NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amewaomba radhi Watanzania kwa kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru za mwaka jana, huku akitoa sababu mbili za kutokufanya shughuli hiyo.
Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru zilizofanyika jana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Dk. Magufuli alizitaja sababu zilizomlazimisha achukue uamuzi huo kuwa ni gharama kubwa zilizofikia Sh bilioni nne zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo, lakini pia alikuwa bado hajamaliza kuunda Serikali yake.
Ingawa fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo alizipeleka kwenye ujenzi wa barabara ya Mwenge- Morocco yenye urefu wa kilomita 4.3, uamuzi wake huo ulizua maneno, wengine wakimpongeza na wengine wakimpinga kwa hoja kwamba atafuta historia inayogusa taifa kwa vizazi vijavyo.
Magufuli ambaye jana alivunja mwiko kwa kuzungumza katika sherehe hizo, alisema:
“Nafahamu siku kama ya leo (jana) sitakiwi kuongea lakini naomba niwasalimu kidogo…nilipoambiwa kuhusu fedha za sherehe za Uhuru, nikauliza gharama nikaambiwa Sh bilioni nne, nikawauliza tena fedha hizo ni za nini na kitu gani kitafanyika? wakanijibu ni kwa ajili ya posho, chakula na vinywaji, nikawauliza hicho chakula watakula Watanzania wote? Wakaniambia hapana.
“Nikaagiza zile fedha zitumike kujenga barabara ambayo imepunguza msongamano na Watanzania wengi wanaitumia na watatumia katika maisha yao yote, inawezekana niliwakosea kwa kufanya hivyo mnisamehe, najua kuna watu waliumia kwa kukosa sherehe hizo lakini fedha zile mimi niliziona nyingi nikaamua kufanya maamuzi hayo,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Akieleza sababu za kukubali kufanya sherehe za mwaka huu, alisema ni pamoja na gharama ndogo lakini pia akiamini itakuwa ya mwisho kufanyika mkoani Dar es Salaam.
“Mwaka huu gharama ni ndogo sana, hakuna hata chakula baada ya sherehe hii, hakuna dhifa ya taifa kwa hiyo tukimaliza hapa ndio tumemalizana,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na umati uliokusanyika uwanjani hapo.
“Ni matumaini yangu itakuwa sherehe ya mwisho kufanyika Dar es Salaam, ni matumaini yangu kuwa sherehe za mwakani zitafanyika katika makao makuu ya nchi Dodoma, wapenda gwaride itabidi wasafiri mpaka Dodoma,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika miaka 55 ya Uhuru, alisema nchi imepiga hatua kubwa katika masuala mbalimbali hasa ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi ikiwemo barabara, madaraja, vivuko pamoja na uboreshwaji wa huduma za jamii.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kulinda mipaka ya nchi na kuwapo kwa mshikamano wa wananchi bila kujali ubaguzi wa rangi, dini na kabila.
“Nawashukuru hawa wazee 17 wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere kwa kutuletea Uhuru, isingekuwa wao ukute tungekuwa tunatawaliwa mpaka sasa, tuendelee kuwa na umoja na mshikamano,” alisema Dk. Magufuli.
Mbali na hilo, Dk. Magufuli pia alizitaja changamoto zinazoikabili Serikali yake zikiwamo umaskini, ukosefu wa ajira, upatikanaji wa huduma za jamii na rushwa.
“Tutaendelea kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuchukua hatua kali na kuwatumbua hadharani waliozoea kula hadharani,” alisema Dk. Magufuli.
Aliwataka wananchi kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kupambana na rushwa kwa kuwa suala hilo ni saratani.
Viongozi mbalimbali walihudhuria hafla hiyo akiwemo rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na mke wake, mama Mwanamwema, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Wengine ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na wake zake wawili, mama Siti na mama Hadija.
Walikuwapo pia mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, mama Fatuma Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na mke wake, mama Shadia Karume, Mke wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, mama Salma Kikwete.
Hata hivyo, Mke wa Rais Magufuli, Mama Janeth, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Kikwete hawakuwapo katika maadhimisho hayo, huku kukiwa na taarifa kuwa wapo nje ya nchi.
Mbali na hao, hakuna Waziri Mkuu yeyote mstaafu aliyehudhuria sherehe hizo wala uwakilishi wa kiongozi yeyote kutoka nje ya nchi pamoja na juzi kutolewa taarifa kuwa kutakuwa na ugeni wa viongozi hao watakaoongozwa na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
Mbali na hao, sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amiri Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuberi Ali Maulid pamoja na mawaziri.
Viongizi wa kisiasa waliokuwapo katika ghafla hiyo ni pamoja Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa UDP Taifa, John Cheyo na Mwenyekiti wa Taifa wa UPDP, Fahmi Dovutwa.
Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa gwaride na shamrashamra za vikundi vya ngoma katika sherehe hiyo, hakukuwa na shughuli ya urushaji wa ndege za kivita kama ilivyo kawaida ya miaka iliyopita, pia hakukuwa na tukio la halaiki ambalo hufanywa na watoto wanaokuwa wamevalia nguo zenye rangi za bendera ya Tanzania.