29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

JPM AAGIZA KUANGALIWA UPYA MKATABA TBC, STARTIMES

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


Rais Dk. John Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhakikisha anauangalia upya mkataba kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Kampuni ya Startimes.

Amesema endapo mkataba huo hauna manufaa afanye uamuzi kwa sababu  haiwezekani kila wakati kampuni hiyo kudai kupata hasara kila wakati.

Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipoitembelea  TBC ambako  alisema   anamuamini Waziri Mwakyembe kwa sababu  ni mwanasheria.

“Ninakuamini simamia na huu mkataba na Startimes, haiwezekani mtu mnaingia mkataba wa miaka mingi halafu faida wanapata wao.

“Kila siku unasema unapata hasara lakini upo mwezi wa kwanza wa pili halafu bado upo,  chukua hatua zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa,” alisema Rais Magufuli.

  Rais Magufuli alijionea jinsi miundombinu ya shirika hilo inavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za uchakavu na teknolojia duni.

Alisema Serikali itafanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya ya studio za kisasa za kurushia matangazo katika makao makuu ya nchi mjini Dodoma.

  Dk. Magufuli hivi karibuni alitoa Sh bilioni tatu kwa ajili ya kuisaidia TBC na alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk. Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo, kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.

Kuhusu maslahi ya wafanyakazi, aliwahakikishia kuwa Serikali itaboresha stahili zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo.

Alimuagiza Dk. Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho  zinazofikia Sh bilioni 1.285  ambazo wafanyakazi hao wanadai kuanzia Oktoba 2016.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles