27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aeleza sababu za kumteua Bashe

*Asema amevutiwa na uchambuzi wake bungeni

*Amtaka Simbachawene akasimamie maeneo matatu muhimu

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameeleza sababu za kumteua Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na kumpa maagizo ya kuiboresha sekta hiyo.

Juzi Rais Magufuli alimteua Bashe kujaza nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye mwezi uliopita aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Pia alimteua Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) baada ya kutengua uteuzi wa January Makamba.

Akizungumza jana Ikulu Dar es Salaam,  wakati wa kuwaapisha mawaziri hao, Rais Magufuli alisema ana imani na Bashe kutokana na michango ambayo amekuwa akiitoa bungeni kuhusu kilimo kinavyoweza kuleta manufaa nchini.

“Bashe nakupongeza kwa kuchaguliwa naibu waziri wa sekta ambayo ni muhimu sana, nimekuwa nakusikiliza sana bungeni michango yako imekuwa ni mizuri.

“Unatoa ‘analysis’ (uchambuzi) ya namna kilimo kinavyoweza kuleta manufaa katika uchumi wa nchi yetu, ‘analysis’ zile ‘zimeni–impress’, nilizipenda, sasa zile zilikuwa za bungeni, nataka sasa ukaziweke kwenye ‘practical’ (vitendo).

“Ndiyo maana nimekuweka kwenye wizara ya kilimo, hayo yote ya ‘theory’ (nadharia) uliyokuwa ukiyazungumza bungeni na tukafurahia, sasa yakawe kwenye ‘practical’ (nadharia).

“Na mimi nina matumaini makubwa kwa sababu huwezi ukazungumza tu ‘theory’ (nadharia) halafu ‘practical’ (vitendo) ikakataa, ni matumaini yangu kwamba yale ambayo uliyafikiria, umeyashauri, sasa kayatekeleze,” alisema Rais Magufuli.

Alisema sekta ya kilimo ni muhimu, lakini ina changamoto nyingi na wizi mwingi, hivyo akaitaka Wizara ya Kilimo kuwasimamia wakulima wanyonge na kushirikiana na wizara nyingine kama ya biashara na Jeshi la Magereza kuzimaliza.

“Mtapigwa vita, mtazungumzwa, nendeni muyavumilie mumuachie Mungu, kashirikianeni na wanyonge, nina uhakika mtafanya makubwa,” alisema.

Alitolea mfano wa Bodi ya Sukari ambayo alisema imekuwa ikifanya kazi nzuri, lakini inapigwa vita na wafanyabiashara wa sukari ambao walizoea kuitumia kwa masilahi yao.

“Inapigwa vita sana na nilikuwa nasubiri tu waziri aivunje na yeye angekipata cha mtema kuni, lakini hajaivunja,” alisema.

Aliitaka wizara hiyo pia kwenda kusimamia mazao ya kilimo yalete faida na wananchi ili wapate utajiri kutokana na kilimo.

BEI YA KAHAWA

Kuhusu bei ya kahawa, alisema wawekezaji ni lazima wanunue kwa Sh 1,500 na kuendelea na akaagiza wafanyabiashara wachache ambao wameanza kuwadanganya wananchi wasiiuze washughulikiwe bila kuonewa huruma.

“Pamba kilo ni kuanzia Sh 1,200 na si chini ya hapo, wakinunua wafanyabiashara na wakawakopesha, mkampata mtu mwingine ambaye anataka kuwalipa iuzeni,” alisema.

KILICHOMPONZA MAKAMBA

Mkuu huyo wa nchi pia alitaja sababu zilizosababisha amng’oe Makamba kuwa ni ucheleweshaji wa utoaji vibali kwa wawekezaji, kutotekelezwa haraka kwa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na Idara ya Mazingira kutokuwa na matokeo licha ya kuwa na fedha nyingi zikiwemo za wafadhili.   

“Idara ya Mazingira fedha nyingi zinapelekwa, lakini ‘impact’ (faida) yake haionekani, fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili haziwi ‘reflected’ (haziakisi) kwenye miradi husika.

“Kuna miradi hewa, Rufiji walisema ilipandwa mikoko, lakini haipo, nataka haya (Simbachawene) ukayashughulikie,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu vibali, alisema kumekuwa na ucheleweshaji na kutaka wawekezaji wasiwekewe vipangamizi kwa visingizio vya Nemc na ikiwezekana wawekeze kwanza halafu vibali vitakuja baadaye.

“Nimekuwa nikipata matatizo sana katika suala hili, mpaka uzungumze ndiyo unasikia kimetolewa baada ya siku tano, unajiuliza kwanini hakikutolewa mwaka mzima uliopita.

“Pasiwe na ucheleweshaji wa kutoa vibali kwa viwanda vyetu, sisi tunataka kuwa na viwanda vya kutosha,” alisema.

Akizungumzia suala la mifuko ya plastiki, alisema limechukua muda mrefu licha ya kusaini utekelezaji wake miaka minne iliyopita, hadi alipoamua kutoa amri ya lazima.

“Mifuko ya plastiki lilichukua muda mrefu, miaka minne nikasaini halikutekelezwa, makamu wa rais, waziri mkuu akaenda kuzungumza bungeni halikutekelezwa mpaka mwishoni nilipotoa amri ya lazima ndiyo likatekelezwa, sasa usiende kufanya hivyo, wewe (Simbachawene) kayatekeleze haya kwa sababu ndio yale uliyoyaapa,” alisema.

Rais Magufuli pia alimtaka Simbachawene kusimamia vizuri suala la muungano na kuwa chachu ya kuuimarisha badala ya kuwa chachu ya kuuharibu.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema anatarajia kukutana na wafugaji wote nchini ili kujua changamoto zinazowakabili na kuzishughulikia ufugaji uweze kuleta tija katika uchumi.

SIMBACHAWENE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Simbachawene, aliahidi kufanya kazi kwa bidii kuokoa uharibifu wa mazingira.

“Nafahamu kwamba nchi yetu inayo matatizo makubwa sana katika eneo la mazingira, ziko rasilimali fedha nyingi zinazoingia kupitia sekta binafsi na umma ambazo mara nyingi haziendi moja kwa moja kutatua matatizo ya mazingira, bali zinatumika katika utawala zaidi.

“Tunavyoona hali ya uharibifu wa mazingira kwenye maeneo tunayoishi vyanzo vya maji vinazidi kutoweka, misitu inatoweka, mito inakauka, mabwawa yanakauka, lakini fedha zinazoingia ni nyingi, lakini hazitatui matatizo yanayoendelea,” alisema Simbachawene.

Alisema Wizara ya Mazingira ni wezeshi kwa sababu uchumi wa viwanda, kilimo, mifugo, utalii na shughuli zote zinategemea mazingira, hivyo atajitahidi kushirikiana na wenzake kuhakikisha wanafanya mambo kwa usahihi.

Kuhusu muungano, alisema msingi wake si yale yaliyoandikwa katika katiba, bali ni wa kihistoria, lakini unajengeka katika maelewano zaidi kuliko maandishi.

“Nafahamu umuhimu wa viapo, ukiapishwa leo utaendelea na kiapo hicho hata utakapokuwa nje ya utumishi, hiki cha leo (jana) ni kiapo changu cha tano, si jambo dogo, nitaendelea kuviheshimu viapo hivi hata nitakapokuwa nje, na hata katika uzee wangu,” alisema.

BASHE

Naibu Waziri wa Kilimo, Bashe, alisema atajitahidi kadiri ya uwezo wake kuhakikisha anatimiza majukumu aliyopewa.

“Nakushukuru sana (Rais Magufuli), nafahamu imani uliyoionesha kwangu na wananchi wa Jimbo la Nzega, hii maana yake ni utumishi na wala si heshima ya kwenda kuitwa naibu waziri. Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kutimiza wajibu wangu,” alisema Bashe.

Alisema alipokuwa katika Kamati ya Bajeti alipata elimu kubwa ya kufahamu changamoto zinazoikabili nchi, hasa sekta ya kilimo ambayo inaajiri kati ya asilimia 60 hadi 70 ya Watanzania.

“Ndiyo sekta ambayo inahudumia wanyonge, ninafahamu changamoto zinazoikabili sekta hii na sasa nitakwenda kujifunza na kuziona katika ‘field’.

“Tumekuwa tukiita kilimo cha kujikimu, lakini nafahamu kwamba kilimo ni biashara, kilimo ni maisha na uchumi wa nchi hii ambayo ni ndoto yako kujenga uchumi wa viwanda, ni lazima tuwatendee haki wakulima,” alisema Bashe.

MWELEKEO WA WIZARA

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema wako kwenye mchakato wa kuanzisha Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazomkabili mkulima na sekta hiyo kwa ujumla.

Aliyasema hayo jana wakati wa kikao kazi cha uongozi wa juu wa wizara hiyo kilichokuwa na lengo la kutoa taswira ya mwelekeo wa wizara, ambacho kilihudhuriwa pia na naibu mawaziri wa kilimo, Omary Mgumba na Hussein Bashe na Katibu Mkuu, Mathew Mtigumwe.

 “Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo na tayari tupo katika hatua za mwisho, hatuna sheria ya kilimo, na inayotumika sasa ni sera ya kilimo iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya,” alisema Hasunga.

Alisema sheria zinazotumika sasa ni za bodi za mazao mbalimbali ambazo pia zina changamoto zake na kwamba kuna mazao ambayo hayana bodi hali inayosababisha kushindwa kuwatetea wakulima wa mazao husika.

Mazao yaliyo katika utaratibu wa bodi ni pamoja na pamba, kahawa, chai, korosho, pareto na tumbaku kwa upande wa mazao ya biashara na yale ambayo hayana bodi ni ya chakula ambayo nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Kuhusu usajili wa wakulima wa mazao yote, aliziagiza bodi kuwapatia vitambulisho kuwatambua ili wanapofanyika kazi zao iwe rahisi kuwahudumia.

Waziri huyo pia alizungumzia umuhimu wa kuanzisha bima ya mazao itakayokuwa suluhisho kwa wakulima ambao kwa muda mrefu wamekosa utetezi pindi wanapopatwa na majanga kutokana na uchache wa mvua ama vinginevyo, jambo linalochangia kukosekana kwa mazao ya kutosha.

Aliwataka naibu mawaziri hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kutimiza azma ya Serikali ya kuimarisha uchumi wa wananchi na maendeleo kwa ujumla.

January NA NENO LA MWISHO

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January, aliwapongeza Bashe na Simbachawene kwa kuaminiwa huku akiwatakia heri na kuwaahidi ushirikiano wa dhati.

Katika ujumbe alioutoa jana kupitia ukurasa wake wa Twitter na kuupa jina ‘Neno la mwisho kwenye hili’ alisema; “Namshukuru rais kwa kuniamini, makamu wa rais kwa kunielekeza, waziri mkuu kwa kunisimamia, timu ya wizara, Nemc na mawaziri wote kwa ushirikiano.”

NAPE APONGEZA

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) alipongeza uteuzi wa Bashe na Simbachawane  ambao alisema ni bora.

“Uteuzi wa Hussein Bashe na Simbachawene ni katika teuzi bora kabisa, ninawapongeza na kuwatakia majukumu mema! Kaka January karibu ‘back bench’, hongera kwa utumishi wako,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles