*Ni kutokana na kupandisha bei ya umeme
* Bosi wa Ewura hatihati, hofu yatanda
RENATHA KIPAKA, Bukoba na na ASHA BANI, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba Tanesco.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa kutokana na kutenguliwa kwa Mramba, Rais Dk. Magufuli amemteua Dk. Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco.
Kabla ya uteuzi huo Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akiwa mjini Bukoba jana Rais Dk. John Magufuli, alisema amekerwa na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.
Kutokana na hali hiyo, amesema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa, alipokuwa akitoa salaamu za Mwaka Mpya baada ya ibada ya Jumapili iliyofanyika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma mjini hapa.
Alisema uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), kutangaza ongezeko la bei ya umeme kuanzia Januari mosi, mwaka huu umefanyika bila kumwarifu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan au yeye mwenyewe.
Kutokana na hali hiyo, Rais Dk.Magufuli alimshukuru na kumpongeza, Profesa Muhongo kwa uamuzi wake wa kuzuia ongezeko la asilimia 8.5 lilitotangazwa juzi na Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlamgosi.
Alisema amesikitishwa na kitedo cha Ewura kupandisha bei ya umeme kiholela bila kuzingatia hali ya uchumi wa Watanzania ambao wengi wao ni wanyonge.
“Kilichonisikitisha ni kwamba waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi wala sikujua, nimesikia kwenye vyombo vya habari, hawakumuuliza waziri mwenye dhamana, wala Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.
“… haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye uamuzi peke yake bila kushirikisha mamlaka nyingine, ndugu zangu haya nayo ni majipu ya kutumbuliwa na wapo wengi,” alisema Rais Dk. Magufuli huku akishangiliwa na waumini wa kanisa hilo.
Alisema Watanzania wanapaswa kumwombea na kuliombea Taifa, kwani majukumu yanayomkabili ni makubwa yakiwamo ya kuwatumbua wale wanaojifanya ni miungu watu kwa kufanya kazi bila kujali hali za wenzao au kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Alisema katika kipindi hiki ambacho Taifa limejielekeza kutimiza dhamira yake ya kuanzisha viwanda ili kurahisisha maisha ya Watanzania wanyonge, Serikali imejipanga kuhakikisha wananufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Alisema hataki kusikia bei ya umeme inapandishwa, kwani kitendo hicho kinakwamisha malengo na jithada zake za kufikisha umeme vijiji ambako kuna Watanzania wengi.
“Umeme ndiyo unategemewa ili kutimiza ahadi yangu ya Tanzania ya viwanda, nawataka watumishi wa umma kufuata sheria na taratibu za kiutumishi na si vinginevyo,” alionya Rais Dk. Magufuli.
Ikiwa Rais Magufuli atalazimika kuchukua hatua hiyo kwa Mkurugenzi wa Ewura, pia kuna hatari ya kuvunjwa bodi ya mamlaka hiyo kwa sababu ilibariki ongezeko hilo.
Baada ya kuzungumza na waamini, Rais Dk. Magufuli alikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Ishozi ambacho kilibomolewa na tetemeko la ardhi Septemba 10, mwaka jana.
Watendaji waliotumbuliwa
Desemba 17, mwaka jana, Rais Dk.Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela.
Uamuzi huo ulifanyika siku moja baada ya Dk. Mwele kutangaza matokeo ya utafiti wa homa ya Zika bila kumshirikisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Utafiti huo ulifanywa na NIMR kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Bugando (Cuhas) hivi karibuni.
Katika matokeo hayo aliyoyatangaza, Dk. Mwele, alisema asilimia 43.8 ya watoto wachanga 80 kati ya watu 533 ambao walichukuliwa sampuli na kupimwa, wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya zika.
Desemba 7, mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alimng’oa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru na nafasi yake kurithiwa na Dk. Osward Mashindano.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa Dk. Mashindano anachukua nafasi hiyo na Mafuru atapangiwa kazi nyingine.
Kabla ya kuondolewa, Mafuru aliibuka na kauli tata ambayo ilionekana kupingana na masimamo wa Rais Dk. Magufuli kuhusu uamuzi wa baadhi ya taasisi za umma kuweka fedha kwenye akaunti maalumu (Fixed Deposit Accounts).
Mafuru aliitoa kauli hiyo Novemba 30, mwaka jana katika mahojiano maalumu na kituo kimoja cha redio.
Alisema haiwezekani watumishi wa umma kuiba fedha zinazowekwa katika Fixed Deposit Accounts kwa sababu miamala ya benki ni ya uwazi.
Akihutubia katika mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Bungo wilayani Kibaha mkoani Pwani, Rais Dk. Magufuli alisema aliitumbua bodi hiyo kutokana na kukiuka taratibu.
Alisema kitendo chao cha kuidhinisha fedha hizo kuwekwa katika benki tofauti, ni tofauti na maelekezo kwani huo ndiyo ulikuwa mchezo unaofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali.
Rais Magufuli alisema kumekuwa na mchezo wa wakuu wa taasisi mbalimbali kuchukua fedha na kuziwekwa kwenye akaunti maalumu ambako serikali inakwenda kukopa kwa gharama kubwa.
ASKOFU KILAINI
Kwa upande wa Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa jithada zake za kuhakikisha analeta usawa na uwajibikaji kwa watendaji wa uma.
Alisema hali ya sasa kwa utendaji wa Serikali imebadilika hasa unapokwenda ofisini hakuna usumbufu wa kusubiri mtumishi wala tabia ya kuombwa kitu kidogo au kauli ya kusema umetuachaje.
Alisema Watanzania wanatakiwa kutumia sherehe za mwaka mpya 2017 kujitathimini na kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza hasa kwa mwaka uliomalizika, hususan majanga ya tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka jana na kusababisha maafa na vidonda kwa katika Mkoa wa Kagera.
Muhongo apiga ‘stop’
Juzi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kusitisha bei mpya ya umeme iliyotangazwa na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlamgosi.
Taarifa ya kusitisha kwa bei hiyo ilitolewa na Profesa Muhongo kupitia barua yake kwa Ewura.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu alisema kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu nne, ikiwamo kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.
“Ewura walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei kupanda, wao wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni kwamba Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.
“Hivi tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita Ewura na Tanesco tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao wametangaza hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa Muhongo.
Katika sababu ya tatu ya kusitisha bei hiyo, Profesa Muhongo alisema hakuna ukweli kuwa kupandisha bei ya umeme kutasababisha Tanesco imalize matatizo yake kifedha.
Desemba 30, mwaka jana kabla ya mwaka mpya wa 2017 kuanza, Ewura ilitangaza kuridhia ongezeko la bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 8.5.
Ewura imepitisha ongezeko hilo linalotajwa kuwa litawaumiza watumiaji wa umeme, baada ya kuyafanyia uchambuzi wa kina maombi yaliyowasilishwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Uamuzi huo, ulitangazwa na Ngamlamgosi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam.
Alisema katika maombi ya awali yaliyowasilishwa Oktoba 4, mwaka huu, Tanesco ilipendekeza gharama za umeme ziongezeke kwa kiwango cha asilimia 18.19 jambo lililokataliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura.