27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AKWEPA MTEGO WA KUVUNJA KATIBA

AMINA OMARI – KOROGWE na AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM

WAKATI kukiwa na wimbi la watu wanaotaka Rais Dk. John Magufuli aongezewe muda wa uongozi, jana alikwepa mtego huo kwa kusema ameapa kuilinda Katiba, hivyo suala la kuongeza muda haliwezekani.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kituo cha mabasi kilichopo katika eneo la Kilole, Wilaya ya Korogwe Mjini mkoani Tanga.

Kauli hiyo ilifuatia wito uliotolewa na Mbunge wa Korogwe Mjini, Steven Ngonyani (Maji Marefu), ambaye awali alisema Rais Magufuli inafaa aongezewe muda wa miaka 10 baada ya kipindi chake cha kikatiba kwisha ili amalize kutekeleza ahadi zake.

Mbali na Ngonyani, Juni 26, mwaka huu,    Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, naye alisema kama si suala la Katiba, Rais Magufuli angefaa kuongoza miaka yote.

Katika kuendeleza falsafa hiyo, aliyewahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Laurence Mabawa, hivi karibuni alifanya mkutano na waandishi wa habari na kutangaza  kampeni aliyoipa jina la ‘Magufuli Baki’, huku akisema atazunguka mikoani kuitangaza.

 

ARUKA MTEGO WA KIKATIBA

Jana Rais Magufuli akihutubia mjini Korogwe, alisema: “Mheshimiwa Ngonyani naomba nikuambie, nimeapa kulinda Katiba na sheria, ndiyo maana mtani wangu ulipozungumza hapa kwamba unataka miaka 20 zaidi nilielewa unataka niishi miaka 20 zaidi sio miaka 20 ya urais, hilo haliwezekani,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kazi ya urais ambayo inaambatana na kutumbua majipu (kuwashughulikia watumishi) ni ngumu  kwa kuwa yapo majipu mengine yameshaoza.

“Majipu mengine yameoza, yaliyooza mengine yanakutumbukia mdomoni, unataka kwenda kula unashindwa hata kwenda kula, ni kazi ngumu, ni kazi ‘very risk’ (hatari), lakini lazima nifanye kwa niaba ya Watanzania,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema anafanya kazi ya kutumbua majipu kwa sababu ni jasiri na asipofanya hivyo huenda hakuna atakayeweza.

“Nisipotumbua nani atakuja tena kutumbua? Inawezekana asipatikane mwingine wa kutumbua, sasa angalau  nitumbue yote kwa sababu mimi ni jasiri wa kutumbua, atakayekuja baada ya miaka yangu akute yote yameshatumbuka,” alisema Dk. Magufuli.

 

ASISITIZA KUTOGAWA CHAKULA

Mbali na hilo, Dk. Magufuli alisisitiza kuwa Serikali yake haitopelekea msaada katika maeneo yenye njaa kwa kuwa wana uwezo wa kulima.

“Wakati wa kukaa kwenye magenge na kupiga maneno umepita, mnakaa mnasubiri mletewe, havitakuja kwenye utawala wangu, mnakaa mnasubiri tu alafu mnasema tuna njaa, kwangu mimi njaa nafuu ikuue kuliko nikuletee chakula.

“Kwa sababu mwenzako ana chakula wewe huna, wenzako wameotesha mahindi wewe pale ya kwako hayapo, hakuna kuvumilia hali ya namna hiyo, lazima niwaeleze ukweli, nafuu mnichukie, lakini nimewaeleza ukweli,” alisema Dk. Magufuli.

 

KUBADILISHA SHERIA YA VAT

Rais pia amemwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha bungeni muswada wa sheria wa kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye fedha zinazotelewa kwa mkopo wenye masharti nafuu kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Unapotoza VAT kwa mradi ambao umefadhiliwa kama barabara na wewe unaiweka kodi pamoja na kwamba ni kwa mujibu wa sheria, inabidi Serikali itenge tena fedha nyingine za kulipia VAT kwa yule mkandarasi.

“Na wakati mwingine ujanja unaofanyika unamlipa mkandarasi pesa yote ya VAT, yeye anakwenda Mamlaka ya Mapato (TRA) anakwenda kuongea nao analipa asilimia 40, kwa hiyo anayeumia ni Serikali,” alisema.

Hivyo alimwagiza Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Suleiman Jaffo, kusimamia makubalino ya mkataba walioingia kati ya Serikali na benki ya dunia kuwa miradi yote ya maendeleo inayofadhiliwa na benki hiyo haitaweza kutozwa kodi.

“Hivyo fedha zilizotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kutekeleza na kuendeleza miradi mbalimbali  ya maendeleo wanayoitekeleza katika nchi hii kama Dola milioni 168 na Dola milioni 200 makubaliano yatabaki hivyo hivyo, swala la VAT halitahesabika katika miradi hiyo,” alisisitiza.

Hata hivyo Dk. Magufuli alisema kuwa swala la VAT litaendelea kuangaliwa vizuri katika miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

 

AAGIZA VIFAA VYA RELI KUACHIWA

Alisema pia kuna vifaa vya kutekeleza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ambavyo vimesababisha uchelewesheji wa mradi kwa sababu vilizuiwa bandarini hadi vilipiwe kodi.

Dk. Magufuli alisema ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 300 unaogharimu Sh trilioni mbili, unasimamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

“Kodi inakusanywa na Serikali, reli ni ya serikali, ni ujinga kujiumiza kiasi hicho, kutokana na sheria tunazoziweka ambazo zinatubana wenyewe na kukwamisha shughuli zetu za kujiletea maendeleo kwa haraka,” alisema.

 

ATOA SIKU 14 KWA MKANDARASI

Akiwa wilayani Handeni, ametoa siku 14 kwa mkandarasi ambaye tayari ameshalipwa Sh bilioni 2.8 kuchimba mabwawa ya maji katika eneo la Mkata.

“Natoa wiki mbili mkandarasi wrudi kwenye eneo la mradi na kuanza kutekeleza kwa gharama zao wenyewe mpaka pale Serikali itakapotoa cheti ndipo ataweza kulipwa tena fedha nyingine,” alisisitiza.

Aidha alisema kuwa Serikali yake haiwezi kuvumilia kuona fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi hazitumiki inavyoelekezwa, hivyo ni lazima mkandarasi aliyepewa mradi na mshauri arudi katika eneo la mradi haraka.

 

MAKAMBA ALIA NA KIWANDA CHA CHAI

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, January Makamba, alimuomba Rais Magufuli kuingilia katika ufufuaji wa kiwanda cha kuzalisha chai cha Mponde.

Alisema kuwa kufungwa kwa kiwanda hicho kulitokana na wakulima kumkataa mwekezaji na kutaka Serikali ikichukuwe na kutafuta namna bora ya kukiendesha.

“Wakati mwingine Rais unasema tusifukue makaburi, lakini inalazimika kuyafukua ili tuweze kusonga mbele kwani wakulima wanalalamika kwa kufungwa kwa kiwanda kile,” alisema Waziri Makamba.

Alisema licha ya Serikali kuagiza mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza kwenye viwanda, lakini masharti ya uwekezaji yaliyotewa na mfuko wa LAPF yanarudisha nyuma juhudi hizo.

“Kuna changamoto mbili, moja Serikali imemshtaki mwekezaji wa awali, lakini mfuko wa LAPF wao wanataka kuendesha kiwanda na mwekezaji ambaye wakulima wamemkataa na Serikali imemshtaki,” alisema Makamba.

Alisema kuwa ili kiwanda hicho kiweze kufufuliwa, kinahitajika kiasi cha Sh bilioni 4, kwani tayari kina miundombinu yote, hata ukiweka jenereta kinaweza kufanya kazi vizuri.

Jana Rais Magufuli alihitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Tanga, ambako pamoja na mambo mengine, Jumamosi ya wiki iliyopita yeye na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, waliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Chongoleani, Tanga.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Nampongeza mheshimiwa kwa uchapaji kazi ilam ajitahidi juu ya suala la ajira maana vijana wamemaliza vyuo wako mtaani tu na wakati wengi wao wakiwa watoto wa wakulima ambao ndiyo mheshimwa rais anawapigania kama tabaka la chini, sawa ajira zimetangazwa lakini hazionekani SIJUI ZITATOKA LINI

  2. Nikweri magufuli analo sema kuna baadhi ya wananchi hawaji shughurushi kwakukaa vijiwen.kuhusu urais naunga mkono walio tangulia kusema aongoze miaka 20 angalau sisi wamyonge tuheshimike asante

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles