27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM akerwa na mkandarasi wa barabara

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mnivata na kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutompa kazi nyingine mkandarasi anayejenga barabara hiyo.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 50 ni sehemu ya barabara kuu ya Mtwara – Newala – Masasi (kilomita 210) na inajengwa na Kampuni ya Dott Services Limited ya nchini Uganda kwa gharama ya Sh bilioni 89.5.

Akizungumza jana wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo, Rais Magufuli alisema licha ya kucheleweshewa fedha lakini rekodi ya mkandarasi huyo si nzuri.

“Sijafurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huu, hauendi vizuri, makandarasi ya ovyo ovyo ndio yanapewa kazi.

“Inawezekana baada ya mimi kutoka Wizara ya Ujenzi mmepata mawaziri ambao wanawaeleza maneno matamu matamu, kwangu hayo yalishaisha, nataka barabara hii iishe.

“Nawafahamu makandarasi wote, hatuwezi kusubiri barabara tangu 2017 tunakwenda hadi 2019 watu hawajaona barabara, unachimbachimba mashimo tu,” alisema Rais Magufuli.

Aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutowapa kazi makandarasi wenye rekodi mbaya hata kama watakuwa wameshinda zabuni.

“Msiwape kazi hata kama wameshinda tenda, huwezi ukasubiri barabara miaka mitatu kilomita 50. Wizara ya Ujenzi, ‘consultant’ pamoja na mkandarasi mmeingia kwenye 18 zangu, nataka barabara iishe.

“Msimpe kazi nyingine yoyotemkandarasi huyu mpaka amalize kazi hii, hata kama ameshinda.

“Msimamieni usiku na mchana, mshauri kama hawezi ku – perform mfukuzeni, wasije Tanzania kufanya majaribio hapa ni mahala pa kazi,” alisema.

Aliitaka Wizara ya Ujenzi kutumia Sheria namba 17 ya 1997 na kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ili wale ambao hawana rekodi nzuri wafukuzwe.

Rais Magufuli pia alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele, kuongeza kilomita nyingine 100 na wakishapitisha bajeti waanze maandalizi ya ujenzi.

USHURU WA HALMASHAURI

Rais Magufuli alisema hakuna halmashauri itakayopata ushuru kwa kuwa walishindwa kusimamia vizuri zao la korosho.

“Hakuna ushuru wa halmashauri hata senti tano hampati, mkitaka ushuru msimamie vizuri zao la korosho, muwalipe wananchi bei nzuri ili na ninyi mkusanye ushuru wenu.

“Siwezi nikawalipa halafu nije niwakusanyie ushuru, ninajua Tandahimba mmejiandaa kwa ajili ya ushuru msahau.

“Halmashauri mmeshindwa kusimamia zao la korosho badala ya wakulima kupewa bei nzuri wanapewa mpaka Sh 1,500 halmashauri mpo mnaangalia tu wananchi wananyanyaswa.

“Namimi pia ni Waziri wa Tamisemi nione mkurugenzi ameniomba hizo fedha kama ataendelea kuwa mkurugenzi, nimwone wa kuja kuniomba hiyo fedha utaombea kijijini huku ukiwa unalima.

“Mkitaka mkajipange vizuri kwenye msimu unaokuja mnunue korosho mkusanye na ushuru lakini wananchi muwalipe fedha nzuri,” alisema Rais Magufuli.

NALIENDELE

RAIS Magufuli alikipongeza Kituo cha Utafiti cha Naliendele na kuiagiza Wizara ya Kilimo ikiimarishe na kukiongezea bajeti ya kutosha kwani kimesaidia katika utafiti wa zao la korosho.

Pia alikitaka kituo hicho kuendelea na utafiti wa kutengeneza juisi kupitia korosho na ikiwezekana hata kupata kinywaji chenye kilevi lakini kilichothibitishwa maabara.

“Mtengeneze gongo ya aina yake ambayo ni nzuri na kupitishwa kwenye vipimo vyote vya maabara…anayetaka kulewa kwa dakika mbili analewa kwa dakika mbili,” alisema Rais Magufuli.

WAZIRI WA UJENZI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kamwelwe alisema tayari ametekeleza maagizo ya Rais Magufuli na kwamba zaidi ya Sh bilioni 20 zimetolewa kwa ajili ya mkandarasi huyo na yule anayejenga Kiwanja cha Ndege Mtwara.

“Jana (juzi) niliongea na mwenzangu (Waziri wa Fedha) na tayari Sh bilioni 7 zimepatikana kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Mtwara hivyo, mkandarasi hana kisingizio cha kushindwa kufanya kazi.

“Licha ya fedha hizo pia Sh bilioni 16 zimeingizwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara Mnivata – Mtwara.

“Napambana kibiashara, Malawi walikuwa wanatumia Bandari ya Beira ambayo ni kilomita 800 hivyo, tukikamilisha barabara hii watahamia kufanya biashara Bandari ya Mtwara,” alisema Waziri Kamwele.

TANROADS

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tanroads, alisema ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mnivata unagharimu Sh bilioni 89.5 na itajengwa kwa miezi 21.

Alisema mkandarasi alianza kazi Aprili 2017 na hadi sasa ameshasafisha kilomita 43, kujenga tuta la barabara kilomita 32, tabaka la chini kilomita 19.63, tabaka kuu la msingi kilomita 14.25 na tabaka la lami kilomita 8.5.

Alisema maendeleo ya mradi huo yamefikia asilimia 48.23 na hadi sasa mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 22.8 kati ya madai yake ya Sh bilioni 38.8.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, alisema barabara hiyo ndiyo kiungo cha mkoa kwani inaunganisha wilaya zote na hutumika kwa usafirishaji wa zao la korosho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles