Na KULWA MZEE-DODOMA
MBUNGE wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema), amemwomba Rais Dk. John Magufuli kujaza nafasi za aliyekuwa Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk. Abdallah Possi na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ili wabunge wa CCM watulie.
Nafasi ya Dk. Possi iko wazi tangu Januari mwaka huu alipoteuliwa kuwa balozi, huku ya Profesa Muhongo ikiwa wazi tangu Mei 24, uteuzi wake ulipotenguliwa na Rais Magufuli kutokana na uchunguzi wa ripoti ya kwanza ya makinikia.
“Namuomba Rais ajaze nafasi ya Profesa Muhongo na Possi, kwa sababu nimeona kuna baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanashindana kutafuta nafasi hizo kwa kushambulia upande huu. Kwa hiyo naomba niseme tu kwamba, afanye uteuzi huo haraka,” alisema Haonga alipopewa nafasi ya kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2017/18 bungeni jana.
Kabla ya kumaliza, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, aliyekuwa akiendesha kikao cha asubuhi, alimkatisha kwa kusema “wewe changia bajeti, acha haya mambo”.
Baada ya maelezo hayo, Haonga alisema: “Mheshimiwa mwenyekiti, baada ya ushauri huo naomba sasa niendelee kuchangia bajeti iliyo mbele yetu.”
PAULINE GEKUL
Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), akichangia bajeti, alisema Serikali inatakiwa kuwa wazi ili wabunge waishauri kwani kwa kuleta vitu vya mafungu hawatapata nafasi ya kuishauri.
“Kwa sasa Serikali imekusanya asilimia 70, leo mnaleta trilioni 31/- wakati makusanyo ni asilimia 70. Mgetuambia ukweli wapi mmekwama kuliko kuleta makadirio makubwa.
“Serikali imepanga kuzimisha kabisa Serikali za Mitaa, vyanzo vyote mmeshindwa mnakuja kuchukua katika vyanzo vyetu huku.
“Bajeti hii ya kuua Serikali za Mitaa kwa asilimia 100, kwani hadi sasa Serikali haijakusanya kodi ya majengo, ni bora mngetuachia sisi halmashauri tukakusanya.
“Sasa hivi mmetuachia makusanyo ya kodi katika masoko na stendi, wakati kuna watu wanahitaji mishahara na vyanzo hakuna.
“Fedha mnazokusanya mnadai mtarejesha, ni uongo hazirejeshwi, leo mnataka tuwatoze faini ya Sh 100,000, 200,000 hadi Sh 1,000 mtu akitupa taka, hata katika rambo, ilikuwa Sh 50,000 mmepandisha.
“Mmepandisha faini kutoka Sh 50,000 hadi milioni, hicho ndiyo chanzo mlichotuachia, kwanza hiki chanzo hakiwahusu, ni sheria ndogo za halmashauri,” alisema.
Alisema Serikali Kuu imeamua kunyonga halmashauri zote.
WILLIAM NGELEJA
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), alisema anaungana na wote wanaounga mkono bajeti hiyo asilimia 100.
Alisema Sengerema kuna mradi mkubwa wa maji ambao tayari umekamilika, kuna miradi kadhaa imebuniwa na kwamba bajeti hiyo imezingatia vizuri jimboni kwake.
“Hatuwezi kuzungumzia viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika, viwanda na reli inayojengwa vyote vinahitaji umeme mwingi sana.
“Kuna haja ya kushirikisha sekta binafsi kushirikiana na Serikali kuwekeza katika vyanzo vya umeme,” alisema.
JANET MBENE
Mbunge wa Ileje, Janet Mbene (CCM), alisema tozo ya mazao ifanyiwe kazi kwa kuweka tozo moja kwa mazao yote ya biashara na chakula.
Alisema pamoja na kuorodhesha kodi, TRA ianze kutoa elimu ya kulipa kodi, wafahamishwe walipakodi wanalipaje ili kupunguza usumbufu.
Alisema miradi ya kimkakati imekuwa ya siku nyingi, hivyo imalizwe mikataba ya uwekezaji, ulipaji wa fidia ili miradi ya mkakati ifanye kazi.