22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

JPM APIGA MARUFUKU WAFANYABIASHARA SOKONI KUTOZWA USHURU

ZIARA: Rais Dk. John Magufuli akiongea na wananchi wa Bomang’ombe, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro waliomsimamisha kwa muda wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) alipowasili kwa ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani humo jana

 

Na Upendo Mosha – Hai

RAIS Dk. John Magufuli amepiga marufuku halmashauri za wilaya zote kuwatoza ushuru wafanyabiashara wadogo katika masoko mbalimbali na badala yake wasimamie ukusanyaji kwa wafanyabiashara wakubwa.

Pia Rais Magufuli amenusa harufu ya ubadhirifu wa Sh bilioni 1.3 zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika mji mdogo wa Bomang’ombe na kuahidi kufuatilia zilipo fedha hizo.

Kauli hizo alizitoa mjini hapa jana wakati akizungumza na wafanyabiashara na wananchi katika soko la mazao na mbogamboga la Kwasadala lililopo Hai mkoani Kilimanjaro baada ya kumsimamisha akiwa njiani kuelekea Ikulu ndogo Mjini Moshi.

“Mkurugenzi wa halmashauri uko wapi? Njoo hapa, mnatoza ushuru hapa, nilishatoa maelekezo mara kadhaa na hapa narudia tena, hakuna kutoza ushuru kwa watu wanaoleta mikungu miwili ya ndizi.

“Watozeni wafanyabiashara wakubwa na fedha hizo pia mtumie kuboresha soko hili,” alisema.

Magufuli alisema anashangazwa na uwepo wa madiwani wanaoshindwa kutetea wananchi wanaowaongoza kwa sababu iwapo wangetenda kazi zao kikamilifu wangeshughulikia suala la ushuru na kuondoa kero hiyo ya muda mrefu.

“Huyu diwani wa Kata ya Masama Kusini angekuwa wa CCM ningemtumbua hapa hapa, haiwezekani anakwenda katika vikao vya halmashauri halafu ashindwe kuwatetea nyinyi wafanyabiashara wadogo kwa hoja kama hii, sasa hamtatozwa ushuru tena,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika eneo la Bomang’ombe, alisema anashangazwa mradi huo kuendelea kucheleweshwa wakati Serikali ilishatenga kiasi cha Sh bilioni 1.3.

“Nashangazwa hadi sasa barabara ya hapa haijajengwa na tayari Serikali ilishatenga fedha kiasi cha Sh bilioni 1.3, inavyoonyesha kuna jambo nyuma yake linaloendelea ambalo sio zuri, nitalifanyia kazi suala hili,” alisema.

Aliahidi kumtuma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kufuatilia zilipo fedha hizo zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara hiyo.

Kuhusu ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Sadala/Masama, alisema umekamilika kwa baadhi ya maeneo na imebaki ujenzi wa madaraja.

Kauli hiyo ilitokana na swali lililoulizwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu, aliyehoji ujenzi wa barabara za lami kwa urefu wa kilomita tano.

Pia Mchomvu alikiri kutengwa kwa kiasi hicho cha fedha katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, lakini hadi kufikia sasa kiasi kilichopelekwa ni Sh milioni 350 pekee.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli, aliahidi kuvipatia umeme baadhi ya vijiji vinavyounda Kata ya Masama Kusini kabla ya kumalizika kwa mwaka mmoja kwa sababu tayari Serikali imeandaa mipango ya kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,215FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles