28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

JPM AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA KWA WABUNGE

Mbunge wa Nkasi, Ali Mohamed Kessy (CCM), akionesha funguo ya gari la wagonjwa baada ya kukabidhiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (kushoto) yaliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

 

 

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ametoa magari mapya matatu ya kubebea wagonjwa kwa wabunge watatu ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yao.

Magari hayo yalikabidhiwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi,  kwa niaba ya Rais Dk. Magufuli.

Waliokabidhiwa ni pamoja na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Munde Tambwe na mwenzake wa Mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga wote wa CCM .

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli ametoa magari hayo baada ya kuguswa na kilio cha muda mrefu cha wabunge hao waliokuwa wakiomba wananchi wao wapatiwe magari ya wagonjwa.

“Mheshimiwa Rais ameamua kuwakabidhi nyinyi haya magari kutokana na vilio vyenu ambavyo amekuwa akivisikia mara kwa mara, Keissy umekuwa hata ukitafuta miadi ya kuja kumwona Rais kwa suala hili, waheshimiwa wabunge wamekuwa wakiyazungumza haya kwa muda mrefu.

“Tunafahamu kila mbunge katika jimbo lake anahitaji kupata huduma kama hii na huduma kama hii ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa hiyo sisi Serikali kila tunapopata uwezo basi tunasaidia pale tunapoweza kufikia kwa wakati ule, tulishatoa magari mengine matatu kama haya Chalinze na vituo vingine vya Morogoro,”  alisema Balozi Kijazi.

Balozi Kijazi aliwapongeza wabunge hao kwa kupata magari hayo kwa ajili ya wananchi wao na amewasihi kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yadumu muda mrefu na yawahudumie wananchi wote bila kujali dini, kabila, itikadi zao za kisiasa wala makundi.

Wabunge hao walimshukuru Rais Magufuli kwa kusikia  kilio chao cha kuwasaidia wananchi magari ya kubebea wagonjwa na wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuwapigania Watanzania hasa wanyonge anayoifanya.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles