28.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

JKT watakiwa kumaliza ujenzi wa Ikulu kwa wakati

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MAKATIBU wakuu na manaibu wa wizara mbalimbali wametembelea eneo inapojengwa Ofisi ya  Ikulu ya Chamwino jijini hapa  huku, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akilitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kumaliza ujenzi huo kwa muda uliopangwa.

Akizungumza jana wakati wa ziara hiyo, Kijazi alisema waliamua kuwapa kazi hiyo JKT kutokana na vigezo vya usalama, gharama, muda na ubora wa jengo.

Alisema wanapotumia  majeshi wanataka kazi ikamilike kwa haraka na mara zote Jeshi huwa halishindwi kazi.

Vilevile aliitaka JKT  kubana matumizi pale ambapo inawezekana bila kuathiri ubora wa jengo hilo kwa kuhakikisha linadumu kwa muda mrefu.

“Jengo la Ikulu tunalo pale (Dar es Salaam) na lina umri mkubwa tu, kwa hiyo hatutegemei jengo hili lililojengwa na jeshi letu baada ya miaka mitano tuanze kuona kasoro,”alisema.

Alisema walipowapa kazi hiyo waliamini kuwa ubora wa jengo hilo utafanana na ule wa Ikulu ya Dar es Salaam ama zaidi ya ule.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Suma JKT, Brigedia Jenerali Rajab Mabele, alisema kazi hiyo ilianza Februari 12 mwaka huu na inahusisha ujenzi wa jengo lenye ukubwa wa mita za mraba 9,340.

Alisema ujenzi huo umegawanyika katika majengo madogo sita na unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Desemba mwaka huu.

“Ujenzi huu hadi sasa tathimini ya msingi ni asilimia 97.4 na ujenzi wa jengo zima ni asilimia 35. Hapo awali ujenzi wa mradi huu ulikuwa na changamoto zilizosababishwa na hali ya hewa, mwaka huu mvua zilikuwa ni nyingi na hivyo kusababisha kuchelewa kuanza kazi kwa wakati,” alisema.

Hata hivyo, alisema changamoto hizo zimetatuliwa na ujenzi wa jengo hilo unaendelea kwa kasi.

Aliahidi kuwa jeshi hilo litaendelea kufanya kazi mchana na usiku ili kufidia muda wa miezi miwili uliopotea kutokana na changamoto mbalimbali.

Aidha, alisema wanaendelea na uboreshaji wa mazingira ya eneo hilo ambapo wameshapanda miti 5,600 kwenye eneo hilo.

Alishukuru Serikali kwa kuwapa miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo imewawezesha kununua magari, zana za kilimo, mitambo na kutoa gawio katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Hassan Abbas, alisema wamejiridhisha kuwa ujenzi unaendelea kwa kasi ambayo wanajeshi wanajenga mchana na usiku ili kukamilisha kazi hiyo Desemba mwaka huu.

Aidha, alisema Serikali imeshahamia jijini Dodoma na kwa takwimu za wiki iliyopita idadi ya wafanyakazi wa Serikali waliokwisha hamia jijini hapa imefikia 17,080.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles