JPM AMTAKA BOSI DAWASA AACHIE NGAZI

0
1032
RAIS Dk. John Maguful
RAIS Dk. John Maguful

NORA DAMIAN Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amemtaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa),  Archard Mutalemwa, kustaafu haraka kabla mabaya hayajamkuta.

Amesema mtu anaweza akawa na umbo zuri ambalo halizeeki lakini umri huwa unakwenda hivyo akamtaka astaafu na kuwaachia nafasi hiyo vijana.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji Ruvu Juu mkoani Pwani ambako anaendelea na ziara yake.

“Wapo watu wanaouliza Mutalemwa atastaafu lini?   Mimi nilianza kumsikia tangu nikiwa sekondari, napenda kuzungumza kwa uwazi ndugu yangu, jiandae kustaafu haraka kabla mabaya hayajakukuta.

“Nafahamu data (taarifa) zako zote ndiyo maana nazungumza kwa ‘polite language’.

“Inawezekana waziri akawa rafiki yako kama ambavyo mawaziri wote wamekuwa marafiki zako lakini this is your time (huu ni wakati wako), umefanya kazi nzuri waachie vijana.

“Kama umenisikia nielewe, kama hujanielewa usije kusema…najaribu kuzungumza Kihaya. Mimi si kwamba sikupendi lakini najua ukikaa sana mahali si vizuri kwa hiyo si vibaya kuondoka,” alisema Rais Dk. Magufuli bila kufafanua.

Kuhusu mradi huo, alisema umeongeza uwezo wa uzalishaji maji   Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na kufikia mita za ujazo milioni 504 wakati mahitaji ni mita milioni 544.

“Dhambi ya wizara ya maji sasa imeanza kupotea kwa sababu nimeona kazi nzuri inayofurahisha, kazi imefanyika kweli,” alisema.

Katika hotuba hiyo, rais aliitaka wizara hiyo kukamilisha haraka miradi iliyokwama ukiwamo ule wa mkoani Lindi na ikiwezekana uongozi uhamie mkoani humo  uusimamie ukamilike.

Alisema kwa sasa upatikanaji wa maji kwa kila mwananchi ni wastani wa mita za ujazo 1,800 lakini endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kuna hatari ya kiwango hicho kushuka hadi kufikia mita za ujazo 883 mwaka 2035.

MADENI YA DAWASCO

Rais Dk. Magufuli alilitaka shirika hilo kufanya uhakiki wa madeni ya idara na taasisi mbalimbali yanayofikia Sh bilioni 40.

Alisema  kama ni halali wamwandikie waziri wa fedha na yeye atazikata fedha hizo katika bajeti za wadaiwa husika.

“Najua nipo kwenye mtego mkubwa lakini nasema mtu asipolipa ankara iwe taasisi yoyote hata kama ni Ikulu ninarudia kusema, kata.

“Tumezoea kudekezana, fedha wanazo lakini kulipa bili ya maji inakuwa tatizo… wewe kama ni mkurugenzi wa halmashauri, mkuu wa wilaya ama mkuu wa mkoa halafu bajeti ipo kwa nini ushindwe kulipia maji ama umeme?

“Maana yake hufai tutatafuta mwingine ambaye atajali kulipa umeme na maji na tukifukuza kama 20 hivi wale watakaokuja watakuwa wanawahi kwenda kuulizia ankara za maji,” alisema.

Hata hivyo alilitaka shirika hilo kulipa deni inalodaiwa na Tanesco la Sh bilioni 8.7.

“Wizara inalalamikiwa kwa mambo mengi na mengine nina ushahidi nayo, kuna ankara za kubambikiziwa, maji hupati lakini kila mwezi unaletewa ankara na wanajua namna ya kuchezea mita,” alisema.

Dk. Magufuli alikituhumu kiwanda kimoja  (bila kukitaja) cha  Dar es Salaam ambacho alisema kilifungiwa bomba la maji bila kupitishwa kwenye mita na kampuni moja iliyokuwa inajenga barabara ilikuwa hailipi ankara za maji.

WAZIRI WA MAJI

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, alisema ili kudhibiti upotevu wa maji utafungwa mfumo rasmi wa usomaji mita kwa njia ya mtandao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here