26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AIPA MAAGIZO WIZARA YA MIFUGO

Na Mwandishi Maalumu-Dodoma


RAIS, Dk. John Magufuli ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutumia  matokeo ya utafiti  wa wingi wa rasilimali za uvuvi za  Bahari Kuu uliofanywa na  meli ya utafiti   ya Dk. Fridtjof Nansen kutoka nchini Norway ili kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi nchini.

Meli hiyo imefanya utafiti kwa ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Akizungumza katika Bandari ya Dar es Salam kwenye hafla ya kuikaribisha  meli hiyo  baada ya kumaliza  kufanya utafiti wa siku 12 kwenye  bahari ya Tanzania na kuiaga kuendelea na safari ya utafiti kwa niaba ya Rais, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, aliitaka wizara na taasisi zote za Serikali  kutumia tafiti  zinazofanywa ili kuleta maendeleo katika sekta husika.

“Kufanya utafiti ni jambo moja na kutumia taarifa za utafiti uliofanyika ni jambo jingine, kwa hiyo hakikisheni mnatumia taarifa za tafiti hizi kikamilifu,” alisema  Balozi Kijazi.

Pamoja na hali hiyo alitoa siku 30 kwa watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) walioshiriki utafiti katika meli ya Dk. Fridtjof Nansen washirikiane na watafiti wenzao kuleta matokeo ya utafiti huo Serikalini ili uanze kufanyiwa kazi na hatimaye  kuleta tija kwenye Sekta ya Uvuvi.

Wakati huo huo Balozi Kijazi aliishukuru Serikali ya Norway, Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa ufadhili, utaalamu pamoja na kuisaidia Tanzania katika nyanja za sayansi za kwenye maji.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga  Mpina alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumtuma Katibu Mkuu Kiongozi kumwakilisha  katika hafla hiyo  na kumwomba kusaidia ununuzi wa meli ya utafiti.

Waziri Mpina alisema utafiti huo uliohusisha maji ya ndani na Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ), na ni wa kwanza kufanyika katika nchi yetu kwa Ukanda wa Uchumi wa Bahari, Wizara yake itahakikisha kuwa inatumia kikamilifu taarifa za utafiti huo ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi nchini.

Aliiomba Serikali kusaidia ununuzi wa meli ya doria kwenye ukanda wa bahari kuu ili kufanya doria za mara kwa mara  katika maji yetu na kulinda rasilimali za nchi.

“Tutapambana na wavuvi haramu bila suluhu hadi kuutokomeza uvuvi haramu hapa Tanzania, hatutoshindwa na tumedhamiria kwa dhati kufanikisha hili. Penye nia pana njia, tumepania.

“Kwa heshima na taadhima ninaamini kuwa Mheshimiwa  Rais atafanya kila awezalo kwa uwezo wake ili kuhakikisha kuwa sekta ya uvuvi inakuwa na rasilimali za uvuvi zinasimamiwa kwa njia endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Waziri Mpina.

Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini, Hanne-Marie Kaarstad, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanya utafiti huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika Nyanja mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles