32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ahamisha umiliki wa Magomeni Kota

Pg 2Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

RAIS Dk.John Magufuli, amehamisha umiliki wa eneo la ekari 33 la Magomeni Kota   Dar es Salaam kutoka kwa Manispaa ya Kinondoni.

Kwa sababu hiyo,   viwanja hivyo sasa vitamilikiwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Rais pia  ameagiza kuhamishiwa Serikali Kuu, nyumba na maeneo  yote ya aina hiyo kote nchini, ambayo mwaka 1991 yalitolewa katika umiliki wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuhamishiwa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kauli hiyo ilitolewa   Dar es Salaam jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipozungumza na wakazi wa Magomeni Kota waliobomolewa nyumba zao.

Alisema Rais Magufuli  amefanya uamuzi huo baada ya Manispaa ya Kinondoni kushindwa kutekeleza mkataba wake kwa wananchi hao.

Lukuvi  alisema mwaka 2011 Manispaa ya Kinondoni iliingia mkataba na wakazi waliokuwa wamepanga katika eneo hilo kwa makubaliano ya kuliendeleza, kwa kujenga nyumba za kisasa ambazo zingeuzwa kwa wapangaji hao.

Kwa mujibu wa mkataba huo, halmashauri ilikubali kuwalipa wakazi hao fedha kwa ajili ya kulipia kodi baada ya nyumba zao kubomolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja, wakati nyumba mpya zikitengenezwa

“Baada ya wakazi wa Magomeni kuleta malalamiko yao niliyafanyia kazi kwa   mwezi mmoja na sasa Rais  ameagiza eneo hilo lichukuliwe na kuendelezwa na Serikali Kuu kupitia wizara yangu.

“Pia ameagiza nyumba na maeneo yote ya aina hii kote nchini ambayo yalikuwa chini ya Tamisemi yarudishwe Serikali kuu na yaendelezwe,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema kwa  eneo la Magomeni,   Rais Magufuli, ameagiza Serikali Kuu iliendelezw eneo hilo kwa kujenga nyumba za makazi na kuwauzia waliokuwa wapangaji wa nyumba hizo.

Alisisitiza kwamba serikali imefuta hati na mikataba yote ya sasa inayohusu eneo hilo na   wakazi watakaonunua nyumba hizo watapewa kila mmoja hati yake ya kumiliki nyumba.

Waziri alisema  wataalamu wa wizara yake wameshapima eneo hilo na wameanza kutengeneza mchoro wa majengo yatakayojengwa.

“Wataalamu wangu wamekwishaanza michoro ya majengo hayo ambayo yatakuwa ni ghorofa zenye nyumba 644 za vyumba vitatu vya kisasa na zitauzwa kwa kuwapa kipaumbele wakazi waliokuwa pale,” alisema Lukuvi.

Alisema baada ya kukamilika  mchoro atakutana tena na wakazi hao ili wakubaliane bei ya kununulia nyumba hizo na kwamba zitakuwa za gharama nafuu kwa vile  hazitajumuishwa gharama ya ardhi.

Lukuvi alisema serikali inaendelea kutafuta fedha za kujenga nyumba hizo huku akiwahimiza wakazi hao kutoa fedha zao mapema   ziweze kusaidia ujenzi wa nyumba hizo  haraka.

“Mwenyekiti wenu aliniambia mpo tayari kutoa fedha mtakazoambiwa za kununulia nyumba hizo hivyo wakati serikali inatafuta fedha hizo mnaweza mkaamua kutoa fedha zenu mapema tukaanza ujenzi,” alisema Lukuvi.

Wakili wa Wakazi hao, Twaha Tasilima, alimshukuru Rais Magufuli kwa kumaliza tatizo hilo na kusisitiza kuwa agizo hilo linatakiwa kuwekwa katika maandishi rasmi ili yakasajiliwe mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles