27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Joto lapanda NMB Marathon, ukaguzi njia wafana

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

JOTO la Mbio za Hisani za NMB Marathon 2022 zinazolenga kukusanya kiasi cha Sh milioni 600 kusaidia matibabu ya kinamama wenye Fistula nchini wanaotibiwa kwenye Hospitali ya CCBRT, limezidi kupanda baada ya kufanyika kwa ufanisi ukaguzi wa njia zitakazotumika ‘routes check’ hapo Septemba 24.

Huu ni msimu wa pili wa mbio hizo, ambazo zilianza kutimua vumbi mwaka jana, lengo likiwa ni kukusanya Sh bilioni 1 katika miaka minne, lakini mafanikio yaliyowezesha kukusanya Sh milioni 400 badala ya 250, yakaisukuma Benki ya NMB inayoandaa kupanga kumalizia Sh milioni 600 zilizobaki mwaka huu.

Ukaguzi wa njia zitakazotumiwa na wakimbiaji wa mbio hizo, ulifanyika Jumamosi ukihusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, zilizoanzia na kuishia Leaders Club Kinondoni jijini Dar es Salaam, mahali ambako ndiko zitakorindima mbio zenyewe hapo Septemba 24, ambako Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, atakuwa Mgeni Rasmi.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mratibu wa mbio hizo, Suleiman Nyambui, alisema majaribio ya ukaguzi wa njia yamekuwa na mafanikio kwa washiriki na kwamba matumaini yao kama waratibu ni kwamba, wanariadha watakaojisajili kushiriki mbio hizo watafurahia kutokana na maandalizi yaliyopo.

“Kumekuwa na mafanikio makubwa katika ukaguzi huu, na washiriki wameridhishwa sana na alama za barabarani zilizopo kila kona ya njia, vituo vya kupokelea maji ya kunywa.

“Changamoto ya hizi mbio mara nyingi huwa ni alama katika njia za kukimbilia kwa washiriki wa umbali tofauti, ila NMB Marathon hakuna atakayepotea, labda mtu aamue mwenyewe kujipoteza,” alisema Nyambui huku akiwataja Emmanuel Giniki na Failuna Matanga kuwa miongoni mwa watakaoshiriki.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akoonay, alisema ukaguzi huo ulioshirikisha zaidi ya wakimbiaji 100, umefanyika kwa ufanisi mkubwa, huku akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kujisajili katika matawi ya benki hiyo na mtandaoni ili kufanikisha ukusanyaji wa Sh milioni 600.

“Mbio hizi ni muendelezo wa zile za mwaka jana. Tuliweka lengo la kukusanya Sh bilioni 1, lakini mwaka wa kwanza tu tukapata Sh milioni 400, ufanisi uliotusukuma kuweka lengo la kukusanya Sh milioni 600 mwaka huu ili kumaliza lengo la miaka minne katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza.

Kiongozi mwanzilishi wa Klabu ya Mbio za Taratibu cha EFM, Maulid Kitenge, aliisifu NMB kwa uwekezaji katika maandalizi ya mbio hizo na kwamba ana uhakika wanariadha watakaoshiriki hapo Septemba 24, mwaka huu watafurahia kuwa sehemu ya tukio hilo linaloenda kurejesha tabasamu kwa kinamama wenye Fistula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles