Na SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM
BALOZI wa mpira wa kikapu Tanzania, Jokate Mwegelo, kesho anatarajiwa kushuhudia mchezo wa Ligi ya Vijana (U-16), kati ya Don Bosco dhidi ya Msasani, utakaopigwa kwenye Uwanja wa JMK Park, Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA jana, Mkurugenzi wa Vijana Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Bahati Mgunda, alisema ujio wa Jokate katika mechi za kesho una umuhimu mkubwa hasa katika kuhamasisha wachezaji kucheza kwa viwango.
“Ligi yetu ya vijana itaendelea wikiendi hii ambapo tutakuwa na Balozi wa Kikapu Tanzania anayefahamika kwa jina la Jokate, ambaye pia ni mwigizaji na msanii wa kizazi kipya cha muziki hapa nyumbani.
“Ujio wa Jokate una umuhimu mkubwa hasa katika kuhamasisha timu zinazoshiriki ligi hii kujituma ili bingwa apatikane,” alisema Mgunda.
Mbali na hilo, Mgunda alisema Jokate atapata nafasi ya kuzungumza na wachezaji wa kike wa mchezo huo akiwamo nahodha Jescar Ngisaise, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuhudhuria mafunzo maalumu ya mchezo huo yatakayofanyika nchini Afrika Kusini.
Michezo mingine itakayochezwa kesho itaikutanisha timu ya Chang’ombe dhidi ya Muhimbili, ukifuatiwa na mchezo kati ya New York na Gerezani.