RAIS John Magufuli amesema nchi imeweka dhamira ya kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 pamoja na kuzalisha ajira kwa asilimia 40.
Kauli hiyo aliitoa jana Ikulu Dar es Salaam, alipokutana na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.
“Sasa nimeona niwaite waheshimiwa mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo tunaoutaka na mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda.
“Nataka badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji waje wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu wetu kupata ajira, Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu,” alisema Rais Magufuli.
Pia aliwataka mabalozi kutangaza na kuwavutia watalii kuja nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa nchini katika nchi wanazowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo ofisi za ubalozi na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.
Rais Magufuli aliwataka mabalozi kufanya kazi kwa juhudi, kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.
Aidha, Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma zinazotumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya lazima pamoja na kuwarejesha watumishi wasiokuwa wa lazima.
“Kuna wafanyakazi kwenye Balozi zetu hawana sifa, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani anapangiwa ubalozini. Wakati mwingine unakuta ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani,” alisema Rais Magufuli.