Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesitisha mafunzo ya JKT kundi la kujitolea kwa mwaka 2020-2021.
Hivyo, limewataka vijana ambao walikuwa bado hawajaripoti wasiende  kuripoti katika makambi waliyopangiwa mpaka hapo itakapotangazwa tena na wale ambao wamefika kurejea nyumbani.
Hayo yameelezwa jana Januari 19, 2021 na Kaimu Mkuu wa Utawala JKT, Kanali Hassan Mabena wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.
Kanali Mabena amesema mafunzo hayo yalikuwa yaanze hivi karibuni katika makambi mbalimbali nchini hivyo wameyasitisha kwa muda mpaka hapo itakapotangazwa.
Amesema kutokana na kusitishwa kwa mafunzo hayo JKT inawataka vijana wote ambao walichaguliwa na kuripoti makambini kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya JKT ya kujitolea warejee majumbani kwao.
Kanali Mabena amesema na wale ambao walikuwa bado hawajaripoti wasiende kuripoti katika makambi waliyopangiwa mpaka hapo itakapotangazwa tena.