasiwasi gani?

“Najua mnaweza mkatafuta sababu, kama mnataka tubadilishe sheria Bunge bado linaendelea, tutapeleka hati ya dharura,” alisema.

Rais Magufuli pia alipiga marufuku ujenzi wa vituo vingine vya ukusanyaji wa taarifa na kutaka fedha zitumike kwa shughuli nyingine za maendeleo.

“Mnataka vifike vingapi ndani ya Serikali ndiyo mridhike? Hakuna sababu ya kila wizara kujenga ‘data center,” alisema.

 

KODI ZA VILEO

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizitaka mamlaka husika kuacha kufikiria kupandisha kodi za vileo kila mwaka na badala yake zibuni vyanzo vipya vya mapato.

“Watu wetu utakuta wanafikiria kupandisha bia… jina langu la Pombe. Tuna wachumi kibao ‘they never think beyond the border, they think a complex issues’ na mwisho wa siku hawapati kodi yenyewe.

“Tunabaki kufukuzana, kulipa kodi kunakuwa ni tatizo badala ya kuwa kitu muhimu kwa watu wote,” alisema.

Alisema hata kodi za nyumba baadhi ya watu wamekuwa wakikwepa kulipa kutokana na kupangiwa viwango vikubwa vya kati ya Sh milioni 2 hadi 3 na kwamba kama vingekuwa vya Sh 10,000 hadi 100,000 watu wangehamasika kulipa.

“Tunakimbizana na wamachinga, tungeamua tukachapisha hata vitambulisho tu vya kuvaa halafu mmachinga akilipie Sh 10,000 fedha ambazo tungekusanya zingekuwa kiasi gani.

 “Kama tungeamua tukawa na kituo kimoja cha kusajili madini yote yanayosafirishwa halafu mtu atoe tu Sh 10,000 tungekuwa tumekusanya kiasi gani,” alisema Rais Magufuli.

 

UBINAFSISHAJI TTCL

Rais Magufuli alisema licha ya kutopata faida, Kampuni ya simu ya TTCL mwaka 1992 ilitoa gawio la Sh bilioni moja kwa Serikali, lakini tangu ilipobinafsishwa haikuwahi kutoa.

“Nachukia ubinafsishaji wa ovyo, ni nafuu tungebaki na TTCL wakati ule badala ya kuibinafsisha, nataka watu waelewe Serikali ninayoiongoza inataka kufanya biashara na wawekezaji waaminifu. Biashara yoyote duniani lazima iwanufaishe na wahusika wa nchi hiyo,” alisema.

Kampuni hiyo kwa sasa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 baada ya kununua hisa zilizokuwa zinamilikiwa na mwekezaji kwa Sh bilioni 14.6 na tayari imeanza kutengeneza faida.

Alisema kati ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa, viko vilivyofanya vizuri, lakini 197 havifanyi kazi na kwamba vingine vimeng’olewa mashine na kubaki kuwa maghala.

 

WATAALAMU WAZALENDO

Alisema wataalamu wa ndani waliojenga mfumo wa ukusanyaji kodi kielektroniki hawakufanya kazi bure kwa sababu wanalipwa mshahara.

“Kama wanalipwa mshahara hawajafanya bure, ‘unless’ kama mshahara hautoshi tuseme tuwaongezee, walisoma kompyuta na mimi nikasoma siasa, ndiyo kazi waliyoiomba,” alisema.

Hata hivyo, alisema kadiri mapato yatakapokuwa yakipatikana, Serikali itafikiria kuwaongezea mishahara wataalamu hao.

 

RAIS WA ZANZIBAR

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema ukusanyaji wa kodi ulio sahihi na makini ndio unaoipa uwezo Serikali katika kuendeleza uchumi na kusaidia maendeleo ya nchi.

“Serikali zote makini haziwezi kuendesha nchi bila ukusanyaji wa kodi na mapato, lazima uwepo utaratibu wa kuhakikisha kila mtu analipa kodi na mapato yanakusanywa vizuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi,” alisema Dk. Shein.

Alisema TRA na ZRB zimedhihirisha kuwa zinaweza kuleta mabadiliko na kutolea mfano wakati alipoingia madarakani Novemba 3 mwaka 2010, mapato yaliyokuwa yakikusanywa wakati huo yameongezeka kwa wastani wa mara nne.

“Uchumi unajengwa na wananchi wenyewe na unajengwa kwa Serikali makini kukusanya kodi, hivyo lazima tuhakikishe kodi inakusanywa vizuri kwa sababu wapo binadamu ambao ni watiifu kwa nchi yao na wengine si watiifu na hawa ndio wanaopiga chenga,” alisema.

 

TRA

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, alisema kupitia mfumo huo kodi za Serikali zitakusanywa moja kwa moja kielektroniki bila kuhusisha mtu yeyote, kuanzia hatua ya mwanzo hadi mwisho.

Kichere alisema mfumo huo utakuwa ukikusanya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi ya ushuru wa bidhaa.

Alisema mfumo huo unalenga kupata taarifa sahihi za mauzo yote, uhakiki na kutuma taarifa kwa wakati kama ilivyobainishwa kwenye sheria za kodi.

“Tumekuwa tukikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za namna ya kujiridhisha kwamba kodi zitokanazo na miamala ya kielektroniki ni sahihi, namna ya kukusanya kodi bila kuathiriwa na utashi wa mtu, ukusanyaji wa kodi kwa wakati,” alisema Kichere.

Kamishna huyo alisema utekelezaji wa mfumo huo utafanywa kwa awamu tatu ambapo ya kwanza itahusisha ujenzi wa mfumo na kuunganisha kampuni za Airtel, Vodacom, Tigo, TTCL, Zantel, Halotel, Smile na Smart.

Alisema hadi sasa tayari Halotel, Smart na TTCL zimeunganishwa katika mfumo huo na Smile iko kwenye hatua za mwisho.

Kichere alisema awamu ya pili itahusisha kuunganisha mfumo huo na taasisi za kifedha wakati awamu ya tatu itahusisha mifumo yote ya taasisi na makampuni yanayotoa huduma za malipo kielektroniki.

Alisema katika mfumo huo taarifa sahihi za miamala ya huduma zitolewazo na kampuni za mawasiliano ya simu zitahusisha sauti, vocha, ujumbe mfupi, bando, miamala ya kifedha baina ya simu na simu, simu na benki, ala, miito na malipo ya huduma mbalimbali.

Kwa upande wa miamala ya kibenki, alisema itahusisha kadi za kutolea fedha, benki kwa benki, benki na simu na malipo ya huduma mbalimbali.

Pia alisema miamala ya kielektroniki inayofanyika kutoa huduma za televisheni itahusishwa kwenye kununua vocha za visembuzi.  

Alisema pia mfumo huo umehusisha moduli tisa ambazo zinafanya kazi kuhakikisha kwamba kodi inakadiriwa, kukusanywa na kupelekwa moja kwa moja katika akaunti za TRA na ZRB zilizopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Hatukusudii kumwonea mlipakodi, kinachotakiwa ni kukusanya kodi ya Serikali kwa mujibu wa sheria. Mfumo huu hautasababisha ongezeko lolote la kodi kwa watoa huduma wala watumiaji wa huduma, kwahiyo hatutakiwi kuwa na wasiwasi,” alisema.

Kichere alisema mfumo huo utafanya kazi sambamba kwa kubadilishana taarifa na mfumo wa kusimamia mawasiliano ya simu uliopo TCRA ili kuwa na uhakika wa taarifa na hatimaye kupata kodi stahiki.

Alisema Serikali itapata taarifa sahihi kuhusu miamala yote inayofanyika kupitia mitandao, upatikanaji wa takwimu za uhakika kwa shughuli za maendeleo, kupata kodi stahiki kwa wakati, kuongeza ufanisi na uwazi katika ukusanyaji kodi na kujenga mazingira ya kuaminiana na kushirikiana.

Kamishna huyo pia aliwakabidhi Ipad (kifaa cha mawasiliano) Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Shein ambazo zitawawezesha kuangalia kiasi cha kodi kilichokusanywa popote pale watakapokuwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles