30.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 7, 2021

JPM aadhimisha miaka 42 ya CCM kwa kutembelea vyombo vya habari vya chama

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ameadhimisha miaka 42 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutembelea Kampuni ya African Media Group (AMG), huku akisema Tanzania haiwezi kuwa soko la kuangalia vyombo vya habari kutoka nje, kwani vingi vimekuwa na mwelekeo hasi dhidi ya Tanzania.

Akizungumza jana baada ya kutembelea Kituo cha Channel Ten na Redio Magic vilivyo chini ya Kampuni ya African Media Group (AMG) ambayo ni mali ya CCM, Rais Magufuli alisema vyombo vya habari nchini vina wajibu wa kuzungumza masuala chanya.

 “Vyombo vya nje kamwe haviwezi kuzungumza ‘positive’ kila siku ‘there always negative’, sasa mna wajibu wa kuzungumza yaliyo ‘positive’,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Alivitaka vyombo hivyo kuwa mfano kwa kupanua uelewa wa Watanzania hasa kuhusu masuala ya kilimo, ufugaji na biashara.

“Ningependa nikimaliza uongozi wangu tuwe na mabilionea hata 50 lakini wanaolipa kodi, tuweke Tanzania kwanza na ninyi vijana ni wakati wenu wa kulijenga hili taifa,” alisema.

Akijibu kero mbalimbali zilizowasilishwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, Rais Dk. Magufuli aliahidi kuwapatia Sh milioni 100 kuwezesha ununuzi wa vifaa zikiwamo kamera.

“Huwezi kuwa na chombo halafu kinaonekana Dar es Salaam tu, tutakaa kwenye chama tuangalie namna gani tutatoa mtaji wa kutosha kusaidia hivi vyombo,” alisema.

Pia aliuagiza uongozi wa kampuni hiyo kufanya uchunguzi wa kina katika majengo yanayomilikiwa na CCM na lile litakalowapendeza wamjulishe ili waweze kuhama katika jengo la sasa.

“Sikujua hivi vitu vizuri vyote kama vinatoka kwenye jengo la ajabu kama hili (jengo chakavu). Mnisadie kufanya uchunguzi kwenye majengo yanayomilikiwa na CCM mtakalo litamani niambieni,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu nyongeza ya mishahara, Rais Magufuli alisema suala hilo litaangaliwa kwa wafanyakazi wote wa chama hicho kwani wengi wana mishahara midogo.

Aliwataka wafanyakazi hao kuzingatia sheria, katiba na maadili ya uandishi wa habari.

“Sijatoa mipaka yoyote, ni suala pana kidogo, vyombo vya habari vinatakiwa kuwa huru kuzungumza na kila mmoja azingatie sheria na maadili ya nchi yetu,” alisema.

Rais Magufuli pia aliutaka uongozi kuhakikisha wanabana matumizi kinachokusanywa kisiishie kwenye matumizi.

Awali Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya AMG, Theresia Mtewele, alisema jengo wanalotumia sasa wamepanga kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), lakini ni chakavu na kusababisha watumishi kufanya kazi katika mazingira magumu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (COTWU – T) katika kampuni hiyo, Mary Edward, alishauri uboreshwaji wa vyombo hivyo uende sambamba na kujali masilahi ya wafanyakazi kwani hawajaongezwa mishahara kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,424FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles