22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 3, 2023

Contact us: [email protected]

JPM AKUTANA NA WAZIRI WA ISRAEL


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Avigdor Lieberman Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika jana, yalihudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Balozi wa Israel hapa nchini, Noah Gal Gendler, viongozi wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli, alimshukuru Lieberman kwa kuitembelea Tanzania na alimuhakikishia Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuukuza zaidi na kuuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya mataifa hayo.

Rais Magufuli ametaka makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel katika maeneo mbalimbali yakiwamo ulinzi, usalama, mafunzo na masuala ya kiuchumi yatiwe saini haraka ili utekelezaji uanze mara moja.

“Tanzania na Israel ni marafiki wa miaka mingi, nataka kuona urafiki wetu unakua zaidi, nawakaribisha wawekezaji kutoka Israel kuja kuwekeza katika kilimo, madini na gesi na pia kuwepo ndege za moja kwa moja kutoka Israel hadi Dar es Salaam na Kilimanjaro ili kukuza utalii,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na makubaliano hayo, Rais Magufuli alimwomba Lieberman kumfikishia ujumbe Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wa kumwalika kutembelea Tanzania na pia kuanzisha ofisi ya ubalozi hapa nchini badala ya kutumia ofisi za ubalozi zilizopo Nairobi, Kenya.

Kwa upande wake, Waziri Lieberman alimshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha na kufanya naye mazungumzo.

Pia amemhakikishia Israel imejipanga kuongeza uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania katika maeneo yote ya makubaliano na kusaidia kilimo na usindikaji wa chakula.

Aprili 6 mwaka jana, Rais Magufuli alikutana na balozi wa Israel nchini, Yahel Vilan, Ikulu Dar es Salaam na kutoa wito kwa Waziri Mkuu Netanyahu kufungua ubalozi wake hapa nchini.

Mwaka juzi, Israel ilifungua ofisi ndogo ya ubalozi nchini.

Katika mazungumzo na balozi huyo, Rais Magufuli alimhakikishia Tanzania imedhamiria kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano wake na taifa hilo la mashariki ya mbali, hasa katika masuala ya uwekezaji, biashara, utalii na uboreshaji wa huduma za kijamii.

Rais Magufuli alisema ili kufanikisha dhamira hiyo, Tanzania imefungua ubalozi nchini Israel na amemwomba balozi huyo kupeleka ujumbe kwa Netanyahu kuhusu nchi hiyo kufungua ofisi za ubalozi nchini.

“Naamini uhusiano na ushirikiano wetu utaongeza manufaa zaidi kwa nchi zetu na watu wake.

“Nimefurahishwa sana na taarifa kuwa watalii wataanza kuja kwa ndege moja kwa moja kutoka Tel Aviv, Israel na hivi karibuni ndege yenye watalii zaidi ya 200 itakuja nchini kwetu.

“Nawakaribisha sana watalii na wawekezaji kutoka Israel,” alisema Rais Magufuli.

Balozi Vilan aliahidi Israel itajenga jengo la wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo, ikiwamo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,270FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles