28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM afufua ufisadi wa rada

*Akumbusha Waziri Uingereza alijiuzulu ila wa Tanzania hakufanya hivyo

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amekumbushia kashfa ya ununuzi wa rada ya kuongoza ndege kutoka Kampuni ya Bae System ya Uingereza mwaka 2002, ambayo ilinunuliwa kwa gharama kubwa zaidi ya uhalisia.

Katika kashfa hiyo, Uingereza ndiyo iliyobaini mchezo huo mchafu na kufanya uchunguzi uliosababisha Novemba 2013 Tanzania irejeshewe Dola za Marekani milioni 29.5 sawa na Sh bilioni 73.

Kutokana na kashfa hiyo, aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Andrew Chenge alijiuzulu kutokana na ununuzi huo kufanywa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Chenge alijiuzulu baada ya tuhuma dhidi yake za kujilimbikizia fedha kuchapishwa na gazeti la The Guardian la Uingereza, ambalo lilieleza kuanza kwa uchunguzi dhidi yake baada ya zaidi ya Dola za Marekani milioni moja kukutwa katika akaunti yake.

ALIYOZUNGUMZA JPM

Jana, wakati akizindua rada za kuongoza ndege Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Rais Magufuli alikumbushia kashfa hiyo akisema lazima aseme ukweli Tanzania ilikotoka na inakokwenda.

Alieleza kushangazwa kwa hatua ya watendaji serikalini wakati huo waliohusika katika kashfa hiyo kutojiuzulu wakati waliohusika kwa upande wa Uingereza walijiuzulu.

Katika hilo, alisema baadhi ya viongozi hao hao waliohusika katika kashfa hiyo wamekuwa wakosoaji wakubwa katika Serikali yake anayoiongoza, huku wakiwa wamesahahu uchafu walioufanya huko nyuma.

“Mheshimiwa Spika (Job Ndugai) naye kakumbushia machungu ambayo tumeyapata nchi yetu, fedha ilipangwa kununua rada, mabilioni ya fedha ya kununua rada moja wala haikuwa nne, lakini haikununuliwa, tukapigwa.

“Lakini hawa TCAA chini ya uongozi wa wizara pamoja na Johari (Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Hamza Johari) zimetumika Sh bilioni 67 tu, tunakuwa na rada nne ambazo zinaona nchi nzima kwa Sh bilioni 67.

“Wakati ule ilikuwa inunuliwe rada moja, nayo haikufika, aliyehusika kule Uingereza alijiuzulu, wa kwetu hakujiuzulu, sifahamu labda watajiuzulu siku zinazokuja na inawezekana ndio wamekuwa wakosoaji wakubwa, wamesahau uchafu walioufanyizia katika nchi yetu.

“Nayasema haya kwa uchungu na wakati mwingine ninapoyasema haya yawezekana wana tafsiri tofauti, lakini lazima tuseme ukweli ili tujue tulikotoka na kule tunakoenda, kwa hiyo kwa kweli Johari wewe ni Johari kweli katika kazi.

“Hili nalisema kwa dhati bila unafiki, hata ukimwangalia unaona mtu anazungumza ‘point’ tupu, ningekuwa na binti hata ungeoa,” alisema Rais Magufuli.

NDEGE ILIYOZUILIWA

Akizungumzia kuhusu ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220-300 iliyozuiliwa nchini Afrika Kusini katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo na baadaye kuachiwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Guteng, alisema ni wivu wa watu kwa sababu wameona Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linafanya vizuri.

Mwezi uliopita ndege hiyo ilizuiliwa nchini Afrika Kusini baada ya mkulima Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya Dola za Marekani milioni 33, hata hivyo Serikali ya Tanzania ilishinda kesi hiyo bila kutoa fedha yoyote.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli aliwatoa hofu Watanzania kuhusu mwenendo wa ATCL akisema inafanya vizuri na kwamba ndege zote ziko salama.

Vilevile alisema mradi wa rada hizo utaleta manufaa makubwa ikiwemo kuboresha huduma za ndege, hasa katika kipindi hiki Serikali ilivyojizatiti kuimarisha usafiri wa anga nchini ikiwemo kufufuka kwa ATCL.

“Na hapa nataka niwaambie shirika letu linaendelea vizuri sana ndiyo maana mkisikia watu wakikamata ndege yetu msishangae sana ni kwa sababu shirika letu linafanya kazi nzuri.

“Lakini hii kwangu ni sawa na kelele za chura ambazo hazimzuii ng’ombe kunywa maji akiwa na kiu… saa nyingine huwa naukumbuka wimbo, nafikiri sauti ya Solo (wimbo wa wasanii wa Kenya wa kundi la Sauti Soul) anasema wao wakifunika wengine wanafunua, yaani hawazuiliwi kufanya kitu. Sisi tupo hivyo, wakijaribu hivi tutafanya hivi ili nchi yetu ifike tulikopanga,” alisema Rais Magufuli.

Aidha alisema awali ATCL ilikuwa ikishikilia asilimia 3 ya soko la ndani, lakini sasa hivi ni asilimia 75 pamoja na kuingia katika soko la kimataifa kwa kwenda nchi mbalimbali. 

“Safari hizi zitachangia kukuza sekta ya utalii, kwa mafanikio haya lazima watajitokeza watu wenye wivu ambao hawakosekani. Lakini hatutakubali mtu yeyote alichezee shirika na Tanzania lazima tufike tunakotakiwa kufika,” alisema Rais Magufuli.

Vilevile alimsifia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Anga Tanzania (TCAA), Johari kutokana na kufanikisha kwake mradi wa ufungaji wa rada katika viwanja viwili vya ndege nchini.

Viwanja hivyo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (Kia). Songwe na Mwanza utekelezaji wake bado unaendelea.

“Johari safi sana, hii ndiyo mifano ya vijana wanaojituma. Sina zawadi ya kukupa, lakini mwaka huu ukiamua kwenda Hijja nitakulipia ili ukamshukuru Mungu kwa utendaji wako.

“Aprili mwaka huu tulikutana hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa rada nne, leo tumekutana kwa ajili ya kuzindua rada iliyosimikwa hapa JNIA.

“Nimefurahi sana, wote mnajua mimi sipendi miradi inayoishia njiani, hasa ninayoiwekea jiwe la msingi. baadaye unaambiwa haujakamilika,” alisema Rais Magufuli.

MRITHI WA LISSU

Wakati huo huo, Rais Magufuli alitumia pia uzinduzi huo kumpongeza Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM), akisema jimbo hilo lilikuwa limetelekezwa na Tundu Lissu.

Mtaturu ambaye alichaguliwa hivi karibuni kuwa mbunge wa jimbo hilo, naye alihudhuria uzinduzi huo akiwa kama mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu.

“Nimefurahi kumwona hapa kwenye Kamati ya Miundombinu mbunge wa CUF (hakumtaja jina), lakini pia na mheshimiwa nani yule wa lililokuwa jimbo lililokuwa limetelekezwa…sasa ameshika huyu, safi kabisa, hongereni, mpigie makofi na nakuahidi Serikali yangu tutashughulikia maji katika jimbo lako,” alisema Rais Magufuli.

UTEKELEZAJI MRADI WA RADA

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Johari, alifafanua kuhusu utekelezaji wa mradi wa rada mbili za kuongoza ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na ule wa Kilimanjaro (Kia).

Alisema eneo la kwanza ni shughuli zilizofanyika Ufaransa na Uingereza zikihusisha uundaji mitambo, majaribio ya kiwandani na kusafirisha mitambo kuja nchini.

Vilevile alisema shughuli nyingine ni mafunzo kwa wahandisi na waongozaji ndege walioyapata nchini Ufaransa na chuo cha kuongezea ndege cha Afrika Kusini huku wataalamu 53 wakipata mafunzo hayo, kati yao 12 wakipata mafunzo ya ukufunzi.

Alisema shughuli zilizofanyika nchini ni ujenzi wa majengo katika kituo cha Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro na usimikaji wa mitambo kwenye vyumba vya kuongozea ndege ambao umeshakamilika.

“Mradi huu ulihusisha kuunganisha mfumo unaoainisha mifumo mingine ya kusimamia anga iliyopo sanjari na mfumo wa ukokotoaji wa ankara,” alisema Johari.

BALOZI WA UFARANSA

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederick Clavier, alisema nchi yake inaunga mkono juhudi za kuimarisha uchumi wa viwanda utakaosaidia kufikisha taifa kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Mradi huo wa rada umetekelezwa na mkandarasi Thales Air Sytem (SAS) kutoka Ufaransa na rada mbili zikazotumika kuongozea ndege kwenye viwanja vya JNIA na KIA umekamilika huku zingine zikiwa kwenye mchakato.

SPIKA WA BUNGE

Awali, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema huko nyuma rada ilipangwa kununuliwa, lakini ununuzi wake ulikuwa na mapungufu makubwa na baada ya kelele nyingi kupigwa ndipo wabunge wanne wakaenda Uingereza kuishawishi Serikali ya Uingereza ili fedha hizo zirudi.

 “Sina nia ya kurudia kilichotokea, lakini baada ya juhudi mbalimbali kushindikana wabunge wanne akiwemo Mussa Zungu, John Cheyo, Angella Kairuki pamoja na mimi wakati huo nikiwa naibu spika tukaenda Uingereza.

“Kwakweli tulifanya kazi kubwa sana kwa muda wa mwezi mmoja, tukaishawishi Serikali ya Uingereza na Bunge kuhusu umuhimu wa kurudishwa zile fedha na kweli baadaye fedha zile zikarudi.

“Yapo mambo huwa hayasemwi, lakini ni muhimu kwa nchi yetu na sasa mambo yamebadilika kwa kweli, kwamba rada nne zimenunuliwa na hakuna ufisadi wowote uliofanyika,” alisema Spika Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles