24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

JPM AFIKIRIA KURUHUSU VPL

 ZAINAB IDDY –DAR ES SALAAM 

WAKATI Mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba wakisubiri kwa hamu timu yao kutangazwa mabingwa wa msimu huu, Rais wa Jamuhuri ya Muungamo wa Tanzania, John Magufuli, amesema anafikiria kuruhusu ligi ziendelee. 

Ikumbukwe kwamba, Machi 17 mwaka huu Serikali ilipiga marufuku shughuli zinazosababisha mikusanyiko ya watu ikiwemo michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona. 

Hatua hiyo ilililazimisha Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) na Bodi ya Ligi(TPLB)kusimamisha Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza(FDL),Ligi Daraja la Pili(SDL) na mashindano mengine yaliyo chini yao.

Wakati Ligi Kuu inasimama, timu ya Simba ndiyo ilikuwa inakamata uongozi katika msimamo ikiwa na pointi 71, huku Azam inayofuata kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 na Yanga iliyopo nafasi ya tatu na pointi 51, lakini ina mchezo mmoja mkononi. 

Kutokana na janga la corona kuendelea kutishia maisha ya watu huku likisababisha vifo vya maelfu ya watu duniani, baadhi ya vyama na mashirikisho la soka ya nchi yamelazimika kuwatangaza mabingwa wa ligi zao kwa kuangalia nani yuko nafasi ya kwanza. 

Kwa hapa nchini, baadhi ya wadau wa soka wametaka TFF nayo ichukue hatua kama hiyo kwa kuitangaza Simba kuwa bingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu. 

 Chama cha Soka cha nchi jirani ya Kenya (FKF), siku chache zilizopita kilitangaza timu ya Gor Mahiya kuwa mabingwa wa ligi ya nchi hiyo, ikitumia kigezo cha nafasi yake kwenye msimamo ambayo ilikuwa inaongoza ikiwa na pointi 54, baada ya kushuka dimbani mara 23.

 Lakini pia ikitokea Ligi Kuu Bara itafutwa na Simba kupewa ubingwa, timu za Singida United, Mbeya City, Mbao na Alliance zitakuwa hatarini kushuka daraja kutokana na kuwa nafasi za chini kwenye msimamo.

Akihutubia Taifa kutoka mkoani Geita, wakati wa tukio la kumuapisha Mwingulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi ya marehemu Agustino Maiga aliyefariki wiki iliyopita, Rais Magufuli alisema kama ataruhusu ligi kuendelea basi wapenzi wa soka watalazimika kutazama mechi kupitia runinga.

Alisema anafikiria kuchukua uamuzi huo baada ya kubaini wanamichezo si waanga wakubwa wa corona, sababu inayotokana na mazoezi wanayofanya.

“Hii inadhirisha wanaofanya mazoezi corona inawakwepa,kuzuia ligi isiendelee ni kuwafanya wanachezaji kupata virusi hivyo.

“Nasubiri wataalamu wangu wanishauri vizuri kwanza ili ligi iendelee kuchezwa, kwa sababu upo uwezekano tukaishi na corona kama vile tunavyoishi na virusi vya Ukimwi, naomba tusitishane juu ya virusi hivi tunatakiwa kuchapa kazi,”alisema Dk Magufuli.

Wakati huo huo, kwa taarifa ambazo MTANZANIA ilizipata kutoka ndani ya TFF zinadai kuwa, ikiwa Serikali itaruhusu ligi kuendelea, itataanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi huu.

“Kama serikali itaruhusu ligi kuendelea tutaanza mwisho wa mwezi huu na kila timu itatakiwa kucheza mechi tatu ndani ya wiki moja ili kumaliza kabla ya Julai, kipindi ambacho ligi zinatakiwa ziwe zimesimama na kuruhuszu kuanza kwa usajili wa msimu 2020/21 ambao tukienda vizuri utaanza kama kawaida mwishoni mwa Agosti,”alisema mtoa habari huyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles