JOSEPH OMOG: NITAFANYA KAZI NA MWENYE UWEZO SIMBA

0
913

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAKATI klabu ya soka ya Simba ikiendelea kusajili mastaa kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, ameeleza kuwa yupo tayari kufanya kazi na mchezaji yeyote atakayesajiliwa lakini kikubwa awe na uwezo wa kuisaidia timu.

Mpaka sasa Simba inatajwa kumalizana na wachezaji, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Aishi Manula, Shomari Kapombe, John Bocco, Jamal Mwambeleko, Ally Shomary na Emmanel Mseja, huku wakiwa mbioni kumsainisha aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma.

Usajili huo uliokwenda shule kwa Wekundu hao wa Msimbazi, huenda ukawa tishio katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao na michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Omog alisema hana tatizo na wachezaji wanaosajiliwa lakini yeye anahitaji watu wa kazi ambao watakikomboa kikosi hicho.

“Nilikabidhi ripoti ambayo ilielekeza ninachotaka, hivyo sina tatizo na wachezaji wanaosajiliwa lakini tutakutana wakati msimu wa maandalizi ya ligi kuu utakapoanza.

“Kwa usajili unaofanywa ni matumaini yangu kwamba nitakuwa na kikosi bora chenye wachezaji wenye uwezo na watakaojituma,” alisema Omog.

Alisema anafurahi kuona Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba inafanya kazi kwa nguvu kuhakikisha kinapatikana kikosi bora ambacho anaamini kitapambana ili kuiwezesha timu kutwaa mataji.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, amewaomba mashabiki kuwa watulivu katika suala la kumpata Ngoma kwani bado kamati inaendelea kulishughulikia.

Kaburu alisema wanafahamu kuwa Ngoma ni mchezaji mzuri na wanatamani awepo kikosini hivyo suala lake bado kidogo na litakapokamilika basi wataliweka wazi.

“Haraka haraka haina baraka, tatizo watu wanataka kila kitu kifanywe kwa haraka wakati mambo ya usajili yanahitaji kuwa na subira,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here