25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AIDUWAZA CCM, ACT UTEUZI WA MGHWIRA

 

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam,

RAIS Dk. John Magufuli jana amemteua Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, mwenyekiti huyo wa chama cha upinzani, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Said Meck Sadiki.

Mbali na Mghwira, Rais Magufuli pia amewateua Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi (DIGP), Abdulrahman Kaniki na Meja Jenerali Issah Nassor kuwa mabalozi.

Kabla ya uteuzi huo, Meja Jenerali Nassor alikuwa Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Katika uteuzi huo wa watu watatu, uliozua mjadala na hata kuleta mshituko mkubwa ndani ya siasa za vyama vya upinzani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni ule wa Mghwira.

Ingawa hii si mara ya kwanza kwa Rais anayetokana na CCM kuwateua wapinzani katika nafasi mbalimbali, kinachozua maswali zaidi katika uteuzi huu wa sasa wa Mghwira, ni kumpeleka katika mkoa ambao ni ngome ya chama cha upinzani cha Chadema.  

Itakumbukwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa wakati wa utawala wake aliwahi kumteua kada wa CUF, Hamad Rashid kuwa mbunge, huku Rais mstaafu Jakaya Kikwete akimteua kiongozi wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia katika nafasi hiyo hiyo.

Mghwira ambaye amepewa cheo tofauti na kile cha ubunge, uteuzi wake umewafanya baadhi ya makada wa vyama vya pande zote kuanza kuhoji na hata kufikiri kwamba huenda ama kuna usaliti au ajenda za kiutawala wasizozijua.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya makada wa CCM wamekwenda mbali zaidi na kutafuta katiba ya chama chao na kuangalia kama cheo alichopewa Mghwira hakina madhara katika siasa zao.

Mghwira ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi aligombea urais kupitia ACT- Wazalendo na kushika nafasi ya tatu, akipata kura 98,763 nyuma ya Rais Magufuli aliyepata kura 8,882,935 na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa wa Chadema aliyevuna kura 6,072,848, sasa atalazimika kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM.

Si hilo tu, licha ya kuwa ni mwanasiasa wa upinzani, atabeba jukumu la kuwa  Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Mghwira ndiye aliyekuwa mpinzani wa kwanza kumpongeza Magufuli baada ya kushinda urais, pia miongoni mwa wapinzani wachache waliohudhuria hafla ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Uteuzi wake pia umekuja zikiwa zimepita siku kadhaa baada ya Rais Magufuli Aprili 4, mwaka huu kumteua mshauri wa ACT- Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Uteuzi wake unaelezwa na baadhi ya wachambuzi wa siasa za kishindani nchini kama ni mwendelezo wa wimbi la viongozi wa chama hicho ama kuondoka katika majukumu yao ya kichama au kuondoka jumla.

Mbali na Mghwira na Profesa Kitila, wengine walioondoka ndani ya chama hicho ni Katibu Mkuu wake, Samson Mwigamba ambaye aling’atuka Mei, mwaka jana na kusema anakwenda masomoni.

Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali ambaye amejiunga CCM na aliyekuwa Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa wa sekretarieti wa chama hicho, Habibu Mchange, ambaye aliondoka Desemba 10, mwaka jana.

Miongoni mwa watu wa mwanzo kuondoka ndani ya chama hicho ni aliyekuwa mgombea ubunge wa Morogoro Mjini, Selemani Msindi maarufu Afande Sele.

Afande Sele alitangaza uamuzi huo Desemba 15, mwaka jana baada ya kudai kutoridhishwa na viongozi wa chama hicho, akisema msimamo wao umekuwa haueleweki na anashindwa kujua iwapo msimamo wao ni kuunga mkono upinzani au CCM.

Mwingine aliyetangaza kujiondoa hivi karibuni ni aliyekuwa Mshauri wa chama hicho, Wakili Albert Msando, baada ya video yake akiwa ndani ya gari na msanii wa kupamba video za wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Gigy Money huku wakitomasana kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Akizungumzia uteuzi wa Mghwira, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema hawezi kutoa maoni.

“Siwezi kutoa maoni kwa sasa kwa sababu bado sijawasiliana na mwenyekiti (Mghwira) ambaye kwa sasa yuko Marekani,” alisema Zitto.

Akijibu swali kwa nini anashindwa kutoa maoni kwa sasa tofauti na ilivyokuwa wakati wa uteuzi wa Kitila, alisema: “Tofauti ni kwamba Kitila alikuwa nchini wakati uteuzi unafanyika na tulipata muda mrefu wa kuzungumza na kujadiliana na kukubaalina kabla sijatoa maoni.”

Naye Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema kuna mambo mawili ya msingi yakijumuisha suala binafsi na la kichama.

“Mtu unapoteuliwa, linateuliwa jina la mtu kwamba Kitila Mkumbo, Anna Mghwira umeteuliwa kwenye nafasi fulani, kwa hiyo wao kwa mtu mmoja mmoja wanayo nafasi ya kufanya uamuzi wanaoona unafaa kwa wao wenyewe,” alisema.

Shaibu alisema pamoja na chama hicho kuwa na wanachama wengi, lakini katika ngazi ya chama uteuzi huo ni changamoto kwa kuwa wanaondoka viongozi wakubwa waliokuwa mihimili.

“Lakini katika ngazi ya chama, sisi ni chama cha siasa cha upinzani na Rais Magufuli aliyefanya teuzi hizi ni Rais wa Jamhuri, lakini pia Mwenyekiti wa CCM, kwa hiyo mbali na wao kuwa na uamuzi wao na kwamba nafasi wanazoteuliwa ni za kwenda kuhudumia wananchi, lakini kwetu ni changamoto kwa maana mnaondokewa na viongozi wakubwa ambao walikuwa mihimili, ukitazama watu wanne, watano waliokuwa mihimili ya ACT, huwezi kuwatoa Mghwira na Kitila,” alisema Shaibu.

Kuhusu uteuzi huo ulivyopokewa, alisema kumekuwa na dhana mbalimbali ambazo si rahisi kuzikwepa.

“Mfano uteuzi wa sasa, imezoeleka, nasema ni mazoea tu kwamba Mkuu wa Mkoa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, lakini pia ndani ya CCM wao wenyewe walishajipangia kwa taratibu zao kuwa mmoja wa wajumbe wa vikao vya mkoa ni pamoja na RC, kwa hiyo wamezoea hivyo kuwa ukiwa mkuu wa mkoa unakuwa sehemu ya CCM. Hilo nasema ni mazoea kwa kuwa katiba na taratibu za CCM hazibani watu wote Tanzania, zinawaongoza wana CCM,” alisema.

Hata hivyo Shaibu alisema jambo hilo linabaki kuwa mtego kwa upande mwingine na kushauri asubiriwe Mghwira mwenyewe azungumzie uteuzi wake.

Gazeti hili lilimtafuta Mghwira kwa simu ya mkononi, lakini hakupatikana kutokana na namba zake kutopatikana na Shaibu alisema kiongozi huyo alikuwa nje ya nchi kuhudhuria kongamano la wanawake.

Shaibu alisema Mghwira angekuwapo tayari viongozi wangekutana na kulijadili na kungekuwa na mwafaka.

Akizungumzia wimbi la wanachama wao kuondoka, alisema suala hilo lilikuwa la lazima kwa sababu lilikiweka chama hicho sehemu nzuri na huo ndiyo uadilifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles