27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amesahau aliposema mgogoro wa Z’bar haumhusu?

dk-shein-akiteta-jambo-na-rais-magufuliNa BALINAGWE MWAMBUNGU

IMETOKEA Hong Kong, inaweza kutokea Tanzania pia. Vijana wa ‘kizazi kipya’ ambacho kimekuwa kikifanya harakati kutaka mabadiliko ya uhuru zaidi na utawala wa kidemokrasia nchini humo, kimefanikiwa kushinda viti kadhaa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Septemba 4, 2016 na kuwaingiza wanaharakati hao katika Baraza la Kutunga Sheria (LegCO).

Vijana hao wanaunga mkono harakati za kutaka kukinasua Kisiwa cha Hong Kong kutoka utawala wa China Bara na kusimamia mambo yake yenyewe. Kisiwa hicho kilikuwa koloni la Uingereza kwa miaka 156, lakini walikirejesha China usiku wa Juni 30, 1997.

Lakini pamoja na kufanikiwa kupata viti katika Bunge, vijana hao ambao walikuwa wanaongozwa na Jonathan Law, chini ya vuguvugu lililoitwa “Umbrella Protests” lililoanza kampeni zake 2014 na kuunganisha nguvu na vyama vingine vya upinzani, bado wabunge wanaounga mkono China, watakuwa na viti vingi. Bunge hilo lina jumla ya viti 70.

Wanasiasa hao wapya wanadai uhuru na demokrasia zaidi kutoka Beijing na kwamba China inaingilia masuala ya kisiasa ya Hong Kong ambapo ni kinyume cha mapatano ya awali, kwamba kutakuwa na nchi moja lakini tawala mbili; one country, two systems.

Naliangalia suala la Hong Kong na kulinganisha na hali ya hapa Tanzania. Tanzania ni nchi moja, lakini kuna tawala mbili; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Tanzania bara, kama ilivyo China kwa Hong Kong, inaonekana kuwa kikwazo kwa Zanzibar ambayo inapenda kuwa sehemu ya Tanzania lakini pia ibaki na utambulisho wake, iendeshe mambo yake yanayohusu Zanzibar kwa uhuru.

Miaka ya hivi karibuni, pamekuwapo na madai kwamba Zanzibar inaonewa kwamba Serikali ya Muungano imenyang’anya baadhi ya mambo ambayo hayakuwa ya Muungano na hivyo kuzua malalamiko kwamba mwisho wa siku, Zanzibar itapoteza utambulisho wake. Wazanzibari wengine wanakwenda mbali zaidi na kusema kamwe nchi yao haiwezi kuwa koloni la Tanganyika.

Ubishani mkubwa ulitokea wakati wa Bunge la Katiba (ingawaje liliishia njiani), wajumbe kutoka Bara hasa wa Chama Cha Mapinduzi, walitetea sana suala la Serikali mbili kwa sababu ya ubinafsi zaidi wa chama chao, kuliko kujenga hoja na kuushawishi umma wa Watanzania kwamba kulikuwa na umuhimu kuendelea na mfumo wa sasa wa tawala mbili.

Wazanzibari kwa upande wao, walikwenda Dodoma wakiwa wanaunga mkono mapendekezo ya Tume ya Jaji Joseph Warioba ya kuwa na Serikali tatu kama suluhisho la kuondoa kile kinachoitwa ‘kero za Muungano’. Wazanzibari walitaka mambo yaliyokuwa kwenye makubaliano ya Muungano mwaka 1964, ndiyo yaendelee kutambuliwa kuwa mambo ya Muungano. Lakini inaelekea walizidiwa nguvu au ‘walilainishwa’ na waparaganyika. Hoja ya pamoja waliyotoka nayo Zanzibar, haikupata mtu wa kuisimamia.

Mwaka 2015 haukuwa wakati mwafaka wa kupeleka hoja ya mabadiliko ya Katiba kwa kuwa ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu na kwa kuangalia upepo ulivyokuwa unavuma, Chama Cha Mapinduzi kisingeweza kuhimili vishindo viwili, kuundwa kwa Katiba mpya na mabadiliko ya mfumo kutoka mfumo wa Serikali mbili kwenda wa Serikali tatu.

Kule Zanzibar tulishuhudia vuguvugu la uamsho likiweza kuwashawishi vijana wengi wa Zanzibar kwamba matatizo yao, ukosefu wa ajira na hali mbaya ya kiuchumi vinasababishwa na Serikali ya Muungano kutoipa Zanzibar umuhimu stahiki.

Wazanzibari katika ujumla wao wanasema misaada na miradi inayofadhiliwa na wabia wa maendeleo, haiwafikii. Wanataka Zanzibar iwe na uwezo wa kukopa kutoka mashirika ya kimataifa na kuingia mikataba na nchi wahisani.

Aidha, Wazanzibari walifufua hoja ya kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), hoja ambayo ilileta mfarakano mkubwa bungeni mwaka (1995) na ikasababisha wabunge wa bara kuunda kundi la G55 na kutaka Serikali ya Tanganyika irejeshwe.

Uamsho lilipata nguvu visiwani na likaonekana kuwa ni tishio kwa chama tawala na Serikali ya Muungano, lakini lilikuwa linavumiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ingawa hakuna sheria inayokataza uhuru wa kutoa maoni au kujiunga na kikundi chochote halali, ikaibuliwa hoja kwamba Uamsho ni kikundi cha watu hatari na kinaweza kuleta madhara makubwa kwa nchi.

Vuguvugu la Uamsho likasambaratishwa kwa madai kwamba lilikuwa la kigaidi na lilikuwa linachochea uasi. Hadi leo hii viongozi wake wanasota rumande na kesi yao inaendelea kupigwa kalenda.

Nailinganisha hali ya Zanzibar na ilivyokuwa kule Hong Kong mwaka 2014, ambapo vijana wa kizazi kipya waliingia mitaani wakidai mabadiliko tofauti na Zanzibar ni watu wa makamo ambao wamekuwa mstari wa mbele wa kutaka kuinusuru Zanzibar isimezwe na Tanzania bara.

Wanasema wanaosema wataimarisha Muungano, wana maana ya kuingiza mambo ambayo hayakuwamo kwenye mapatano ya Muungano na hivyo kuipunguza madaraka ya ndani ya nchi yao.

Kwa Wazanzibari katika umoja wao, wanataka Zanzibar ibaki kuwa nchi na katika hili hawatofautiani. Itikadi yao katika hili ni moja. Ndio maana utawala wa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alifanya mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar mwaka 2010 ambayo sasa inatamka kwamba Zanzibar ni nchi, tamko ambalo linakwenda kinyume na la Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Lakini nani anajali? Baadhi ya wanasiasa na wanasheria wakasema Karume alikuwa amevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa dhidi yake.

Kiongozi wa nchi anapotamka hadharani tena akiwa Zanzibar kwamba ataimarisha Muungano na kwamba Muungano hauwezi kuvunjika yeye akiwa madarakani, ni kauli wasiyopenda kuisikia Wazanzibari. Kwa wanaowajua Wazanzibari, walikuwa wanashangilia kuonesha kwamba wanakubali kauli yake, lakini ndani ya nyoyo zao ni tofauti.

Zanzibar wanataka kuwa na eneo lao la kutafuta gesi asilia na mafuta na wanasema katika hili hawataki mkono wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, gesi na mafuta si masuala ya Muungano. Mkuu wa nchi azisome vizuri siasa za Zanzibar!

Kwa Wazanzibari kuimarisha Muungano, maana yake kunyofoa madaraka kutoka Serikali ya Mapinduzi na kuyafanya ya Muungano vinginevyo nani alitamka kwamba Muungano uko hatarini kuvunjika?

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipinga kwa nguvu zake zote kuirudisha Serikali ya Tanganyika akiogopa kwamba kwa kufanya hivyo, Wazanzibari walikuwa na woga wa kumezwa.

Mambo ya awali yaliyomo kwenye makubaliano ya Muungano yalikuwa 11 tu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama, Polisi, Uraia na Uhamiaji, Usimamizi wa Sarafu na Fedha, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kodi ya Mapato, Usafiri na Usafirishaji wa Anga, Posta na Simu, Bandari, Mikopo na Biashara na Nchi za Nje na Utumishi wa Muungano.

Mambo mengine Wazanzibari wanadai yaliyoongezwa kinyemela hadi kufikia 21 au 22 na wanataka yawekwe mezani yajadiliwe upya. Tayari wamekubaliwa kuingia mikataba ya utafiti wa mafuta na gesi kama Zanzibar.

UCHAGUZI MKUU

Ni habari iliyo wazi kwa wananchi wa Pemba na Unguja kwamba Chama Cha Mapinduzi kilipigwa chali na Chama cha Wananchi (CUF) na kilichofanyika kufuta matokeo ya uchaguzi ni ‘uhuni’ maana aliyeyafuta matokeo hayo hakuwa na madaraka kisheria.

Lakini mkuu wa nchi Rais John Magufuli anatonesha vidonda vya wapiga kura anapotamka hadharani kwamba uchaguzi wa marudio ambao CUF walisusia ulikuwa huru na wa haki na kwamba hakutakuwa na uchaguzi wa marudio.

Amesahau kwamba aliwahi kuombwa kuingilia kati mgogoro huo wa kisiasa na alijibu kwa mkato kwamba masuala ya uchaguzi wa marudio Zanzibar yalikuwa hayamhusu!

0713 262 672

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles