24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aibua maswali matano kutekwa Mo

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameibua maswali matano kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’, huku akionesha kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi hadi sasa.

Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na Mo alivyofika Gymkhana na watekaji kuacha silaha zao, muda mfupi baadaye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kuonekana akinywa chai na mtekwaji huku aliyedaiwa kuhifadhi wahalifu hao akiwa hajafikishwa mahakamani hadi sasa.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri na makamishna wapya wa Jeshi la Polisi, alisema ameshangazwa kuona hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

 “Watanzania si wajinga, wanafahamu na wanajua ‘ku-analyze’ mambo, alipotekwa Mohammed tulipata ‘story’ nyingi, lakini lilipokuja kumalizika lile suala limeacha maswali mengi zaidi.

“Aliyetekwa alikutwa Gymkhana, alikwendaje pale, lakini bunduki ziliachwa pale, wakajaribu kuchoma gari, lakini baadaye tunamuona aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa maelezo hayapo.

“Lakini baada ya siku chache tunaelezwa nyumba alikokuwa ametekwa na aliyebeba watekaji huyu hapa, lakini baadaye kimya mpaka leo na miezi imepita.

“Tukio hili limeacha maswali mengi bila majibu, nikajiuliza labda ndiyo mambo ya kisasa kama lilivyo jina la Kamanda Mambosasa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Watanzania wanataka kuona hatua zinachukuliwa, lakini dosari ndogondogo zinalichafua Jeshi la Polisi.

“Watanzania wanataka kuona angalau huyo mmiliki wa nyumba akajibu, haya hata kama Watanzania wakinyamaza, lakini mioyo yao haitakaa kimya.

“Walitegemea huyo aliyeonyesha nyumba alimokuwa akiishi anapelekwa mahakamani kesho, lakini hakuna, mkilianzisha suala lazima limalizike,” alisema.

Alisema makamishna wapya na makamanda wengine wa Jeshi la Polisi lazima wajenge taswira nzuri ya jeshi hilo na akataka wachache wanaolichafua washughulikiwe.

“Usiogope IGP kubadili kamishna au kupunguza nyota zao wala usisite, ambao wanashindwa ‘ku–perform’ wasiwe kila siku wanapelekwa makao makuu, waende wakawe chini ya ma–RPC wengine,” alisema.

Rais Magufuli alisema hata kitengo cha Finacial Crime waliamua kivunjwe na kuelekeza wakuu wa polisi katika wilaya za Rombo, Tanga na Pangani watolewe kwa madai ya kujihusisha na biashara ya magendo.

MO ALIVYOTEKWA

Mo alitekwa alfajiri ya Oktoba 11 alipokuwa akielekea katika Gym ya Hoteli ya Colosseum iliyoko Oysterbay, Dar es Salaam na aliachiwa usiku wa manane wa Oktoba 20, mwaka jana.

Kulingana na taarifa za awali zilizotolewa na polisi, watekaji hawakuwa Watanzania, wawili kati yao walikuwa wanaongea Kingereza chenye lafudhi sawia na za nchi za kusini mwa Afrika na mmoja alikuwa akiongea Kiswahili kibovu.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Naibu wake, Hamad Masauni, kwa nyakati tofauti walikaririwa wakisema vyombo vya ndani vya ulinzi vina uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Jumla ya watu 26 walikamatwa kutokana na tukio hilo na baadaye 19 waliachiwa kwa dhamana.

Baada ya kukaa kimya kwa siku nne, familia ya Mo ilijitokeza na kutangaza kuwa watatoa zawadi ya Sh bilioni moja kwa yeyote atakayewapatia taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwake.

Mo anakisiwa kuwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni 1.5 kwa mujibu wa jarida la masuala ya fedha la Forbes na kumfanya kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki na bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika.

MAKAMISHNA WAPYA

Rais Magufuli alisema kazi ya kuwapata makamishna hao wa Jeshi la Polisi haikuwa nyepesi na ilibidi amuite waziri husika, katibu mkuu na mkuu wa Jeshi la Polisi na kuchambua kila jina.

“Kazi za kulitumikia taifa zinahitaji kujitoa, huwezi kuwa kamanda wa operesheni halafu askari wako kila siku wanapigwa risasi wanakufa. Leo wanakufa saba, kesho wawili halafu bado unajiita kamanda, sasa tuliona Sabas anafaa.

“Mkumbo kule Arusha kazi ilifanyika vizuri hadi ukaumia mguu na mkono, kila mmoja tunafahamu utendaji wake. RPC wa Shinyanga alifanya vizuri sakata la dhahabu na wa Simiyu na yule aliyekuwa anakaimu Arusha.

“Yule wa Mwanza ameponea chupuchupu, hawawezi watu kuiba dhahabu wewe unakwenda kujificha Ukerewe, lakini kwa sababu ya ‘performance’ yake tumesema ngoja tumuangalie ndio maana tumempeleka Arusha,” alisema Rais Magufuli.

Alisema watu wasitegemee kupata vyeo kwa sababu ni waandamizi bali watapata kutokana na utendaji wao.

“Vijana wadogo wadogo ambao wengi ni waaminifu msiwakatishe tamaa, anamshika mtu unamwambia muachie huyo, mnawadhalilisha,” alisema.

MABADILIKO MAWAZIRI

Rais Magufuli alisema mabadiliko ya mawaziri ni ya kawaida na amelenga kuboresha timu yake katika Baraza la Mawaziri.

“Wizara ya Mambo ya Nje inahitaji watu wa kuwasukuma sukuma ndiyo maana nimeamua kumpeleka Kabudi ili ‘diplomatic’ iliyopo pale ikaungane na sheria, nafikiri mambo yatakwenda vizuri.

“Wizara ya Katiba na Sheria uhitaji wote wawe wanasheria, lazima upeleke ‘diplomatic’ wakafanye kazi vizuri, hivyo ni ‘logic’ ya kawaida tu,” alisema Rais Magufuli.

Juzi Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo katika Bazara la Mawaziri kwa kuwabadilisha Dk. Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles