25.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 31, 2023

Contact us: [email protected]

JPM aeleza dira uenyekiti SADC

NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

RAIS Dk John Magufuli ameanza rasmi safari ya mwaka mmoja ya kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), huku akiainisha dira yake na changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo.

Rais Magufuli alipokea uenyekiti huo jana kutoka kwa Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob, wakati wa mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo unaoendelea nchini na kuzishukuru nchi wanachama kwa imani waliyoionyesha kwake.

Akitoa hotuba yake ya kwanza kama mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Rais Magufuli alisema ajenda yake kubwa kama Mwenyekiti wa SADC ni kuwa na jumuiya ambayo itajikita na kuwekeza kwenye Viwanda.

Alisema mambo makuu atakayoyashughulikia ni pamoja na ujenzi wa viwanda, kukuza uchumi katika nchi wanachama, kuhakikisha amani, umoja na usalama vinaendelea kuwepo, kulinda rasilimali na Zimbabwe kuondolewa vikwazo vya kiuchumi na jumuiya za kimataifa.

 “Hii itatupa nafasi ya kutimiza malengo yetu kama inavyosema kauli mbiu yetu ya ‘Mazingira Wezeshi kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda, Ongezeko la Biashara na Ajira Kikanda’.

 “Nchi zetu si maskini, ni tajiri sana, tuna rasilimali za kila namna ukiacha watu milioni 327 wanaopatikana SADC, kuna rasilimali za mifugo, bahari, madini, misitu na nyingine.

“Tunachangia sehemu kubwa ya madini duniani, asilimia 26 ya dhahabu, asilimia 55 ya almasi, asilimia 21 ya shaba na asilimia 72 ya madini mengine inatoka kwetu hivyo, lazima tufanye kazi kwa ushirikiano kuhakikisha tunatumia rasilimali hizi kwa manufaa,” alisema Rais Magufuli.

Zimbabwe

Akizungumzia suala la Zimbabwe alisema imekuwa chini ya vikwazo vya kiuchumi kwa muda mrefu ambavyo vimeathiri karibu eneo lote la jumuiya hiyo.

“Jumuiya ya Kimataifa iondoe vikwazo ambavyo imeviwekea Zimbabwe, nchi hii imeshafungua ukurasa mpya na iko tayari kushirikiana na jumuiya zote. Nchi wanachama wa Sadc ziendelee kuzungumza kwa sauti moja kuhusu kuondolewa kwa vikwazo vya Zimbabwe,” alisema.

Alisema pia nchi wanachama zinatakiwa kuwa na dhamira ya dhati kufanya kazi na nchi nyingine kuhakikisha amani na usalama inakuwepo katika nchi zao.

Alisema amepata uzoefu wa kutosha kwa Rais Geingob ambao utamsaidia kutimiza majukumu yake mapya na kuzitaka nchi wanachama zisiwe na wasiwasi.

“Msiwe na mashaka Tanzania iko tayari kusimamia kanuni na mwelekeo wa SADC, jumuiya hii tunaiona ni muhimu ndiyo maana tumeendelea kuwa mwanachama hai.

“Nitajitahidi kutumia uwezo wangu wote kuimarisha zaidi ushirikiano ndani ya ukanda huu na naamini Mungu atanisaidia,” alisema.

Hata hivyo alisema licha ya bara hilo kuwa na amani kuliko mabara mengine, haimaanishi kwamba halina kabisa migogoro kwani katika baadhi ya nchi kuna matishio ya kigaidi, mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame, njaa na magonjwa.

“Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja kushughulikia changamoto hizo kwani amani na usalama ndio msingi muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi,”alisema Rais Magufuli.

Ukuaji mdogo wa uchumi

Rais Magufuli alisema mwaka jana walijwekea mkakati wa kuwa na ukuaji uchumi wa asilimia 7 lakini lengo hilo bado halijafikiwa ambapo umekua kwa asilimia 3.1.

“Mwaka 2005, 2006 na 2007 ukuaji wa Pato la Taifa ndani ya Jumuiya lilikuwa kwa asilimia 6.6 (2005), 7.3 (2006) na 8.0 (2007) lakini mara baada ya hapo ukuaji wake haukuwa wa kuridhisha ambapo mwaka 2012 ilikuwa (4.4), 2013 (4.3), 2014 (3.4), 2015 (2.2), 2016 (1.4), 2017 (3.0) na 2018 (3.1)” alisema Rais Magufuli.

Alisema ili kuweza kukuza uchumi nchi za SADC, viongozi wa mataifa hayo hayana budi kuwa na viwango, sera, sheria na kanuni za pamoja zinazotoa fursa kwa nchi hizo kuwa na mfumo wa pamoja utakaowezesha jumuiya hiyo kuweza kubadilishana ujuzi, uwezo na kuuziana bidhaa na kuondoa masharti mepesi yatakayorahisha ukuaji wa uchumi.

Alisema pamoja na jumuiya hiyo kujiwekea malengo kwa kila nchi za jumuiya hiyo kukuza uchumi wake angalau kufikia kiwango cha asilimia 7 mwaka 2018 kwa kila nchi, ni nchi chache zilizofanikiwa kufikia kiwango hicho, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinafikiwa kwa nchi zote.

 “Wakati wa kubadilisha SADC iliyokuwa na C mbili (akimaanisha Mkutano wa Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika) na kuunda SADC yenye C moja (Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika), viongozi walikuwa na lengo moja kutumia mafanikio ya kisiasa kufikia mafanikio ya kijamii na kiuchumi. Lakini lengo hili halijafikiwa hivyo, kunahitajika jitihada kubwa kuweza kulifikia.

“Kama sekretarieti itafanya kazi kwa ufanisi na mafanikio ingepata majibu kwanini kwa miaka 10 uchumi wetu wa ndani unaendelea kuporomoka, haya ndiyo masuala ya msingi ambayo sekretarieti lazima iyashughulikie na kushauri wanachama kwa mwelekeo mpya,” alisema Rais Magufuli.

Ujenzi wa Viwanda

Rais Magufuli alisema kukosekana kwa viwanda katika nchi nyingi kumesababisha zishindwe kunufaika kibiashara na kubakia kuuza malighafi hali iliyosababisha kupunguza fursa za ajira.

Jumuiya hiyo imedhamiria kuwa na uchumi wa viwanda ambapo inao mkakati wa viwanda wa SADC wa 2015 – 2063 ambao unatekelezwa kwa awamu tatu yaani 2015 – 2020, 2021 – 2050 na 2051 – 2063.

“Hakuna nchi ambayo imewahi kuendelea bila kupitia mapinduzi ya viwanda, karibu asilimia 60 ya bidhaa kutoka SADC ni malighafi hasa za kilimo na madini, ndiyo maana watu wetu wanaendelea kuwa maskini kwa sababu malighafi inauzwa kwa bei ndogo. Tunasababisha ajira ziende kwingine hivyo tujielekeze katika uchumi wa viwanda,” alisema.

Taarifa za Biashara

Rais Magufuli alisema nchi za SADC zina fursa kubwa ya kuwa na rasilimali nyingi za asili ikiwemo ardhi yenye kilomita za mraba milioni 9.8 na idadi ya watu milioni 327 lakini bado hazijanufaika kibiashara kulinganisha na mabara mengine duniani.

Alisema mwaka 2017 jumuiya hiyo iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 143 wakati Mexico na Vietnam zenye kilomita za mraba 331,210 na watu milioni 230 waliuza bidhaa zenye thamani ya Dola bilioni 617.

“Hii inaonyesha wazi kwamba uchumi wetu hauendi vizuri na tuko mbali na malengo yetu ya kiuchumi, na hili nalisema wazi,” alisema.

Aliongeza kuwa malengo ya pamoja yanapaswa kuwekwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo ikiwemo kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa taarifa za biashara ambazo mataifa mengi ya Asia yamekuwa yakitumia fursa hiyo pamoja na kuimarisha na kujenga viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa vitavyowezesha kupunguza gharama za ununuzi wa bidhaa kutoka nje ya Jumuiya hiyo.

Rais Magufuli alitoa mfano kuwa Mei mwaka huu alitembelea nchi nne za SADC na kushangaa baadhi yake zilikuwa na mpango wa kuagiza chakula kutoka nje ya Afrika wakati Tanzania ina tani milioni 2.5 za chakula cha ziada.

Alitaja vikwazo vingine vya kibiashara kuwa ni gharama kubwa za uagizaji bidhaa akisema kuwa ni kubwa zaidi kuliko nchi za Asia na tofauti za kisera katika baadhi ya nchi.

“Mfano leo inawezekana bidhaa inayokubalika katika nchi moja lakini ikakataliwa katika nchi nyingine kwamba haijafikia viwango vya ubora. Kwanini hatuoanishi sera zetu…vinginevyo itakuwa ni ndoto kufikia malengo ya kiuchumi,” alisema Rais Magufuli.

RAIS GEINGOB

Rais Geingob alisema katika kipindi cha uongozi wake kulikuwa na changamoto za masoko, njaa na majanga yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi lakini bado jumuiya hiyo imeendelea kuwa na mafanikio.

Alisema tatizo la mabadiliko ya tabia nchi lilisababisha baadhi ya nchi kukumbwa na vimbunga Idai na Keneth ambavyo viliua zaidi ya watu 1,000 na kuathiri wengine 3,000 kuharibu miundombinu na ekari zaidi ya 80,000 na mvua nyingi katika eneo la Kwazulu Natal.

“Tathmini ya mahitaji ilifanyika katika nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe na mikakati ya kupunguza majanga kama hayo inatakiwa kupewa kipaumbele kwani yanaweza kuwa na athari kubwa kwa nchi zetu,” alisema Rais Geingob

Kwa mujibu wa Rais Geingob baadhi ya nchi tayari zimetangaza hali ya hatari zikiwemo Angola, Lesotho na Zimbabwe na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe kukabili mabadiliko ya tabia nchi ili kuwa na ukuaji wa uchumi endelevu na kutokomeza umaskini.

Rais huyo wa Namibia pia alihimiza kupiga vita ukataji miti, kuweka mikakati ya kutoa majawabu ya haraka yanapotokea majanga, vijana wapewe umuhimu mkubwa na kushirikishwa katika program mbalimbali za jumuiya hiyo, kuongeza kasi katika kutekeleza itifaki za Sadc na kuhimiza uanzishwaji wa viwanda.

“Vijana wengi wanakimbilia Ulaya kutokana na ukosefu wa ajira na kukumbana na matatizo mengi, hivyo tuna haja ya kuhimiza ushiriki wa vijana katika mikakati mbalimbali.

“Jitihada lazima zifanyike kufikia malengo yetu katika eneo la Sadc hususan uboreshaji maisha ya wananchi, tuainishe mikakati itakayoongeza uzalishaji wa viwanda katika eneo letu na kupunguza vikwazo vya biashara baina yetu,” alisema.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana alisema ni kukua kwa denmokrasia katika baadhi ya nchi hasa DRC, Eswatini, Madagascar, Malawi, Comoro na Afrika Kusini ambazo zilibadilishana madaraka kwa amani.

“Baadhi ya nchi zimekuwa zimeendesha chaguzi za amani kwa kuzingatia demokrasia, mabadilishano ya madaraka DRC ni mafanikio na hatua kubwa za kuimarisha demokrasia katika ukanda wetu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,315FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles